TCRA yazungumzia maendeleo ya Postikodi Tanzania
Posted in
No comments
Thursday, August 23, 2012
By
danielmjema.blogspot.com
Prof. John Nkoma akuzungumza kuhusu maendeleo ya postikodi Tanzania katika mkutano na waandishi wa habari jana.
Katibu
Mkuu Wizara ya Mawasiliano, Saysnsi Na Teknolojia Dr. Florens Turuka
akitoa taarifa kuhusu mradi wa Postikodi kwa Mkoa wa DSM jana ktk
mkutano na wasndishi wa habari!
TAARIFA
YA DK. FLORENS TURUKA, KATIBU MKUU, WIZARA YA MAWASILIANO, SAYANSI NA
TEKNOLOJIA KWENYE MKUTANO WA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU HARAMBEE YA
KUCHANGIA UTEKELEZAJI WA MRADI WA ANUANI ZA MAKAZI NA SIMBO ZA POSTA
KATIKA MKOA WA DAR ES SALAAM UKUMBI WA KARIMJEE,
DAR ES SALAAM TAREHE 22/08/2012
Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Meya wa Jiji la Dar es Salaam,
Mameya wa Manispaa za Dar es Salaam
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam
Wakurugenzi wa Halmashauri za Manispaa za Dar es Salaam
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
Posta Masta Mkuu, Shirika la Posta Tanzania,
Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Takwimu ya Taifa
Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana.
Awali
ya yote, nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha
sisi sote kuwa na afya njema na hivyo kuweza kushiriki Mkutano huu wa
utoaji wa taarifa kwa umma kuhusu harambee ya kuchangia utekelezaji wa
mradi wa anuani za makazi na simbo za posta katika Mkoa wa Dar es
Salaam. Nawashukuru viongozi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa utayari
wao wa kutekeleza mfumo huu pamoja na wadau wengine ikiwemo Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Serikali
kupitia Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia imetoa agizo
katika Sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003, la kuanzishwa kwa anuani za
makazi na postikodi, ambapo kila mwananchi ataweza kujitambulisha kwa
kutumia jina la mtaa, namba ya nyumba pamoja na postikodi ya eneo
analoishi.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Katika
kutekeleza agizo la sera hii, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia iliiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kusimamia
utekelezaji wa mfumo huu, ikishirikiana na wadau mbalimbali. Kamati ya
Kitaifa ya Uratibu wa utekelezaji wa mfumo huu mpya wa anuani iliundwa.
Mwenyekiti wa Kamati hii ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi
na Teknolojia, na wajumbe wake ni Makatibu Wakuu kutoka:
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano – Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
Wizara ya Ardhi, Makazi Maji na Nishati – Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa – Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Wizara ya Fedha
Aidha, Wajumbe wengine wa Kamati hii ni Viongozi wa juu wa Taasisi zifuatazo:
Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA)
Postamasta Mkuu, Shirika la Posta Tanzania (TPC)
Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)
Mkurugenzi Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)
Ndugu Waandishi wa Habari,
Utekelezaji
wa mfumo wa anuani za makazi na simbo za posta ulianza kwa majaribio
katika Manispaa ya Arusha mwaka 2009 ambapo eneo kubwa ndani ya Kata 8
zimewekwa majina ya mitaa na namba za nyumba. Kata hizo ni Sekei, Kati,
Levolosi, Kaloleni, Themi, Unga Limited na Olorieni, na tayari nyumba
zipatazo 5,000 zimeshawekewa namba.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kufuatia
mafanikio ya utekelezaji wa mfumo huu kwa majaribio katika Manispaa ya
Arusha, utekelezaji wa awamu ya kwanza umeanza mwaka 2011 katika
Manispaa ya Dodoma ambapo eneo kubwa katika Kata 8 pia zimewekwa majina
ya mitaa na tayari nyumba zipatazo 7,500 tayari zimeshawekewa namba.
Kata zilizohusika katika utekelezaji wa mfumo huu katika Manispaa ya
Dodoma ni Kilimani, Tambukareli, Madukani, Uhuru, Viwandani, Majengo,
Kiwanja cha Ndege na Makole.
Utekelezaji
wa awamu ya kwanza unaendelea kwa Manispaa na Halmashauri zingine hapa
nchini, ambapo kwa mwaka huu wa fedha utekelezaji unatarajiwa kufanyika
katika Manispaa zote za Mkoa wa Dar es salaam na Zanzibar. Utekelezaji
katika Manispaa/Halmashauri nyingine utafuata.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Mfumo
wa anuani za makazi na simbo za posta ni mtambuka. Hivyo, utekelezaji
wake unahitaji ushirikiano mkubwa na wa karibu kutoka kwa wadau
mbalimbali. Kwa mfano, Sera ya Taifa ya Posta inaelekeza uanzishwaji wa
anuani za makazi na postikodi, wakati huo huo mamlaka na madaraka ya
uwekaji wa majina ya mitaa na namba za nyumba, kisheria liko chini ya
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(OWM-TAMISEMI) ambapo utekelezaji wake unafanyika katika ngazi za
Halmashauri. Hivyo, ni dhahiri kuwa kunahitajika ushirikiano mkubwa na
wa karibu wa wadau mbalimbali katika kutekeleza mfumo wa anuani za
makazi na postikodi.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Anuani
za makazi ni muhimu sana katika maendeleo ya nchi yetu, kiuchumi,
kibiashara, kisiasa, na utoaji wa huduma mbalimbali za jamii. Faida za
kuwa na anuani hizi zinamgusa kila mmoja wetu, kuanzia Serikali na
taasisi zake, kampuni kubwa na ndogo, wafanya biashara, watoa huduma
mbalimbali za jamii (umeme, maji, gesi, huduma za kifedha kama mabenki,
wasambazaji wa barua na vifurushi), ulinzi na usalama wa raia watoa
huduma za dharura kama vile zimamoto na magari ya wagonjwa, na wananchi
wenyewe kwa ujumla. Faida za kuwa na anuani za makazi na simbo za posta
kwa Serikali ni msingi wa kutoa vitambulisho vya kitaifa kwa watanzania;
unaongeza ufanisi katika usimamizi ya makazi ya watu; unawezesha
kutambua mali na kaya katika eneo husika; utaongeza tija katika huduma
za uokoaji na maafa; unawezesha ukusanyaji wa kodi mbalimbali kwa
urahisi na kwa wakati; unajenga umoja, mshikamano na utaifa katika nchi;
unaongeza kasi ya kupambana na uhalifu, kuimarisha shughuli za uhamiaji
na kuongeza utalii.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kwa
upande wa huduma za posta, utekelezaji wa mfumo wa anuani za makazi na
simbo za posta, utarahisisha uchambuaji wa barua kuwa wa haraka na
ufanisi zaidi; utawezesha utambuaji wa anuani kwa urahisi zaidi;
utaongeza ufanisi katika usafirishaji na usambazaji wa barua na pia
vifurushi; utaongeza ufanisi katika kushughulikia malalamiko ya wateja;
utapunguza uwezekano wa barua kupotea.
Pia
una manufaa kwa jamii kama vile; kutoa anuani ya uhakika kwa kila
mwananchi au mkazi; itarahisisha utoaji wa utambulisho sahihi;
unarahisisha kupata huduma za jamii kama vile za afya, usalama, maji;
kuwezesha matumizi ya vifaa vya kisasa (kwa mfano vifaa vya kuongoza
magari kwa kutumia mfumo wa GPS) katika miji yetu; unarahisisha
biashara kwani inawezekana kununua bidhaa ukiwa nyumbani kwa kutumia
teknolojia za kisasa kama biashara mtandao; Kutambua mazingira yetu
kirahisi na kufahamu mahali ulipo.
Kwa
upande wa wenzetu wafanyabiashara, anuani za makazi na simbo za posta
zitaboresha maendeleo ya biashara; kupata anuani za kuaminika za wateja;
kuwezesha kutoa mikopo na kukusanya madeni kirahisi hasa kwa mabenki;
utawezesha uendeshaji biashara kwa njia ya mtandao; Itawezesha upangaji
wa mauzo, na utoaji wa matangazo na uhamasishaji katika maeneo ya
biashara kwa kuwafikia kirahisi walengwa; kufanikisha kazi za tafiti za
biashara, kwa mfano, kuwajua wateja wa tabaka fulani na kuwahudumia
ipasavyo.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Katika
kutekeleza mfumo wa anuani za makazi na postikodi, ziko pia changamoto.
Baadhi ya changamoto hizo ni kuwa na maeneo ambayo hayajapangwa vyema
katika miji yetu, usimamizi wa miundombinu ya anuani za makazi na pia
uhaba wa fedha kwa ajili ya kutekeleza mfumo huu kwa haraka ili uweze
kuleta maendeleo haraka zaidi.
Kwa
kutambua umuhimu wa anuani za makazi lakini pia changamoto ya uhaba wa
fedha za kutekeleza mfumo huu katika Mkoa wa Dar es Salaam, Viongozi wa
Mkoa wa Dar es salaam walikubaliana kwa pamoja kuwa kiandaliwe chakula
cha hisani cha kuweza kuchangisha na kupata fedha za kusaidia
utekelezaji wa mfumo huu kwa ufanisi na kwa muda uliopangwa katika Mkoa
wa Dar es Salaam. Hivyo, Inatarajiwa kuwa shughuli za uchangiaji wa
fedha kwa ajili ya kutekeleza mfumo utafanyika hivi karibuni katika
Viwanja vya Karimjee baada ya maandalizi muhimu kukamilika.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Serikali,
kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, imefungua akaunti maalum ya
benki kwa ajili ya uchangiaji wa fedha kwa ajili ya kutekeleza mfumo wa
anuani za makazi katika Mkoa wa Dar es Salaam. Akaunti hiyo inaitwa TCRA
– POSTCODE PROJECT yenye namba 0150315694502 iliyofunguliwa katika
Benki ya CRDB, Tawi la Mlimani City.
Ninatoa
wito kwa wadau wote wa Mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi
kuchangia kupitia akaunti hii ili tuweze kutekeleza mfumo wa anuani za
makazi katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Kwa taarifa
zaidi wasiliana na Ofisi ya Katibu Mkuu, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi
na Teknolojia; Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania, Ofisi ya Postamasta Mkuu, Shirika la Posta Tanzania na Ofisi
ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam.
Asanteni sana kwa kunisikiliza
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :