BAKWATA Yatangaza Waislamu Kugomea Sensa
Posted in
No comments
Thursday, June 14, 2012
By
danielmjema.blogspot.com
BARAZA
Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limetangaza rasmi kutoshiriki sensa
ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika nchi nzima Agosti, hadi ombi
lao la kuingizwa kwa kipengele cha dini kwenye dodoso la sensa
kitakapofanyiwa kazi.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Amir Mkuu wa Jumuiya na
Taasisi za Kiislamu nchini, Shehe Mussa Kundecha, alisema uamuzi huo
umetokana na Serikali kushindwa kusikiliza upande wa Waislamu na kuamua
kutokiingiza kipengele hicho.
Alisema
katika mkutano wa viongozi wa dini na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)
uliofanyika Dodoma Juni 11, waliwasilisha ombi lao la kipengele cha dini
kuingizwa kwenye dodoso za sensa ili kupata idadi kamili ya Watanzania
kidini.
“Kwa
kweli mkutano ulikwenda vizuri, tulitoa sababu zetu za kutaka kipengele
hicho kiwemo ili kuondoa utata wa sasa wa kila taasisi na dini kutoa
takwimu zinazotofautiana na Kamishna wa Takwimu alipokea maombi yetu na
kuahidi kuyawasilisha serikalini na kuyafanyia kazi,” alisema Shehe
Kundecha.
Alisema
cha kushangaza wakati akifunga mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wasira alibainisha wazi kuwa kamwe
Serikali haiwezi kukiingiza kipengele hicho kwenye dodoso za sensa, kwa
kuwa kinavunja umoja, amani na utulivu wa Taifa.
Aidha,
alisema katika kutetea hoja hiyo, Serikali ilitoa mifano ya nchi za
Nigeria na Kenya, ambazo zimefanya sensa na kuingiza kipengele hicho
kwenye dodoso, lakini kutokana na kuibuka kwa vuguvugu la kidini katika
nchi hizo, hadi leo matokeo ya sensa hizo hayajatangazwa.
Shehe
Kundecha alisema Baraza hilo limepokea hoja hizo na kuzisikiliza ingawa
halikubaliani nazo kwa kuwa kwa Tanzania bado zipo taasisi na madhehebu
ya dini yanayotoa takwimu za kidini yakionesha idadi ya Wakristo,
Waislamu na Wapagani huku umoja na amani vikiendelea kuwapo.
“Kama
tatizo ni kuvurugika kwa amani, umoja na utulivu, mbona basi vyombo
hivi visivyohusika na takwimu vinatoa takwimu hizi tena hadi kwenye
mitandao na Serikali kuvifumbia macho, huku kukiwa hakuna umoja wala
amani iliyovunjika? Kwa nini isifanyike sensa ya kidini na kupatikana
takwimu halisi?” Alihoji.
Alisema
kutokana na kauli hiyo, inaonekana wazi kuwa Serikali haijasikiliza
kilio cha Waislamu kutaka kipengele cha dini kiingizwe kwenye dodoso za
sensa, ili zipatikane takwimu sahihi na rasmi za Watanzania kidini.
“Hivyo
basi tunasisitiza Waislamu hatutashiriki sensa mpaka mapendekezo yetu
yatakapofanyiwa kazi, tunataka idadi halisi ya Waislamu, ili nasi tujue
tunawasaidiaje kimaendeleo na kidini,” alisema.
Ustaadh
Sadiki Gogo, alisema mfano uliotumiwa na Serikali kukataa ombi la
kuingizwa kwa kipengele cha dini kwenye dodoso la sensa hauna nguvu, kwa
kuwa umeegemea upande mmoja na kusahau nchi kama Uganda, Uingereza,
Australia na Canada, ambazo katika sensa zao wanatumia kipengele cha
dini na hazina matatizo.
Hivi
karibuni, Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Tanzania, Shehe Ponda Issa
Ponda, alisema atahakikisha Waislamu hawashiriki Sensa ya Watu na Makazi
iwapo Serikali haitarudisha kipengele cha dini katika maswali
wanayoulizwa wananchi.
Alisema
haoni hoja ya msingi ya kuondoa kipengele hicho kwani uzoefu unaonesha
kuwa baada ya Serikali kukiondoa, makundi yenye mwelekeo maalumu hutumia
nafasi hiyo kutoa takwimu za idadi ya Waislamu, Wakristo na Wapagani.
Pamoja
na kauli ya Wasira, Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk Albina Chuwa, alikataa
ombi la mashehe la kujumuisha kipengele cha dini katika dodoso za
maswali wakati wa sensa. Alisisitiza mbele ya viongozi wa dini
mbalimbali wakiwemo mashehe kuwa maswali yanayohusu kabila na dini
hayatajumuishwa kwenye dodoso kwani Serikali haipangi mipango ya
maendeleo ya wananchi kwa kufuata itikadi za kidini au ukabila.
Chanzo Habari Leo
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako

0 MAOINI :