Saturday, June 16, 2012

GAMA: "TUNZENI MAZINGIRA KWA FAIDA YA KESHO"

MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO, LEONIDAS GAMA
KAMATI ya ushauri mkoani Kilimanjaro, RCC, imeazimia kudhibiti uharibifu wa mazingira kwa kuweka mikakati thabiti ikiwemo kutunga sheria ndogo ndogo elekezi kutokana na sheria mama ya mazingira inayosimamia utunzaji wa mazingira katika maeneo yote ya hifadhi, makazi ya watu na maeneo ya wazi nchini.

Maazimio hayo yanatokana na mapendekezo yaliyotolewa katika kikao cha RCC mkoani hapo, kilichofanyika tarehe 29 Februari mwaka huu, na taarifa ya warsha ya mazingira iliyofanyika tarehe 13 juni mwaka huu, na kuhusisha wadau wa mazingira wa mkoa, wilaya, KINAPA, kata zote, vijiji na taasisi zote za serikali kama vile TATeDO na UNDP.

Akiongea katika uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji kwa kila halmashauri za wilaya ya mkoa huo, mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, aliyepia mwenyekiti wa kamati ya ushauri ya mkoa RCC, alisema kuwa, mkoa kwa kauli moja imeazimia kupinga uharibifu wa mazingira pamoja na kutunza vyanzo vya maji ikiwemo mlima Kilimanjaro.

Gama alisema, katika maazimio hayo kamati ya ushauri ya mkoa imeazimia kusitisha kwa muda, utoaji wa vibali vyote vya kukata miti ya asili kwa ajili ya mbao au kuni, kusimamia na kutekeleza sheria zote za mazingira kwa pamoja, kurudisha majukumu ya usimamizi wa eneo la nusu maili kwenye usimamizi ya KINAPA, kutokana na uharibifu mkubwa kwa sasa kuanzia katika eneo hilo.

Maazimio mengine yaliyowekwa ni, kuhakisha kuwa elimu ya mazingira na sheria zake inatolewa kwa jamii kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayoshughulikia mazingira ili kuharakisha zoezi la Kudhibiti uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira kwa kutumia nishati mbadala na majiko banifu.
Aidha Gama, alitoa agizo kwa halmashauri zote mkoani Kilimanjaro, kutumia fedha zinazotolewa na wafadhili kwa kuendeleza zoezi la upandaji miti na sio kulipa madeni ya awali yaliyotumika katika halmashauri hizo kupandia miti kwani zoezi la awali la upandaji lilidhaminiwa na serikali.

Katika maazimio hayo pia, kamati ilitoa agizo kwa halmashauri zote kusimamia vijiji vyote ili viandae mipango ya matumizi bora ya ardhi na kuweka mipaka ya shughuli zote ambazo zinatekelezwa katika kijiji kama vile eneo la kilimo, hifadhi ya misitu, makazi pamoja na maeneo ya malisho.

Na kijiweblog, moshi

No comments:

Post a Comment