Ni Uhalisia Huu Unaotutaka Tuwachukie Wanasiasa Wenye Kuendekeza ....

Posted in
No comments
Sunday, June 10, 2012 By danielmjema.blogspot.com




 
....Ubaguzi wa kisiasa. Wenye kupandikiza mbegu za chuki za kidini, kikabila na hata kikanda miongoni mwetu Watanzania. Nimepata kuandika, kuwa Tanzania ina vyote, kasoro Watanzania.

Kwamba kinachokosekana  ni uzalendo. Mioyo ya wanasiasa wetu wengi imejaa hila badala ya nia za dhati za kuijenga nchi yetu.  Na kama mwanasiasa ana nia ya dhati ya kuijenga nchi yetu hawezi akawabagua Watanzania wenzake wengine wasishiriki siasa na kuijenga nchi yao.

Ndio maana, hata teuzi za wajumbe wa bodi za mashirika ya umma zinatokana na itikadi za vyama; kwamba walio nje ya chama tawala wanabaguliwa, kana kwamba hao hawawezi kuwa na michango ya kuimarisha mashirika ya umma. Halafu tunashangaa kuwa Reli haifanyi kazi, Atcl inavurunda, bandari kugeuka kuwa kijiwe cha wajanja wenye kutafuna, TBS kuachwa ikivurunda mpaka Bodi nzima inakatiwa tiketi kwenda Japan kwa fedha za umma, kujaribu kuyaficha madudu ya TBS,  na  mengi mengineyo.

Ndugu zangu,
Hii ni Nchi Yetu. Ni nchi yetu sote. Haya yote yasitufanye tuichukie nchi yetu tuliyozaliwa, bali yatutie hamasa zaidi ya kuipigania nchi yetu.

Nilifikiri ningeandika sentesi mbili tu kuhusu picha hizo mbili. Nimejikuta naandika mengi. Ndiyo, inasikitisha kuwaona Watanzania wenzetu hao pichani kuwa umuhimu waokwa wanasiasa  uonekana wakati wa kukaribia kwenda kuwaomba kura. Tena, dhiki yao ndio huwa mtaji wa wanasiasa.  Kwa hila na ghilba hushawishiwa, kwa vipande vya khanga, bakuli za sukari na hata lita za pombe ya kupima ,  kuwapigia kura wanasiasa. Kisha wanatelekezwa.

Ndugu zangu, 
Tuna lazima ya kuwapigia kelele wale wote wenye kutenda maovu kwa nchi yetu. Wenye kuwadhalilisha Watanzania wenzetu kwa sababu ya umasikini wao uliotengengezwa na baadhi ya wanasiasa wao. Maana, pamoja na yote haya, jahazi la nchi yetu halijazama, linayumba  sana.

Siku ile tutakapoacha kuwapigia kelele viongozi wanaoisaliti nchi tuliyozaliwa kwa matendo yao, basi, ndio utakuwa mwanzo wa jahazi la nchi yetu kuzama. Na historia itakuja kutuhukumu. Kwa kukaa kwetu kimya.

Na mwanakijiwe
IRINGA

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .