Na Fadhili Athumani, Karatu
MWANARIADHA Dickson Marwa kutoka katika timu ya
Holili, Kilimanjaro ameibuka mshindi wa mbio za ngorongoro Marathon
zilizofanyika Jana wilayani Karatu, Mkoani Arusha kwa kutumia muda wa saa 1:04:49.
Marwa alitumia muda huo katika mbio hizo zinazodhaminiwa
na Kampuni ya Tigo kwa mika 6 mfululizo sasa, zilizoanzia katika geti la
Ngorongoro umbali wa kilometa 21 na kumalizikia katika uwanja wa Mazingira
mjini Karatu.
Katika nafasi ya pili alikuwepo mwanariadha,
Stephano Huche kutoka Arusha ambaye alitumia muda wa saa 1:04:56 akifuatiwa kwa
karibu na Alphonce Felix wa timu ya Winning spirit ya Arusha aliyetimua mbio
hizo kwa muda wa saa 1:05:24.
Washindi wengine katika mbio za kilomeata 21 wanaume
ni Calisti Muhindi wa babati akitumia muda saa 1:05:41, Msenduki Muhamedi wa
Hanang akitumia muda wa saa 1:05:48, Andrew Sambu wa Hanang pia akifuatia
katika nafasi ya sita kwa kutumia muda wa saa 1:05:52 na Damian Chopa wa JKT
aliyetumia muda wa saa 1:05:54 akishika nafasi ya saba.
Katika mbio za wanawake mwanariadha Jackline Sakilu
wa JWTZ alionesha umwamba wake baada ya kuibuka mshindi akitumia muda wa saa
1:16:26 na kuwaacha Zakia Mrisho wa Team 100 (1:17:47) na Mary Naali wa AAAC (1:18:47)
wakimaliza katika nafasi ya pili na tatu mfatano huo.
Awali akizindua mbio hizo Naibu waziri Maliasili na
Utalii, Lazaro Nyalandu aliwataka watanzania kuwa wabunifu na kuanzisha
mashindano kama haya ili kusiadia kuhamasisha utalii wa ndani na wa nje.
Kwa upande wake Balozi wa Malaria msanii Barnaba
Elias alisema kuwa lengo la kushiriki mbio za mwaka huu ni kuhamasisha vijana
kushiriki kikamilifu vita dhidi ya Malaria na kuongeza kuwa kwa kutumia michezo
na sanaa kampeni hiyo imefanikiwa pakubwa mpaka sasa.
Mshindi wa kwanza katika mbio za mwaka huu kwa
upande wa wanaume amejishiundia fedha taslimu shilingi milioni moja, simu ya
mkononi kutoka Tigo na medali huku mshindi wa kilometa 21 wanawake akiondoka na
fedha taslimu shilingi laki tano, Simu ya mkononi na medali huku washindi
wengeni nao wakiondoka na zawadi mbambali.
Mbio za Ngorongoro Marathon zimeandaliwa na kampuni
ya kitalii ya Zara Tours kupitia mfuko wake wa Zara charity, Hifadhi ya Ngorongoro,
na kudhaminiwa na kampuni ya simu za mkononi ya Tigo pamoja na washirika
wengine.
Mwisho.

No comments:
Post a Comment