RT ILIVYOISUKA UPYA KATIBA YAO.....
Na Athumani Issa, Moshi
VYAMA vingi vimekuwa vikijikuta vikiingia katika Migogoro ya mara kwa
mara kutokana na kukosa miongozi sahihi ya kuhakikisha matatizo yote
yanayojitokeza yanatatuliwa kisheria.
Moja ya Vyombo muhimu vinavyoweza kutumika kutatua migogoro hii hasa
ukizingatie penye watu wengi lazima kuwe na migongano ya kimawazo kama
sio kimaslahi.
Katika kutambua hili shirikirisho la Riadha Tanzania (RT),katika
mkutano wake mkuu uliofanyika Julai 27 na 28 mwaka huu, mjini
Morogoro, imeazimia kuhakikisha hali kama hii haijitokezi kabisa na
kama imewahi kujitokeza basi isijirudie tena.
Katika kuhakikisha hilo, RT chini ya Rais wake, Anthony Mtaka
ilitangaza kuingia katika mchakato wa kuandaa katiba ambapo ilimteua
Mwanasheria wake, Thabit Bashiri kusimamia mchakato huo ambaye katika
mkutano mkuu uliofanyika Mjini Morogoro aliwasilisha Rasimu ya Katiba
kwa wajumbe wa Mkutano.
Hivyo basi ili kuhakikisha umma unapata kuelewa kilichomo ndani ya
Rasimu hiyo, Taifa Letu.com ilimtafuta Thabit Bashiri na kufanya naye
mahojiano ya kina ambapo alizungumza mambo kadha wa kadha ikiwemo
baadhi ya mambo muhimu aliyoyazingatia katika kuunda Rasimu hiyo ya
Katiba.
Bashiri anazungumzia mambo mbali mbali ambayo kutokana na uzoefu wake
na Taaluma yake anaamini kama yatazingatiwa na kama yangezingatiwa na
Vyama vingi vya Michezo Tanzania na Duniani kote kwa ujumla, migogoro
yasiyokuwa na lazima yasingetokea, na hapa anaelezea moja baada ya
nyingine:
Taifa letu.com: baada ya kupewa kazi ya kutengeneza Rasimu ya Katiba
ya Shirikisho la Riadha Taifa, ni changamoto gani uliziangalia?
Mwanasheria: Ukweli ni kuwa nilifahamu kuwa moja kati ya matatizo
makubwa yanayovikumba vyama vya michezo nchini Tanzania na barani
Afrika kwa ujumla ni ubovu wa katiba zao.
Ubovu wa katiba kwa asilimia kubwa ndiyo unachangia matatizo
mbalimbali katika vyama vyetu kama kutokuwa na vyanzo vya mapato vya
kutosha, migogoro isiyoisha, rushwa, uchaguzi usio na haki, ufujaji wa
mali za chama, unyanyasaji wa kijinsia, ugandamizwaji kwa wachezaji,
maamuzi yasiyo na haki n.k . Hivyo basi moja kati ya malengo yangu
makuu ilikuwa ni kuja na rasimu ya katiba ambayo itakuwa na lengo la
kuwa suluhisho la matatizo hayo.
Taifa letu.com: Katiba ya zamani haikuwa na yapi ambayo kwa sasa
umejaribukuyazingatia?
Mwanasheria: Katiba iliyopita haikuwa na utambuzi kwa wadau mbalimbali
wa Riadha kama Klabu za Riadha, wawakilishi wa wachezaji,wahamasishaji
(Promoters) na hivyo kusababisha sio tu kukosa mapato bali pia kukosa
nguvu ya kuendeleza riadha nchini Tanzania.
Pia katiba iliyopita ilikuwa na utaratibu uliopitwa na wakati wa
utatuti wa migogoro kiasi kwamba ilishindwa kudhibiti na kuamua
migogoro mbalimbali kwa usawa.
Lakini pia iliruhusu matumizi holela ya fedha za chama,hapakuwa na
udhibiti mzuri wa fedha za chama hivyo kusababisha chama kukosa
uaminifu mbele ya jamii na hivyo wadau na wadhamini kukikimbia na
kukifanya kuwa masikini. Hivyo wakati wa kutengeneza rasimu hii
mpya, mambo hayo yote nimeyazingatia katika kurudisha imani kwa
wananchi na wadau wa riadha ndani na nje ya nchi.
Taifa Letu.com: Je Katiba hii itakuwa na msaada gani kwa RT na
Watanzania wapenda Riadha kwa ujumla?
Mwanasheria: Rasimu hii imelenga katika kuifufua Riadha upya kuanzia
vijijini mpaka mijini, kuleta mahusiano mazuri baina ya wadau wa
Riadha na kuleta uwiano wa kijinsia katika ushiriki na uongozi wa
Riadha.Rasimu hii inalengo la kumfanya mwanariadha au kiongozi
ajivunie kuwa ndani ya familia ya Riadha na aweze kushiriki kwa
dhumuni la kuitangaza na kuiendeleza Riadha Tanzania.
Kwanza, nilipata fursa ya kujionea maendeleo ya vyama vya Riadha
katika nchi zilizopiga hatua katika mchezo wa Riadha, kwa mfano Nchi
kama Kenya, Afrika ya kusini, Msumbiji, Ghana na Zambia zimeweza kuwa
na Katiba bora ambazo zimekuwa chachu ya maendeleo ya Riadha hasa
katika kuwavutia wadhamini.
Sio hivyo tu, ubora wa Katiba zinazoendesha vyama vya nchi hizo
nilizozitoea mfano umechangia kikubwa kuongezeka kwa vyanzo vya mapato, kuungwa mkono na wadau mbalimbali, uratibu mzuri wa migogoro
na uimarishaji thabiti wa viwanja vya michezo hasa katika mchezo huu
wa Riadha.
Taifa letu.com: Lakini Mwanasheria, bado sijaona ni kwa namna gani
Rasimu hii ya ilivyoweza kuzingatia uhamasishaji wa ushiriki wa
wanariadha wa kike ukizingatia kuwa kumekuwa na uhaba wa wanariadha wa
kike wanaoshiriki au kuwania uongozi katika nyadhifa mbalimbali ndani
ya Mchezo huu?
Mwanasheria: Katika mambo ambayo nimeyaingiza kwa makusudi ni kuweka
vifungu ambavyo vinailazimisha kamati ya utendaji kuteua wanawake
wawili kwa kila kamati ndogo watakazoteua.
Lengo kubwa ni kukuza uhamasishaji katika mchezo huu ambapo kadri siku
zinavyozidi kwenda ushiriki wa wasichana unazidi kupungua na hivyo
kuwakosesha wasichana kupata fursa ya kufaidika kutokana na vipaji
vyao na sio hilo tu pia katika rasimu hii nimejaribu kuangalia umihimu
wa kuingiza suala la kamati ya wanawake ambayo kwa asilimia kubwa
itawakilisha sauti ya wanawake katika familia ya Riadha
Taifa Letu.com: Kumekuwa na matukio ya matumizi ya Madawa ya kuongeza
Nguvu miongoni mwa wanariadha, mfano hivi karibuni tulisikia sakata la
mwanariadha wa Marekani,Tyson Gay, kukutwa na kosa la kutuia madawa ya
kulevya, rasimu hii imejiandaa vipi kukabiliana na hilo?
Mwanasheria: Moja kati ya mambo muhimu ambayo yanahitajika kuwa katika
katiba yoyote ya chama cha Riadha ni kuwa na katiba ambayo inaunga
mkono upingaji wa madawa ya kulevya unaofanywa na WADA (World
Anti-Doping Agency).
Hivyo rasimu hii moja kwa moja inaunga mkono uchunguzi wa wachezaji
kuhusu matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu ambao utakuwa ukifanywa
kila kwenye mashindano yanayoandaliwa na RT na kutuma taarifa kwenda
kwenye Shirikisho la Riadha Duniani.
Taifa Letu.com: Kumekuwa na matukio ya matumizi mabaya ya Fedha ambayo
uzoefu unaonesha kuwa ndio chanzo kikuu cha migogoro ndani ya vyama
vingi vya michezo, hili nalo limezingatiwa vipi katika rasimu hii au
ndio mradi mambo yaende?
Mwanasheria: Kwanza nikushukuru Ndugu mwanadishi kwa Swali lako zuri,
katika Rasimu hii nimeweza kuainisha vyanzo mbalimbali vya mapato
ambavyo RT inaweza kuvitumia na kunufaika navyo na hivyo kuwa na fedha
ya kuweza kusimamia shughuli zake ikiwemo kulipa wafanyakazi,
kusafirisha timu ndani na nje na kuandaa mashindano.
Pia rasimu hii imeweza kuainisha njia nzuri za matumizi ya fedha
zipatikanazo kutokana na vyanzo mbalimbali, ambapo imeelezwa wazi kuwa fedha yoyote ipatikanayo katika RT ni kwa madhumuni ya kuendeleza
mchezo wa Riadha, hivyo kutakuwa na uwasilishwaji na upitishwaji wa
taarifa za fedha kwa kamati ya fedha, kamati ya utendaji na kwenye
mkutano mkuu.
Nafahamu swala la uaminifu nalo ni tatizo miongoni mwa baadhi ya
viongozi wetu, ukisoma kwa makini rasimu hii utagundua kwamba hili
nalo halijaachwa, imeanishwa vizuri katika rasimu kuwa kutakuwa na
mkaguzi huru wa mahesabu atakayekagua taarifa zote za fedha za chama
huku vyama vya mikoa vikihitajika pia kuwasilisha taarifa zao za fedha
kila mwaka, lengo ni kuhakikisha fedha zinatumika kwa dhumuni moja tu
la kuendeleza mchezo wa Riadha nchini Tanzania.
Taifa Letu.com: Mwanasheria utakubaliana na mimi kuwa utatuzi wa
migogoro ndani ya Vyama vingi vya michezo umekuwa wenye mashaka na
mara nyingi kumekuwa na malalamiko kuhusiana na swala hili, vipi
Rasimu hii inashughulikiaje hilo tatizo?
Mwanasheria: Bila shaka Ndugu mwandishi, hilo liko wazi kabisa,
tunafahamu kuwa katika vyama vya michezo, migogoro ndiyo tatizo kuu
ambalo hudumaza michezo na maendeleo ya vyama, hii inatokana na
utaratibu mbovu na wa kiuonevu na usiotoa haki kwa aliyekosa au
aliyekosea na hivyo kusababisha migogoro kuendelea kila kukicha na
kudumaza michezo.
Rasimu hii imeanzisha kamati tatu za sheria, Kamati ya Maadili, Kamati
ya Nidhamu na Kamati ya Rufaa katika kutatua makosa mbalimbali ya
kinidhamu ya chama na wanachama wake.
Pia Katiba imeanzisha baraza la usuluhishi kwa ajili ya kutatua shauri
lolote kati ya wanachana na chama, mchezaji na chama au mchezaji na
mchezaji. Katiba imeweka wazi umuhimu wa kutambua mahakama ya
usuluhishi wa Michezo (CAS) iliyopo Lausanne, Switzerland hivyohaitaruhusiwa kwa shauri la kimichezo kupelekwa katika mahakama
zisizo za kimichezo.
Taifa Letu.com: Ahsante, kuna lipi jipya ambalo rasimu hii imeongeza
ili kuleta chachu ya Maendeleo ya Riadha nchini na pengine kuturudisha
katika enzi za mafanikio ya akina Filbert Bayi na Suleiman Nyambui?
Mwanasheria: Mengi sana, tumejaribu kupendekeza mashindano mapya baina
ya mikoa na mikoa (Inter-regional), pia mashindano ya taifa ya klabu
za Riadha na mashindano ya mikoa ya klabu za Riadha.
Pamoja na hayo, taasisi za elimu na majeshi zimepewa uanachama
shirikishi, lengo hapa ni kuchochea uhamasishaji wa mchezo huu kuanzia
vijijini mpaka mijini na pia kutoa wigo mpana wa kupata wachezaji
wengi kwa kadri inavyowezekana.
Pia katiba hii imediriki kuimarisha uhusiano baina ya RT na vyama vya
mikoa vya Riadha, hii inatokana na kudorora kwa mchezo huu mikoani
hivyo kuhitajika juhudi za dhati katika kuhakikisha kuwa vyama vya
mikoani vinaamka na kufanya kazi iliyokusudiwa kwa maendeleo ya
wanariadha na watanzania kwa ujumla.
Taifa Letu.com: Wadau na Wanachama wanatawezaje kutoa mchango wao
kwenye rasimu hii?
Mwanasheria: Baada ya kupita katika kamati ya utendaji na kufanyiwa
marekebisho kadhaa, rasimu hii itatumwa kwa wanachama na wadau wote
Tanzania nzima na watahitajika kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya katiba
hii kabla ya kuipitisha katika mkutano mkuu ili kuanza kutumika rasmi.
Taifa Letu.com: Nakushukuru sana Mwanasheria, ila kabla hatujaagana
ushauri wako kwa wadau wa riadha kwa jumla ni nini?
Mwanasheria: Binafsi ningependa kuwaomba kwa dhati, kuipitia rasimu
hii ya katiba kwa ajili ya maendeleo ya mchezo huu Tanzania, Naamini
Riadha ndiyo mchezo pekee ambao kama tukiutolea mkazo tunaweza
kupeperusha bendera yetu katika ushiriki wa ngazi za kimataifa.
Tanzania imejaaliwa kuwa na wanaridha wa aina zote,wanariadha wa mbio
ndefu na fupi,miruko na hata mitupo,hivyo kama tutatumia vizuri fursa
hii,tunaweza kuwa na katiba bora ambayo itaweza kuleta maendeleo ya
riadha nchini Tanzania,kupunguza tatizo la ajira na kusaidia ujenzi wa
taifa kupitia mchezo wa Riadha.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Riadha yetu!!
0756038214/0654724337
www.kijiwechetu.blogspot.com
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :