MAANDALIZI YANAHITAJIKA MBIO ZA 'SOKOINE DAY'
Posted in
Kumbukumbu ya Sokoine
,
Riadha
No comments
Monday, April 14, 2014
By
danielmjema.blogspot.com
SOKOINE Min Marathon 2014 imefanyika mwishoni mwa wiki kuadhimisha
miaka 30 ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Moringe
Sokoine, kijijini kwake Monduli Juu mkoani Arusha.
Waziri huyo alitajwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere,
kwamba alikuwa mwerevu sana, licha ya kwamba Mwalimu alisema werevu
kila mmoja anao hata shetani naye ni mwerevu sana, kubwa zaidi kwa
Edward lilikuwa ni hodari wa kazi.
Hii ndio sababu hata Taifa linakumbuka kuadhimisha kutokana na ukweli
kwamba alikuwa na uwezo wa kufanya kazi siku mbili hata tatu bila
kulala hii ilitokana na wema wake na upole kwa watu wa taifa la
Tanzania.
Rais Jakaya Kikwete kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani,
alikuwa mgeni rasmi wa Kumbukumbu ya Kifo cha Sokoine, ambako
alihutubia umati wa watu uliofurika katika kaburi la kiongozi huyo
shupavu aliyeacha historia kwa Tanzania na kuweka shada la maua juu ya
kaburi hilo.
Siku hiyo ilifana kutokana na uwepo kwa michezo mbalimbali ikiwemo
riadha, miruko, kurusha mikuki nk, ambapo wanariadha nguli walipambana
vilivyo katika ‘Sokoine Day 2014.’
Nilichojifunza katika sherehe hizo, mchezo wa riadha unakua kwa
kasi nchini hivyo ni vema ukapewa kipaumbele kutokana na ukweli kwamba
una historia nzuri hapa nchini ambayo bila juhudi tutabakia katika
makabrasha ya historia, kwamba miaka ya 1960 hadi 1990 ulikuwa juu.
Wanariadha wa kujitegemea kina Fabian Joseph (Arusha), Nathalia
Elisante (Arusha) Mary Naali, Selina Amosi (Zanzibar) walikimbia mbio
za kilometa 10 na kutoa ushindani wa hali ya juu.
Holili Youth Athletics Club (HYAC) haikuwa nyuma, nayo iliweza
kufurukuta na kuibuka washindi chipukizi katika kilometa 2 wasichana,
ambako Adelina Audax aliwaongoza wasichana wenzake akifuatiwa na Neema
Mathias na nafasi ya tatu kunyakuliwa na Lidiuna Godfrey wote kutoka
klabuni hapo.
Sakilu akimaliza mbio |
Wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari kutoka maeneo ya karibu na
Monduli Juu walishiriki na kutoa ushindani wa juu kuwahi kushuhudiwa,
kutokana na wanafunzi hao kunirudisha miaka ya nyuma wakati Umitashumta
na Umiseta ulipokuwa ukifanya vema katika kuibua vipaji vya riadha.
Kubwa zaidi mbio hizo ziliathiriwa na msafara wa viongozi wengi wa
kisiasa waliokuwa wakimiminika kwa ajili ya maadhimisho hayo muhimu
nchini Tanzania, kwani mbio zilipokuwa zikianza wanariadha walijikuta
wakisongamana eneo moja hali iliyosababisha wasikimbie kwa muda mzuri.
Alphonce Felix akimaliza mbio hizo katika nafasi ya pili baada ya Fabian Joseph |
Katika mbio kinachoangaliwa ni muda ambao mwanariadha anakimbia kwani
amekuwa wa kwanza ama wa mwisho ni kitu kingine ambacho kwa
wanaotafuta vipaji vya wanariadha watakachoangalia ni muda aliokimbia
mwanariadha husika.
Mshindi wa Kilometa 10 katika kuadhimisha miaka 30 ya kifo cha
Sokoine, Fabian Joseph alikimbia kwa dakika 34:28.04 huku Alphonce
Felix (Holili Youth Athletics Club) alikimbia kwa dakika 34:45.39 na
Dickson Marwa (Holili Youth Athletics Club) bingwa wa mbio hizo mwaka
2013 alikimbia kwa dakika 34:57.47.
Mgeni Rasmi wa maadhimisho ya mwaka huu, Rais Kikwete akiwa na wake wa Sokoine pamoja na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa |
Kitaalamu ukiangalia muda waliokimbia wanariadha hawa hauridhishi
kabisa, kwani Alphonce Felix (HYAC) Bingwa wa Mbio za Mwaka Mpya 2014
zilizofanyika Jijini Dar es Salaam kwa umbali huo huo alikimbia kwa
dakika 28:11.35, ukiangalia sababu ya kushuka ni kutokana na utiriri wa
magari ya waheshimiwa, ukiwamo pia ubovu wa barabara uliojaa tope.
Gidabuday-mratibu wa mbio |
Nilicheka kidogo wakati nilipoona kwa macho yangu ‘kijiko’ cha
TANROADS kikichonga barabara asubuhi wakati wanariadha walipokuwa
wakikimbia na kwa bahati mbaya sana mvua ya manyunyu ikiwa imelifunika
anga na kijiko hicho kikakataa kurudi nyuma na kuziba barabara.
Wanariadha waliokuwa wajanja ndio waliovuka hapo wengine walikata
tamaa kabisa ya kuchukua taji, najua wazi kuwa barabara ilikuwa
ikiwekwa kifusi ili waheshimiwa viongozi wasikwame.
Ili tusikwamishe riadha nchini, ni vema ikafanyika siku moja kabla ya
tukio la Kumbukumbu ya Sokoine, ili na watu wa eneo lile waweze
kujipatia kipato kutokana na uwepo wa watu wengi ndani ya siku tatu au
nne hivi.
SOURCE:Tanzania Daima
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :