BURIANI ADAM KUAMBIANA, UMETUACHIA DUNIA YA KINYONYAJI

No comments
Tuesday, May 20, 2014 By danielmjema.blogspot.com

Tasnia ya filamu Tanzania imepata pigo kubwa baada ya kufariki kwa Adam Philip Kuambiana. Huyu ni mmoja kati ya waigizaji wachache waliokuwa na uwezo mkubwa.Kuambiana alikuwa na vipaji vingi. Alikuwa muongozaji mzuri sana wa filamu (Director), mwandishi wa Script, mtunzi na zaidi alikuwa muigizaji. Katika kila idara aliyoifanyia kazi, aliitendea haki vilivyo.
Ukitaka kujua kama marehemu Kuambiana alikuwa anajua kuongoza filamu, basi jaribu kutazama kazi zake kama vile Hukumu ya ndoa yangu, Regina, Born Again, Simanzi ya moyo, Lerato, Ukurasa mpya na Bado natafuta.
Hii imetokea baada ya takriban miaka miwili tangu kufariki kwa nyota mwingine wa filamu nchini, Steven Kanumba. Kwa watu wanaofuatilia sanaa hiyo inayofanywa na waigizaji wetu wa nyumbani, wawili hawa walikuwa watu muhimu sana.
Lakini kama ilivyokuwa kwa marehemu Kanumba, sidhani kama watu, hasa wenye mamlaka wanamtambua vizuri kijana huyu pamoja na mchango wake. Ni mpaka pale alipofariki, Watanzania wengi ndipo walipomtambua Kanumba alikuwa ni nani, ndipo walipogundua kuwa kumbe alikuwa na mchango mkubwa sana kwa nchi yake na vijana wenzake.
Kama wangemtambua kabla, huenda wangemsaidia katika juhudi zake za kuhakikisha anazipeleka mbele filamu za Tanzania kwa kutafuta soko la nje. Lakini bahati mbaya jambo hili lilifahamika baada ya yeye kufariki.
Na hivi ndivyo ilivyo pia kwa Kuambiana. Kama nilivyosema pale mwanzo, uwezo wa kazi na kipaji alichokuwa nacho, kama wenye mamlaka wangetambua mapema, bila shaka wangemsaidia kuboresha na hivyo kutoa kazi zenye viwango vya kimataifa.
Kuna tatizo kubwa kwa vyombo vyetu vinavyosimamia sanaa. Vinafanya kazi kwa mazoea na havitaki kabisa kubadilika ili kwenda na wakati. Wameichukulia sanaa, iwe ya muziki, filamu, ngoma au uchongaji, kama ni vitu vya kujifurahisha visivyo na maana yoyote, ndiyo maana hata watu wanaojihusisha navyo, hawachukuliwi umuhimu.
Nchini Nigeria kwa mfano, wenye kuhusika na mambo ya filamu walipoona kazi ya vijana wao inafanya vizuri, serikali iliwapa mwongozo na kuhakikisha wanapata soko hadi nje ya mipaka yao. Leo hii, soko la filamu za Nigeria limetapakaa kote Afrika Magharibi na taifa lao linaingiza mamilioni ya fedha zinazotokana na kodi.
Vyombo vyetu vinavyohusika na sanaa vimeshindwa kubadilika na kuiona kama biashara kubwa inayoweza kulisaidia taifa, kazi yao kubwa ni kukemea vitu vidogo kama uvaaji wa nguo fupi katika video za waimbaji na waigizaji wa filamu.
Kazi ambayo walipaswa kuifanya wanafumba macho, matokeo yake vijana wanafanya kazi kubwa lakini maisha yao yanatia huruma. Siku moja kabla marehemu Kuambiana hajafariki, alikutana na mmoja wa wahariri wenzangu wa hapa Global Publishers.
Baada ya kusalimiana, alitamka maneno haya “Naona mwenzangu unanenepa, mimi maisha yananipiga.”
Kauli yake inawakilisha maisha ya wengi. Kwa kazi ambazo amezifanya, kijana huyu alitarajiwa kuwa na maisha mazuri, lakini kwa waliomfahamu, wanatambua jinsi ambavyo hakufanana na uwezo na stahiki yake.
Mamlaka zinazopaswa kuwalinda, zinakaa kimya wakati waigizaji hawa wananyonywa na wasambazaji wa kazi zao, wanafumbia macho uharamia unaofanywa kwenye kazi zao na wala hawasemi kitu wanapowaona wanaingia mikataba ya kinyonyaji ambayo haiwapi haki.
Kanumba alifanya kazi nyingi zinazoendelea kuuzwa hadi sasa, lakini si yeye wala familia yake inayofaidika.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .