CHAMA cha waongoza watalii mlima Kilimanjaro (KGA), kimeitaka serikali na mamlaka husika kuweka bayana viwango vya malipo wanayostahili kulipwa waongoza watalii badala ya sasa, ambapo kila kampuni inalipa
inavyojua.
Rai hiyo imekuja wakati ambapo taarifa zinaeleza kwamba pamoja na serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii mwaka jana kupitisha kima cha chini kinachotakiwa kulipwa kwa waongoza watalii kuwa dola 20, kuna makampuni ambazo zinadaiwa kulipa Dola 10 hadi 5 kwa siku.
Akizungumza katika hafla ya kutunuku vyeti kwa waongoza watalii 84 waliohitimu mafunzo ya huduma ya kwanza, Mwenyekiti wa chama hicho, Respicious Bhaitwa alisema serikali inatakiwa kuingilia kati urasimu
huo ambao unatishia maendeleo ya sekta ya utalii nchini.
Bhaitwa alisema kuna haja ya serikali kupanga kiwango ambacho
kitatumika na makampuni yote kulipia waongoza watalii na kubainisha kuwa hiyo itasaidia kuboresha sekta hiyo na kuifanya bora katika uchangiaji wa pato la taifa.
"Baadhi ya makampuni yameanzisha vikundi vidogo ambavyo vinatumika kudhoofisha umoja wa waongoza watalii, malipo ni ya chini, lakini pia hata hicho kidogo hakitoki kwa wakati sahihi, tunaiomba serikali
kuingilia kati na kupanga kiwango sahihi," alisema Bhaitwa
Alisema katika kuhakikisha hilo ipo haja ya wizara ya maliasili na utalii kushirikiana na KGA katika kuwaendeleza waongoza watalii kwenye mlima wa Kilimanjaro na Meru, ili waweze kuwatumikia katika mkakati wa kuongeza idadi ya watalii na kuboresha utalii wa Tanzania hususani hifadhi za milima.
Kwa upande wake meneja wa Bodi ya Utalii (TTB) tawi la Arusha, Willy Lyimo aliwataka waongoza watalii kujiendeleza kitaaluma kama njia ya pekee ya kutatua matatizo yanayojitokeza kwa sasa.
Alisema ili kupata mafanikio makubwa katika shughuli zao pamoja na kupata heshima stahiki katika jamii ni lazima wazingatie suala la Elimu kwani hata malalamiko ya Malipo yanatokana na Makampuni kuwadharau kwa sababu ya elimu zao duni.
Naye mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Arumeru, ambaye ndiye alikuwa Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Evaliliana Francis alisema Serikali bado inazingatia wazo lake la kuboresha sera ya utalii ya mwaka 1999 ili kuifanya kuendana na mahitaji ya sasa.
No comments:
Post a Comment