Makachero wa Jeshi la Polisi Zanzibar, wamefanikiwa kumtia mbaroni mtu mmoja, Alawi Mohammed Silima (25), mkazi wa Fuoni Melinne, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Mtu huyo anatuhumiwa kuhusika na tukio la kummwagia tindikali Sheha wa Shehia ya Tomondo mjini Zanzibar, Mohammed Omar Saidi Kidevu. Anatuhumiwa kuwa baada ya kutenda kosa hilo alitoweka.
Hayo yamesemwa na Ofisa Habari Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Inspekta Mohammed Mhina.
Mhina alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akisakwa kwa muda mrefu na Polisi kuhusiana na tukio hilo. Alisema mtuhumiwa huyo, alikamatwa juzi usiku akiwa mafichoni katika Eneo la Fuoni, baada ya taarifa za kiintelijensia kubaini kuwepo kwake.
Alisema makachero bado wanaendelea kumhoji mtuhumiwa huyo kwa lengo la kubaini mtandao wa matukio mbalimbali, yakiwemo ya tindikali, yaliyotokea siku za nyuma Visiwani.
Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, kunatokana na taarifa za siri za raia wema. Mhina alisema Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi kukamata watuhumiwa wengine.
Baadhi ya wananchi wa Zanzibar, walipongeza Jeshi la Polisi kukamata mtuhumiwa huyo na waliomba liendelee kusaka watuhumiwa wengine wa matukio mengine kama hayo siku za nyuma visiwani hapa.
Sheha huyo alimwagiwa tindikali saa 2.45 usiku Mei 22, mwaka jana, wakati Sheha huyo alipokuwa akirudi nyumbani akitoka kuchota maji nyumba jirani. Alijeruhiwa vibaya mgongoni, kifuani, sikioni na jicho la upande wa kulia.
Kutokana na tindikali hiyo kumuathiri vibaya, alilalazimika kusafirishwa nje ya nchi kwa matibabu zaidi.