WADAU WA MADINI WALALAMIKIA GHARAMA ZA LESENI....

Posted in
No comments
Tuesday, December 23, 2014 By danielmjema.blogspot.com


WADAU wa ununuzi wa madini ya kati (TASGEDO), na wale wa vyama vya wachimbaji nchini (REMAS) wamepinga hatua ya serikali kupandisha mara dufu gharama ya leseni za utafiti na uchimbaji na leseni za ununuzi wa madini ya Vito na Almasi nchini.

Mtaalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Kungulu Kasongi (aliyevaa shati jeupe) akiwaelezea wachimbaji wadogo namna uchorongaji wa miamba.
Wakizungumza jana na waandishi wa habari mjini Arusha , wadau hao wamesema ongezeko hilo la ada litaleta athari kiuchumi, kwani wanunuzi wakubwa na wadogo wa madini watashindwa kumudu gharama hizo, hasa ikizingatiwa wengi wao hawana mitaji mikubwa ya biashara.
Wamesema hatua ya Serikali kupandisha maradufu viwango vya gharama za leseni mbalimbali haukuzingatia au kufikiria kwamba, wachimbaji na wafanyabiashara wa vito na almasi hawana uwezo wa kuchangia pato la taifa, kwani hawana mitaji mikubwa.
Mwenyekiti wa TASGEDO nchini, Khamis Rioba, amesema hatua hiyo ya serikali kutowashirikisha wadau inalenga kuweka mazingira magumu na kufanya washindwe kuendelea na shughuli zao za uchimbaji na ununuzi wa madini na kwamba kwa namna moja ama nyingine imewafuta wazawa kwenye sekta hiyo.
Amesema madini ni rasilimali na hazina ya Taifa inayopaswa kuheshimiwa, hivyo ameishauri serikali kupunguza ama kurekebisha viwango hivyo na kuweka viwango stahiki vitakavyowezesha wazawa kumudu pasipo shaka.
Naye Katibu wa Chama cha wachimbaji madini Arusha “AREMA” Isaya Letema ameishauri serikali kuwa wiwango vya leseni za viwanja viwe kwa makampuni makubwa ya wawekezaji toka nje ya uchimbaji na uzalishaji wa madini kwani wana mitaji mikubwa ya uchimbaji na uzalishaji madini hapa nchini.
Amesema hivi karibuni serikali ilipandisha leseni ya utafiti wa madini kwa kila kiwanja kutoka shilingi 80,000 na shilingi 160,000 hadi kufikia shilingi 320,000 na shilingi 800,000 gharama za leseni ya wanunuzi wakubwa wa madini ya vito kutoka shilingi 250,000 hadi shilingi milioni 1.6 kwa mwaka.
Aidha maombi ya ada ya leseni hiyo ilikuwa ikitozwa shilingi 50,000 nayo imepanda na kufikia shilingi 320,000 kwa madini ya vito, pia maombi ya ufungaji wa madini kwenda nje ya nchi yaliyokuwa yanatozwa shilingi 50,000 nayo yamepanda hadi kutikia shilingi 320,000.
Sambamba na ada hizo za madini ya almasi yanayopatikana maeneo mbalimbali nchini nayo yamepanda kutoka sh. Milioni moja hadi sh. Milioni 1.2 wakati leseni za wanunuzi wa madini wa kati maarufu kama ‘mabroka’ nazo zimepanda kutoka sh. 115,500 hadi sh. 250,000.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .