WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUEPUKA LUGHA ZA CHUKI

No comments
Monday, May 18, 2015 By danielmjema.blogspot.com

Meza kuu. (Picha zote na Geofrey Adroph wa Pamoja blog).
Mshehereshaji wa Semina Bi. Rose Mwalongo akiwakaribisha washiriki wote waliofika kwenye semina ya siku mbili iliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali nchini la International Association of women in radio and television (AWRTT) kwa kushirikiana na Ethical Journalism Network ambapo wamewakutanisha wanahabari mbalimbali kutoka nchini Tanzania pamoja na nchi za Afrika.
Bi. Rose Haji Mwalimu kutoka IAWRT Tanzania akifungua semina kwa kwa washiriki ambao walikuwa ni wanahabari (hawapo pichani) mbalimbali kutoka nchini Tanzania pamoja na nchi za Afrika wa pili kutoka kushoto ni Rais wa IAWRT Bi. Rachael Nakitare, wa pili kutoka kulia ni Bi. Elisabeth Scwabe-Hansen pamoja na Mkurugenzi wa Ethical Journalism Network (EJN).
Rais wa IAWRT Bi. Rachael Nakitare akitoa semina kwa wanahabari namna ya kusimama katika ukweli na uwazi na pia kuepuka lugha ambazo zinaweza kuleta chuki kwa jamii, na baadae kusababisha machafuko kwenye Uchaguzi mkuu wa 2015.
Bi. Elisabeth Scwabe-Hansen kutoka ubalozi wa Norway akiwasisitiza washiriki wa semina hiyo kuwa makini kipindi chote wanapochukua au kutafuta taarifa ili kuondoa vurugu kwa nchi hasa Tanzania inayotegemea kufanya uchaguzi mwaka huu.
Mkurugenzi wa Ethical Journalism Network (EJN), Aidan White akitoa semina kwa wanahabari pamoja na wadau wa habari (hawapo pichani) kuhusu matumizi mazuri ya uandishi hasa kwenye hiki kipindi cha Uchaguzi.
Baadhi ya washiriki wa semina.
Rais wa Shirikisho la waandishi wa Habari Afrika (FAJ), Mohamed Garba.
Mkurugenzi wa Uwezeshashi na Uwajibikaji wa LHRC, Bi. Imelda Lulu Urio akielezea kuhusu vyombo vya habari vya Tanzania vilivyoanza kuonekana kama kuna aina ya lugha ambazo hazikuwepo hapo awali ambapo amesema kuwa ni wakati sasa wa kuanza kuzuia maana zinaleta chuki kwa taifa hasa suala la udini ambalo limeonekana kushika kasi hapa chini Tanzania.
Bi. Irene Burungi Mugisha kutoka IAWRT nchini Uganda akizungumza jambo.
Wadau wakifuatilia mada kwa umakini.
Mhariri mkuu wa gazeti la The New Times la nchini Rwanda, Bw. Kennedy Ndahiro akitoa mada kwa wanahabari pamoja na wadau wa habari waliohudhuria kwenye semina ya matumizi mazuri ya vyombo vya habari kuelekea uchaguzi mkuu unaotegemea kufanyika mwaka huu.
Rais wa Umoja wa waandishi nchini Uganda, Bi. Lucy Ekadu akiwaasa waandishi wa habari kuwa makini katika utoaji wa habari katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu unaotegemea kufanyika mwaka huu na pia kutoa elimu ya msingi kwa wanahabari ili kutochochea vurugu.
Mhadhiri kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Ayoub Rioba akitoa semina kwa washiriki (hawapo pichani) akiwasilisha mada yake kwenye semina iliyofanyika kwenye hoteli ya Peacock jijini Dar.
Mshiriki Borry Mbaraka akiuliza swali kwa watoa mada.
Rais wa IAWRT, Bi. Rachael Nakitare (wa tatu kutoka kushoto) akiuliza swali kwa mtoa mada (hayupo pichani).
Mtafiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Patience Mlowe akiwasilisha mada yake kwa wanahabari(hawapo pichani).
Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima, Neville Meena akiuliza swali kwa mmoja wa watoa mada wakati wa semina iliyofanyika jana katika hoteli ya Peacock jijini Dar.
Mweka hazina kutoka IAWRT Tanzania, Razia Mwawanga akikazia jambo kwenye semina ya wanahabari.
Wadau wakifuatilia kwa umakini mada.
Washiriki wa Semina hiyo wakiwa katika picha ya pamoja. Na Mwandishi wetu Ikiwa Tanzania inajiandaa kwa ajili ya zoezi la uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, waandishi wa habari nchini wameaswa kujiepusha na lugha za chuki pamoja na uchochezi kipindi chote cha uchaguzi jambo ambalo linaweza kusababisha machafuko kama inavyoonekana katika nchi mbalimbali barani Africa na duniani. Rai hiyo imetolewa jana jijini Dar es salaam katika semina ya siku mbili iliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali nchini la International Association of Women in Radio and Television (IAWRT) kwa kushirikiana na Ethical Journalism Network (EJN) ambapo wamewakutanisha wanahabari mbalimbali kutoka nchini Tanzania pamoja na nchi za Afrika mashariki kwa lengo la kujadili masuala yanayohusiana na lugha za chuki kwa vyombo vya habari vya Afrika pamoja na madhara yake kwa wananchi. Akifungua warsha hiyo mgeni rasmi ambaye ni Raisi wa shirikisho la wanahabari Africa (FAJ) Bw. Mohamed Gabra amesema kuwa moja ya mambo ambayo yamekuwa yakisababisha machafuko makubwa katika nchi nyingi za Afrika na duniani kwa ujumla ni lugha zinazotumika na wanahabari wakati wakiripori baadhi ya habari lugha ambazo amesema kuwa zimekuwa zikileta chuki baina ya watu na mwisho wake kusababisha madhara makubwa ambayo yangeweza kuepukika kama hatua zingechukuliwa mapema. Ametolea mifano kwa nchi kama Rwanda, Kenya, na nchi nyingine za ulaya ambazo zimewahi kuingia katika machafuko ya kisiasa katika kipindi cha uchaguzi kutokana na vyombo vya habari pamoja na wanahabari wenyewe kutumia kalamu zao kuwajengea chuki wananchi na mwisho kusababisha kuibuka kwa machafuko makubwa. Amesema kuwa ili kuhakikisha kuwa Tanzania inafanya uchaguzi mkuu kwa mafanikio na amani ni lazima wanahabari wahakikishe kuwa wanasimama kwenye ukweli na kuhakikisha kuwa wanawaambia wananchi kile ambacho kinatokea na sio kujenga na kutengezeza maneno ambayo mwisho yatasababisha chuki kwa watanzania. Awali akizungumza wakati wa kufungua warsha hiyo Rais wa (IAWRT) Bi. Rachael Nakitare amesema kuwa ni lazima kipindi hiki cha Tanzania kuelekea uchaguzi mkuu ni kipindi cha wanahabari kusimama katika ukweli,uwazi na kuepuka lugha ambazo zinaweza kuleta chuki kwa jamii,na baadae kusababisha machafuko. Baadhi ya watu waliotoa mada katika warsha hiyo ni pamoja na wakili na Mkurugenzi wa uwezeshaji na uwajibikaji kutoka kituo cha sheria na haki za binadamu LHRC Bi. Imelda Lulu Urio ambapo pamoja na mambo mengine ameelezea jinsi vyombo vya habari vya Tanzania vimeanza kuonekana kama kuna aina ya lugha ambazo hazikuwepo hapo awali ambapo amesema kuwa ni wakati sasa wa kuanza kuzuia mambo hayo ili kuepuka mambo makubwa ambayo yanaweza kujitokeza hapo baadae. Wengine waliopata nafasi ya kuchangia katika warsha hiyo ni mwandishi mkongwe nchini ambaye ni Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Dk. Ayoub Rioba ambapo amesema kuwa katika chaguzi mbalimbali katika nchi za Afrika kwa sasa wanasiasa wamekuwa wakiwatumia wanahabari kutaka kujinufaisha wao kisiasa bila kujali madhara ambayo yanaweze kutokea endapo wanahabari watakiuka maadili ya taaluma zao. Baadhi ya wanahabari kutoka mataifa ya nje ya Tanzania kama Kenya, Uganda,wamesema kuwa hakuna tofauti kubwa sana kati ya ufanyaji wa kazi za wanahabari zinazofanywa nchini Tanzania na mataifa yao bali tofauti iliyopo ni sheria zinazowaongoza wanahari katika mataifa hayo.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .