CCM: PANGA LA URAIS KUHAMIA UBUNGE
Posted in
Habari na Jicho Pevu la Kijiwe
No comments
Tuesday, August 4, 2015
By
danielmjema.blogspot.com
Dar es Salaam. Chama cha
Mapinduzi (CCM), kimesema kitatumia ‘panga’ lilelile lililotumika
kumpata mgombea wake wa urais katika kuchuja wagombea ubunge na udiwani
kupitia vikao vyake halali ili kupata wagombea safi.
Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnaye alisema hayo jana Dar es Salaam
katika mkutano na waandishi wa habari, kuzungumzia mchakato wa vikao
vya kamati za chama hicho ili kupata wagombea wa ubunge, uwakilishi na
udiwani baada ya mchakato wa kura za maoni kukamilika.
Alisema
mchakato huo utaanza kwa kikao cha Kamati Maalumu ya CCM Agosti 6 na 7
kuchuja na kupitisha wagombea ubunge na uwakilishi. Agosti 8 na 9,
Sekretarieti itakutana ikifuatiwa na Kamati Kuu pia kwa siku mbili kabla
ya Halmashauri Kuu kukutana Agosti 12 na 13 kuteua wagombea ubunge na
uwakilishi.
“Kura za maoni siyo mwisho wa safari, ni
hatua ya kwanza ya kuona ni nani anayekubalika… siyo kibali cha
kupeperusha bendera ya CCM, kama kuna upungufu vikao vitachukua hatua.
Kura ya maoni si kigezo… kama wamecheza rafu au kutumia rushwa, hata
kama wameshinda kwa kura nyingi, ikithibitika wanaweza kuondolewa,”
alisema Nape na kuongeza:
“Tutafanya kama ilivyokuwa
kwa wagombea urais, kama maadili hayakufuatwa wanaweza kuondolewa siyo
tu wa kwanza, hata wanne, hata kufuta matokeo. Tutachukua hatua kwenye
ubunge, tutachukua hatua kwenye udiwani kwa wale watakaojihusisha na
rushwa. Hawatapata nafasi ya uteuzi kwenye chama chetu. Hatuna muda wa
kuanza kuosha watu na madodoki.”
Alikumbusha jinsi
chama hicho kilivyomteua Dk Khamis Kigwangallah kuwania ubunge wa Nzega
alikoteuliwa licha ya kushika nafasi ya tatu katika kura ya maoni.
Changamoto kura za maoni
Kuhusu
changamoto kwenye upigaji kura za maoni ikiwamo vitendo vya rushwa,
Nape alisema kwa takwimu walizonazo, changamoto zilizojitokeza ni kidogo
ikilinganishwa na miaka ya nyuma... “Hii ni kwa sababu tumeboresha
utaratibu tofauti na huko nyuma. Maeneo mengi yamemaliza na hata yale
ambayo yamekuwa na kasoro za hapa na pale tumezitatua.
“…Kura
za maoni katika chama chetu zimetoa demokrasia na bila shaka
tumefundisha vyama vingine. Vyama vingi vinatoa wagombea mfukoni, lakini
sisi tunawapeleka kwa wanachama wanapigiwa kura,” alisema Nape.
Vigogo kuanguka
Alisema
kuwa kutokana na kukua kwa demokrasia katika chama hicho na kujenga
mfumo mzuri zaidi wa upigaji kura za maoni, hata vigogo wasiofanya
vizuri wameanguka katika kura za maoni. Kauli hiyo ya
Nape imekuja huku kukiwa na ripoti ya baadhi ya mawaziri na wabunge
wanaomaliza muda wao kuanguka katika kura za maoni.
Vigogo kuhama CCM
Alipoulizwa
kuhusu kuhama chama hicho kwa waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na
Mbunge wa Segerea, Dk Makongoro Mahanga na wanaCCM wengine, Nape alisema
siyo jambo la ajabu na kwamba si wa kwanza na wala hawatakuwa wa
mwisho. “Wapo wanaotoka CCM kwenda vyama vingine na wapo wanaotoka vyama
vingine na kuja CCM. Lakini niseme tu kwamba wapo ambao wanataka
uongozi na wapo ambao wanataka kwenda kuongoza watu:
“Anayetaka
kuongoza watu ni mvumilivu, mtulivu na hufuata taratibu. Lakini wapo
ambao lengo siyo kwenda kuongoza watu, lengo ni masilahi binafsi.
Wakikosa uongozi huonyesha tabia zao waziwazi.”
Source: Mwananchi
Source: Mwananchi
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :