KUMBE hata wazungu wameanza kumuiga Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli. Ndivyo ilivyotokea juzi jijini
London baada ya kocha mpya wa Chelsea, Antonio Conte kufanya ziara ya
ghafla katika uwanja wa mazoezi wa timu hiyo.
Conte hakutarajiwa kufanya ziara hiyo licha ya kutangazwa kuwa kocha
mkuu wa Chelsea Jumatatu kutokana na ukweli kwamba kocha wa muda wa
sasa, Guus Hiddink alikuwa mazoezini na wachezaji wake wakijiandaa na
mechi zinazofuata.
Conte alitambulishwa kwa wachezaji wote wa Chelsea juzi na
anatazamiwa kufanya vikao vya siri na kila mchezaji ambaye anataka
kuondoka katika kikosi hicho kilichovurunda msimu huu kwa ajili ya
kuwapa maoni yake.
Wachezaji walishangazwa na ujio wa Conte, ambaye mpaka sasa ni kocha
wa timu ya taifa ya Italia na anatazamiwa kukiongoza kikosi hicho katika
michuano ya Euro 2016 nchini Ufaransa. Aliwasili katika uwanja wa
mazoezi wa Chelsea, Cobham akiwa na Mkurugenzi wa ufundi wa Chelsea,
Michael Emenalo.
Conte anataka kujua wachezaji wanaotaka kuondoka kabla ya kukijenga
upya kikosi chake na anatazamiwa kukutana na mastaa Eden Hazard, John
Terry, Nemanja Matic na Diego Costa ambao hatima zao zipo shakani
Stamford Bridge.
Hazard, ambaye anaendelea kujitibu na tatizo la nyonga, hana uhakika
na hali yake ya baadaye Stamford Bridge huku akiwa anahusishwa na klabu
za Paris Saint-Germain na Real Madrid ambazo zimedaiwa kumtaka.
Matic amekuwa akikerwa na maendeleo yake msimu huu baada ya kung’ara
msimu uliopita ambapo alisaidia kwa kiasi kikubwa kutwaa ubingwa wa Ligi
Kuu ya England na amekiri kwamba yupo tayari kuondoka huku Diego Costa
akivutika na uhamisho wa kurudi Atletico Madrid.
Nahodha John Terry amerudisha matumaini ya kubaki klabuni licha ya
kuonyeshwa mlango wa kutokea Januari mwaka huu baada ya Chelsea
kuthibitisha kwamba haitampa mkataba mpya. Hata hivyo Conte anaweza
kuamuru kuwa Terry mwenye umri wa miaka 35 aendelee kwa msimu mmoja
zaidi.
Vile vile kumeanza kuwa na wasiwasi na hali ya baadaye ya golikipa
namba moja wa Chelsea, Thibaut Courtois ambaye inadaiwa kuwa klabu za
Barcelona na Real Madrid zimeanza kumfukuzia kipa huyo wa kimataifa wa
Ubelgiji.
Baadhi ya wafanyakazi wa uwanja huo wa mazoezi pamoja na benchi la
ufundi la Chelsea walishangazwa na ujio huo licha ya kocha Hiddink
kuendelea kukiweka sawa kikosi chake kwa ajili ya pambano lijalo dhidi
ya Swansea.
Hata hivyo inadaiwa kuwa Conte alikuwa anataka kupata picha halisi ya
kikosi hicho kabla ya kujikita zaidi katika majukumu yake ya timu ya
taifa nchini Ufaransa katika michuano ya Euro 2016 ili awe na sehemu ya
kuanzia mara baada ya kumalizika kwa michuano hiyo.
Inadaiwa kuwa tayari ameanza kuwaandama wachezaji wa kukiimarisha
kikosi cha Chelsea ambapo mmoja kati ya wachezaji anaowasaka ni kiungo
wa nguvu wa AS Roma na timu ya taifa ya Ubelgiji, Radja Nainggolan.
Conte alipaa kwenda England katika siku ambayo waendesha mashkata
nchini Italia wakitaka afungiwe miezi sita na kutozwa faini ya Pauni
6,000 kama akipatikana na hatia ya kupanga matokeo katika kipindi chake
alichokuwa kocha wa Siena nchini humo.
Amekubali kusaini mkataba wa miaka mitatu na nusu Chelsea huku
akilipwa dau la pauni 6.5 kwa mwaka akichukua jumla nafasi ya kocha wa
zamani wa Chelsea, Jose Mourinho ambaye alitimuliwa Desemba mwaka jana
kufuatia matokeo mabovu ya Chelsea katika michuano mbalimbali.

No comments:
Post a Comment