Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Kenya Mheshimiwa Raila Amoro Odinga
amemtembelea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli aliyepo mapumzikoni katika Kijiji cha Kilimani, Wilaya ya Chato
Mkoani Geita.
Mheshimiwa Odinga ambaye ameongozana na mkewe Mama Ida Odinga na
Binti yake Winnie Raila Odinga, wametua kwa Helkopta katika uwanja wa
Shule ya sekondari ya Chato leo tarehe 02 April, 2016 majira ya saa 11
jioni na baadaye kuelekea nyumbani kwa Rais Magufuli ambako wamepokelewa
na wenyeji wao Rais Magufuli mwenyewe na Mkewe Mama Janeth Magufuli.
Akizungumza mara baada ya kuwasili Chato, Mheshimiwa Raila Odinga
amesema yeye na familia yake wapo likizo na wamekuja kumtembelea rafiki
wa familia yao, kwa lengo la kumsalimia.
"Nimekuja kupumzika na nimekuja na Mama na Mtoto wangu wa
kike, na vilevile kuja kutoa pongezi kwa ndugu yangu kwani tangu
achaguliwe sijakuja hapa Chato, na nilisema siendi Dar es salaam
nitakuja hapahapa Chato" Alisema Mheshimiwa Odinga.
Pamoja na kukutana na Rais Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli,
Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya Mheshimiwa Raila Odinga pia amemsalimu Mama
Mzazi wa Rais Bibi Suzana Joseph Magufuli na pia amezulu Makaburi
walimozikwa wanafamilia wa Rais, akiwemo Baba Mzazi Mzee Joseph
Magufuli.

No comments:
Post a Comment