UCHAGUZI TOC NI FURSA YA KUDEKI “MATAPISHI” YA OLIMPIKI 2012
Posted in
No comments
Thursday, November 15, 2012
By
danielmjema.blogspot.com
Kama ulimiss makala haya yaliyochipishwa katika Gazeti lako pendwa la MTANZANIA la Tarehe 26 Octoba mwaka huu. yasome hapa na uweze kupata uelewa wa muelekeo wetu katika michezo!!
Na Fadhili Athumani, Moshi
Mitaani huwa kuna msemo usemao ukiona vyaelea ujue
vimeundwa, msemo huu umejizolea umaarufu hasahasa pale ambapo kuna jambo nzuri
limetokea na nadra kukuta linatumika panapootokea matatazo au mapungufu yoyote
yale katika jamii
Naamini kila mwanamichezo anafahamu kwamba mwaka huu 2012 ni
mwaka wa uchaguzi na bila ajizi vyama vyote vinavyosimamia maswala ya michezo
hapa nchini kwa kuzingatia katiba zao vimekuwa katika hekaheka za kuhakikisha
kuwa wanatumia vema fursa hii ya kuwaadhibu baadhi ya viongozi wao katika
uongozi unaomaliza muda wao au kuwapongeza wacha[pa kazi kwa kuwachagua tena
kuendelea kuwatumikia
Baada ya TFF kupanga kufanya uchaguzi Desemba hii, TAFCA
wakitazamia kufanya ya kwao Novemba 25 huku vyma vya mikoani nazo zikihakikisha
zinafanya chaguzi zao mapema kupisha chaguzi za kitaifa, kamati ya Olimpiki
nchini (TOC) nayo imetangaza tarehe ya uchaguzi wa viongozi wake taifa baada ya
viongozi walioko madarakani kumaliza muda wao, uchguzi ambao kwa mujibu wa
katibu mkuu anayemaliza muda wake, Filbert Bayi, utafanyika Desemba 8 mwaka
huu, mkoani Dodoma
![]() |
BAADHI YA WASHIRIKI WA OLIMPIKI-LONDON 2012 |
Naomba niweke wazi
mapema kwamba mimi binafsi yangu sina tatizo na nia ya waheshimiwa hawa
kugombea tena kuongoza TOC katika maswala mazima ya kuendesha michezo na kusimamia
program za kamati hiyo hapa nchini lakini naomba niwakumbushe tu kuwa “ukiona
pana fuka moshi ujue pana moto hata kama ni kijinga” na kuwakumbusha kwa nia
njema tu wasisahau kazi iliyoko mbele yao ya kudeki matapishi ya wawakilishi
wetu katika mashindano ya Olimpiki 2012 yaliyomalizika hivi karibuni jijini
London.
Katika uchaguzi wa Desemba ambao naamini lengo lake ni
kurekebisha makosa tuliyoyafanya hapo nyuma, kamati ya TOC inayomaliza muda
wake chini ya Mwenyekiti Gulam Rashid imeshabainisha majina ya wajumbe wanne wa
kamisheni itakaosimamia uchaguzi na kuhakikisha kwamba kile kilichodhamiriwa
kinatimia kwa kutupa viongozi makini kwa kufanya uchaguzi wa huru na haki,
itafanya kazi yake na naamini kuwa timu hiyo ya Harrison Chauro, Hamis Ally
Mzee, Abdalla Juma na aliyekuwa mwenyekiti wa timu ya Yanga, Loyd Nchunga
haitafanya makosa
Kila la kheri kwa wagombea wote wa nafasi ya Uenyekiti,
Makamu mwenyekiti, Katibu mkuu, Katibu msaidizi, Mwekahazina, Mweka Hazina
msaidizi na wajumbe kumi wa mkutano mkuu, watano kutoka Bara na watano wengine
kutoka Visiwani, nawatakia kila la kheri mara nyingine katika azma yenu ya
dhati ya kutaka kuleta mageuzi ndani ya TOC na ikiwezekana kuhakikisha katika
mashindano yajayo ya Olimpiki aibu tuliyoipata katika mashindano ya mwaka huu
haijirudii tena ambapo washirki wetu waliishia tu kuwa watalii!
Namjua wengi watashangaa kwa nini nimesisitizia kuwapongeza
wagombea waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali ndani ya TOC nakuwatakia kila
la Kheri katika uchaguzi huo wa Desemba, sifanyi kwa sababu ya kuwapigia
kampeni, la hasha, natumia fursa yangu kama mwanamichezo kuwa kumbusha
watanzania wote wenye uchungu na nchi yao pamoja na viongozi ndani ya TOC
kuhusu umuhimu wa kuweka matakwa ya Taifa mbele kwanza halafu yafuate matakwa
yetu binafsi na hili naomba wagombea wote ndani ya TOC walitilie maanani
Nakumbuka baada ya Kenya kufanya vibaya katika Olimpiki ya
mwaka huu kwa kujinyakulia medali kumi na moja tu katika michezo yote
waliyoshiriki, wanamichezo wan chi hiyo wakiongozwa na serikali ya Rais Kibaki,
walichukizwa na matokeo hayo manbaya kuwahi kutokea katika historia ya Kenya
katika mashindano hayo na mengine mengi ya
kimataifa, kiasi cha kuamua kuunda Tume ya kuchunguza sababu za wanamichezo wake kufanya vibaya
Nakumbuka katika Hotuba yake, mara baada ya Timu hiyo
kurejea Nyumbani, Rais Kibaki alisikika akisema kuwa kitendo cha nchi yake
kufanya vibaya katika Mashindano ya Olimpiki ambayo yeye kwa mtazamo wake
ilikuwa ni fursa ya kuitangaza nchi ya Kenya, ni tusi kubwa kwa Uhuru wa Nchi
hiyo, ni tusi kwa Wananchi walipa kodi wa Nchi hiyo, kutokana na Fedha zao
kutumika katika Kugharamia Safari ya Wanamichezo hao
Rais Kibaki anasema, ni aibu kwa nchi yenye Rasilimali zote
kupata matokeo mabaya kama hayo, huku akiishukia kamati ya Olimpiki ya nchi
hiyo iliyoko chini ya Uenyekiti wa mwanariadha Mkongwe, Kipchoge Keino, pamoja
na Wizara yenye Dhamana ya Michezo na kuwalaumu kwa kuchangia kufanya vibaya
kwa nchi ya Kenya katika Michezo hiyo kwa kushindwa kuandaa kikosi imara nay a
kiushindani
Sio Kibaki tu, kwani hata Wasanii wa Nchi hiyo ambao ni kio
cha Jamii, hawakuachwa nyuma katika kukosoa, kuzungumza na kukemea yale ambayo
wao waliona wanafaa kuyakemea kama wawakilishi wa wengi kutokana na kufanya
vibaya kwa kikosi cha Olimpiki na mmoja wao ni msanii, Hubert Nakitare maarufu,
Nonini , aliyesikika waziwazi akiikosoa kamati ya Olimpiki ya Kenya (NOCK) kwa
kuchangia kufanya kwao Vibaya katika michezo hiyo kwa kuendekeza migogoro
isiyokuwa na lazima
Wakati Rais Kibaki na Msanii Nonini wakijitokeza kuishtumu,
cham,a cha Riadha ya Kenya(AK),na Kamati ya Olimpiki nchini mwao, cha
kushangaza na kusikisha ni kwamba pamoja na Tanzania kufanya utumbo katika
michezo ya London, hakuna na kiongozi hata mmoja, sio Rais, Waziri wala Msanii
yeyote aliyejitokeza kuzungumza aibu tuliyoipata katika michezo ile na cha
kusikitisha zaidi ni kuona viongozi wetu wa sasa ndani ya TOC wakitokea matamko
yakuhuzunisha na kukatisha Tamaa kwa kusema kuwa hata kule kushiriki tu ni sifa
kwa nchi, kweli?
Kuna mtu mmoja ambaye mwanzoni kutokana na kauli zake mimi
binafsi nilikuwa namuona kama kachanganyikiwa, naomba nitumie makala haya
kumtaka radhi ndugu yangu, mwanariadha maarufu nchini, aliyeliletea taifa
heshima katika enzi zake na nathubutu kusema bila woga wowote kuwa, Wilhelm
Gidabudayi, ni mwanamichezo wa kweli na
mfano wa kuigwa kutokana na kujitolea kwake kuzungumza na kukemea yale ambayo
yeye kwa upeo wake aliona yanafaa kuzungumzwa ili watanzania waweze kufahamu
uozo ulioko ndani ya TOC
Gidabudayi katika kutetea kauli zake aliwahi kuhoji
maandalizi na uteuzi wa kikosi kilichotuwakilisha katika michezo ya Olimpiki
kwa kusema kwamba kudai kwamba kikosi hicho hakikuwa tayari kushiriki
mashindano hayo na nakumbuka Gidabudayi alifikia mahali na kudai kikosi kutwa
medali yoyote katika michuano hiyo ilikuwa ni ndoto, akitishia hadi kuchoma
vyeti vyake vyote endapo Tanzania ingerudi na medali hata moja katika michuano,
mwanzoni nilimwona Gidabudayi kama mchochezi na msaliti asiyefaa katika jamii,
lakini ‘Mungu sio Athumani’, maneno ya Gidabudayi hata hayajakauka nadhani kila
anelewa kilichofuata?!
Nakumbuka na nikimnuku Gidabudayi aliwahi kusikika akisema,”
TOC ya sasa imeoza na kama kweli Watanzania wana hamu ya kufanya vizuri kwenye
michuano ijayo ya Olimpiki ni lazima kitu kifanyike kwenye ile kamati tofauti
na hapo ni kutwanga maji kwenye kinu, nashauri Wizara ya michezo ishtuke kwa
nini TOC inasema haihusiki? Maana kama wadau wakubwa na viongozi wa michezo
hapa nchini, TOC iende eneo la tukio(mashinani kutafuta washiriki wa Olimpiki
2012), kuliko kukaa kusubiri iletewe wanamichezo ndipo iwaandae,"
Mwandishi
wa Tanzania Daima, Irene Mark akimkaribisha katika Chumba cha Habari
Katibu wa Hanang Sports Club, Wilhelm Gidabuday walipotembelea ofisi za
gazeti hilo leo.
Sasa kinachonipa wazimu zaidi ni ile kauli ya TOC kupitia Katibu wake, Filbert Bayi kuwa TOC kama kamati ya Olimpiki nchini haiusiki katika maandalizi ya timu na kuongeza kuwa maandalizi ya kikosi ya timu zinazoenda katika Olimpiki kuanzia katika uteuzi wa wanamichezo ni kazi ya Chama cha Riadha (RT) kwa kushirikiana na vyama vingine na kkwamba kazi ya TOC ni kuratibu safari ya kikosi! Hapa Napata kichefuchefu kutokana kupata maswali mengi yasiyokuwa na maji kwamba kama TOC haihusiki na shughuli hizo walizozitaja wao Basi kazi yao hasa ni nini? na kama hawahusiki na maandalizi ya Kikosi hicho nyeti kuna umuhimu gani ya wao kuwepo? Hapa kwa kweli naomba maelekezo
Ni matumaini yangu kwamba wakati tunaingia katika uchaguzi
mkuu wa TOC, mwezi Desemba mwaka huu, tutakumbuka umuhimu wa uchaguzi huo
katika kubadli mwelekeo wa michezo hapa nchini na kurudia enzi za nyuma ambapo
Taifa, iliweza kutoa wanamichezo wazuri kama, Wilhelm Gidabudayi, Filbert Bayi
na wengine wengi ambao naamini nikianza kuwataja hapa tutakesha ambao kwa
kujituma walithubutu kutoa upinzani kwa wanaridha nguli kama Kipchoge Keino na
wengineo
Naamini kama kutakuwa na mikakati mizuri katika uongozi wa
michezo kwa kuanzia kuingiza watu makini ndani ya TOC, kile kilichotokea katika
michezo ya juzi ya Olimpiki, mashindano ya Riadha ya Kilimanjaro Marathon msimu
wa 12, yaliyoshuhudia nchi jirani ya Kenya wakiondoka na medali yote mbele ya
macho yetu na katika Ardhi yetu, hakitajirudia tena!
Mwisho kabisa niwatakie kila la kheri wagombea wote wa
nafasi mbalimbli ya uongozi ndani ya kamati ya Olimpiki (TOC), nikitegemea
kwamba ujio wao utakuwa ni mwanga na mwanzo mpya hapa nchini, tukumbuke kwamba,
Wilhelm Gidabudayi, Filbert Bayi, Gulam Rashid na yeyote Yule ambaye
anajitambua kama mwanamichezo, sote kwa pamoja kazi yetu ni kujenga nyumba
moja; Tanzania. Na naamini kwa hayo nimewasilisha hoja ya Michezo ni Afya na
Ajira.Mungu ibariki Tanzania!
0756038214/0654724337
MWISHO
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :