DUH! ULEVI NOMAAA!!!
Posted in
No comments
Thursday, June 14, 2012
By
danielmjema.blogspot.com

Mtu mmoja akiwa amelala porini baada ya kuzidiwa na kilevi
Pombe
ni kiburudisho muhimu sana kwa walio wengi. Mamilioni ya wanaume na
wanawake ulimwenguni wanatumia au wamewahi kutumia pombe wakati fulani
katika maisha yao.
Umaarufu
wa pombe bila shaka unatokana na uwezo wake katika kumfanya mtumiaji
ajisikie vizuri na kusahau matatizo yanayo mkabili japo kwa muda. Pombe
huondoa aibu, huufanya mwili kusisimka na kuleta furaha.
Kwa
sababu hiyo pombe ni kimbilio la watu wengi wenye furaha, na wenye
matatizo na shida za aina mbalimbali. Kwa mtazamo wa haraka haraka
tunaweza kusema pombe ni nzuri na inafaa kutumiwa kama kiburudisho
endapo mtumiaji atakuwa na kiasi na kuitumia kwa namna inayofaa.
Kwa
upande mwingine pombe ni kitu kibaya sana kwani madhara yake yanazidi
faida na hasa kwa kuzingatia kwamba ni watu wachache sana wanaoweza
kufuata mashalti ya utumiaji kileo kama inavyotakiwa. Leo hii pombe ni
chanzo kikubwa cha ajali za barabarani zinazo sababisha mauaji ya maelfu
ya watu wasiokuwa na hatia.
Pombe ni hatari kwa wajawazito
Pombe
pia ni chanzo kikubwa cha matatizo ya kijamii ikiwa ni pamoja na
kusambaratika kwa familia, na ongezeko la talaka jambo linalosababisha
mateso makubwa kwa watoto.
Aidha,
pombe inachangia sana katika kuleta umaskini kwa mtu binafsi, familia
na hata taifa. Pombe husababisha uzembe kazini, kupunguza uwezo wa
kufikiri na kutoa maamuzi na kusababisha madhara katika ubongo hasa kwa
watumiaji wenye umri mdogo (watoto).
Pombe
pia husababisha matatizo ya kiafya kwa watoto walioko tumboni (ambao
hawajazaliwa). Wanawake wajawazito wanaotumia pombe hujiweka katika
hatari kubwa ya kuharibu akili (ubongo) za watoto wanaowabeba matumboni
mwao.
Ni
kwa sababu hiyo nchi zilizoendelea (kama Marekani na baadhi ya nchi za
ulaya) zimepiga marufuku uuzaji wa pombe kwa vijana wenye umri chini ya
miaka 18, na zinaendesha kampeni za kuwaelimisha akina mama kuepuka
matumizi ya pombe katika kipindi chote cha ujauzito.
Pamoja
na madhara makubwa yanayoletwa na unywaji wa pombe, ni ajabu kwamba
nchini mwetu pombe tumeigeuza kuwa sehemu ya maisha. Watu wengi wenye
kipato cha kawaida hujiingiza katika unywaji pombe wa kupindukia
kutokana na kasumba iliyojengeka nchini mwetu kwamba watu wanaokunywa
pombe kila siku wana pesa nyingi. Watu wanaojiingiza katika ulevi
hufanya hivyo kwa kudhani wanainua 'status' zao.
Wengi
wa walevi hawa hujikakamua kununua pombe zenye bei kubwa zaidi ili
kuonesha kuwa wana pesa na kuwakoga wasiokuwa nazo. Baadhi ya wanywaji
hufikia hatua ya kuweka bili katika mabaa na store zinazouza pombe ili
waweze kunywa pasipo kukosa hata kama hawana pesa (na kulipa mwisho wa
mwezi) jambo linalowaingiza katika umaskini wa kujitakia pasipo kujua.
Ni
kutokana na ongezeko kubwa la wanywaji wa pombe makampuni mbalimbali
yanayo tengeneza na kusambaza vileo yameivamia Tanzania kwa nguvu na
kumwaga pombe za kila aina mitaani. Makampuni haya hujitengenezea faida
kubwa isiyoelezeka.
Aidha
wafanya biashara wengi nchini wameacha kuwekeza katika vitega uchumi
vingine vya kimaendeleo kama kilimo, ufugaji, viwanda vidogo vidogo,
elimu n.k na kugeukia biashara ya pombe ambayo inaelekea kutokuwa na
mpinzani katika kuingiza faida. Si ajabu kwamba katika miji yetu kuna
baa katika kila kona.
Mbaya
zaidi ni kwamba serikali haifanyi jitihada zozote kudhibiti uuzaji na
matumizi ya kileo katika nchi yetu (pengine kutokana na kodi kubwa
inayokusanya kutoka katika biashara ya vileo). Matokeo yake pombe huuzwa
kwa mtu yeyote bila kujali umri wake, muda wala mazingira inapouzwa
pombe hiyo.
Leo
hii makampuni makubwa yanayouza vileo ikiwa ni pamoja na kampuni ya TBL
yanafanya matangazo mengi ya kuwashawishi wananchi kunywa pombe bila
kujali matangazo hayo yanawavutia watoto wadogo. Hebu fikiri yale magari
yanayotangaza bia mitaani kwa kupiga muziki huku kina dada warembo
wakicheza mayenu na kugawa zawadi za bia kwa wananchi waliokusanyika.
Ni
hivi juzi tu kampuni maarufu ya bia nchini iliendesha tamasha kubwa la
muziki ambapo kiingilio ilikuwa kopo la bia ambayo mteja alipaswa
kuinunua uwanjani hapo. Katika tamasha hilo washiriki wengi walikuwa
vijana wadogo wenye umri chini ya miaka 18 ambao waliuziwa pombe bila
hofu wala aibu.
Ni
lazima tukubali ukweli kwamba pombe ni hatali kwa afya na maendeleo.
Ndio maana nchi zilizoendelea (Marekani, Ulaya na hata baadhi ya nchi za
kiarabu) zimeweka taratibu kali za kudhibiti matumizi ya vileo ikiwa ni
pamoja na kuzuia uuzaji wa pombe kwa vijana wenye umri chini ya miaka
21 (kwa USA), kuzuia unywaji wa pombe hadharani, kupanga masaa maalum ya
uuzaji wa pombe na kuzuia aina zote za matangazo ya pombe yanayo
walenga vijana wadogo.
Ni
jambo lililo dhahiri kwamba ulevi ni adui wa maendeleo na hivyo
kuendelea kujenga taifa la walevi ni hatari kwa maendeleo, afya na
usalama wa jamii yetu. Ni kwa sababu hiyo tunaishauri serikali kutoa
elimu kwa umma kuhusu madhara ya utumiaji vileo.
Aidha
ni vema serikali ikatunga sheria kali za kudhibiti uuzaji holela wa
vileo ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku uuzaji wa pombe kwa watoto
wenye umri chini ya miaka 18.Ni muhimu sheria hizo pia zifafanue aina ya
matangazo ambayo makampuni ya uuzaji vileo yanaruhusiwa kufanya ili
kudhibiti matangazo yanayowalenga vijana wadogo, na pia kutamka maeneo
na muda unaoruhusiwa kuuza vileo kisheria.
Kama
serikali isipochukua hatua za haraka kudhibiti ongezeko la walevi
nchini, si ajabu nchi yetu ikaendelea kudidimia katika wimbi kubwa la
umaskini wa kujitakia. Na watu wengi wataendelea kuamini kuwa serikali
inaendekeza ulevi ili wananchi wengi wasione hali ngumu ya maisha
iliyoko nchini na kuipigia kelele serikali.
Na Mwana Dikala
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako

0 MAOINI :