GAMA: "TUNZENI MAZINGIRA KWA FAIDA YA KESHO"
Posted in
No comments
Saturday, June 16, 2012
By
danielmjema.blogspot.com
KAMATI ya ushauri mkoani Kilimanjaro, RCC, imeazimia
kudhibiti uharibifu wa mazingira kwa kuweka mikakati thabiti ikiwemo kutunga
sheria ndogo ndogo elekezi kutokana na sheria mama ya mazingira inayosimamia
utunzaji wa mazingira katika maeneo yote ya hifadhi, makazi ya watu na maeneo
ya wazi nchini.
Maazimio hayo yanatokana na mapendekezo yaliyotolewa
katika kikao cha RCC mkoani hapo, kilichofanyika tarehe 29 Februari mwaka huu,
na taarifa ya warsha ya mazingira iliyofanyika tarehe 13 juni mwaka huu, na
kuhusisha wadau wa mazingira wa mkoa, wilaya, KINAPA, kata zote, vijiji na
taasisi zote za serikali kama vile TATeDO na UNDP.
Akiongea katika uwasilishwaji wa taarifa ya
utekelezaji kwa kila halmashauri za wilaya ya mkoa huo, mkuu wa mkoa wa
Kilimanjaro, Leonidas Gama, aliyepia mwenyekiti wa kamati ya ushauri ya mkoa RCC,
alisema kuwa, mkoa kwa kauli moja imeazimia kupinga uharibifu wa mazingira
pamoja na kutunza vyanzo vya maji ikiwemo mlima Kilimanjaro.
Gama alisema, katika maazimio hayo kamati ya ushauri
ya mkoa imeazimia kusitisha kwa muda, utoaji wa vibali vyote vya kukata miti ya
asili kwa ajili ya mbao au kuni, kusimamia na kutekeleza sheria zote za
mazingira kwa pamoja, kurudisha majukumu ya usimamizi wa eneo la nusu maili kwenye
usimamizi ya KINAPA, kutokana na uharibifu mkubwa kwa sasa kuanzia katika eneo
hilo.
Maazimio mengine yaliyowekwa ni, kuhakisha kuwa
elimu ya mazingira na sheria zake inatolewa kwa jamii kwa kushirikiana na mashirika
yasiyo ya kiserikali yanayoshughulikia mazingira ili kuharakisha zoezi la
Kudhibiti uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira kwa
kutumia nishati mbadala na majiko banifu.
Aidha Gama, alitoa agizo kwa halmashauri zote mkoani
Kilimanjaro, kutumia fedha zinazotolewa na wafadhili kwa kuendeleza zoezi la
upandaji miti na sio kulipa madeni ya awali yaliyotumika katika halmashauri
hizo kupandia miti kwani zoezi la awali la upandaji lilidhaminiwa na serikali.
Katika maazimio hayo pia, kamati ilitoa agizo kwa
halmashauri zote kusimamia vijiji vyote ili viandae mipango ya matumizi bora ya
ardhi na kuweka mipaka ya shughuli zote ambazo zinatekelezwa katika kijiji kama vile eneo la kilimo, hifadhi ya misitu, makazi
pamoja na maeneo ya malisho.
Na kijiweblog, moshi
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako

0 MAOINI :