Sunday, June 17, 2012

MWENYEKITI CCM LONGOI AWEKWA KITI MOTO


WANACHAMA wa chama cha mapinduzi CCM, tawi la longoi kijiji cha Longoi nguzo nne kata ya Machame weruweru wameulalamikia uongozi wa CCM katikia tawi hilo kwa kuuza eneo la chama kwa taasisi ya mradi wa maji sadi na salama wa mkalama bila ridha ya yao.

Tuhuma hizo, za matumizi mabaya ya mali ya chama zimeelekezwa kwa mwenyekiti wa CCM tawi la Longoi, Francis Shiyo, zikimlaumu kutoa eneo la chama kwa taasisi ya mradi wa maji bila ya ridhaa ya wanachama.

Wakiongea na MTANZANIA katika nyakati tofauti mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi CCM kata ya Machame weruweru, Raphael Munishi na Mjumbe wa mkutano mkuu CCM tawi la longoi, Lothi Pyuza walisema kuwa pamoja na kamati ya siasa ya chama kupinga utoaji wa eneo hilo alikataaa kukubaliana na maamuzi ya kamati.

Munishi alisema hapo awali, waliomba kupewa eneo hilo ili wajenge ofisi ya chama wakanyimwa lakini cha kushangaza jamaa hawa walipokuja eneo hilo lilitolewa haraka na kuongeza kwamba kilichowashangaza zaidi ni utaratibu uliotumika katika kuidhinisha eneo hilo kuchukuliwa.

Akizungumzia tuhuma hizo, mwenyekiti wa CCM Tawi la longoi, alikana tuhuma hizo na kusema kwamba mradi wa mkalama unaohusisha vijiji vitano vya mkalama, kawaya, Longoi, kikavu na mjengweni ulijenga ofisi zake hapo baada ya wanachama wote na kamati ya siasa kuridhia eneo hilo kupewa kwa mradi kutokana na kijiji cha longoi kuwa katikati hivyo kuwa kiunganishi cha vijiji vyote.


Meneja wa mradi wa mkalama, Godwin Iddo, alisema anashangaa kuona watu wanaingiza siasa katika miradi ya maendeleo kama hiyo na kusisitiza kwamba uwepo kwa ofisi hiyo katika eneo hilo kihalali na kuongeza kwamba ili kuthibitisha kuwa mradi uko hapo kihalali mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Hai akiongozana na mhandisi mkuu wa wilaya alifika na kubariki ujenzi wa ofisi hiyo.

Iddo alisema katika uzinduzi wa ofisi hiyo, uliofanyika tarehe 25 mei mwaka huu, mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama, aliyewakilishwa na mkuu wa wilaya ya Hai wakati huo, Norman Sigalla alisema ujenzi wa ofisi na kazi za mradi wa maji katika kijiji hicho ni moja katika utekelezaji wa sera za CCM kwa hiyo inashangaza kusikia mradi huo unawekewa pingamizi.

Hata hivyo katika mkutano uliofanyika hapo jana na kuongozwa na katibu wa chama cha mapinduzi wilaya ya Hai, Hassani Mtega, kilitoa hadi tarehe 28 juni mwaka huu kwa viongozi wa mradi wawe wameshaondoka katika eneo husika au wafanye utaratibu wa kukutana na uongozi wa CCM tawi la longoi ili kuangalia uwezekano wa kupata eneo lingine la kujengea ofisi yao.

MWISHO

No comments:

Post a Comment