Dk. Migiro atoa ya moyoni, Spika alia na viti maalumu

Posted in
No comments
Monday, August 6, 2012 By danielmjema.blogspot.com

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asharose Migiro, amesema ni kazi ngumu kufanya kazi katika umoja huo, kwa kuwa hakuna muda wa kupumzika.
asha rose migiro

Kutokana na hali hiyo, amesema siku za mwanzo kushika wadhifa huo, alikuwa akipata shida kwa kuwa alikuwa hajazoea kufanya kazi kwa muda wa saa 24.

Dk. Migiro aliyasema hayo mjini hapa juzi, alipokuwa akizungumza na wabunge wanawake waliokuwa wakiongozwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda.

“Kuna changamoto nyingi nilikubambana nazo na kubwa zaidi ni kwamba kule hakuna kulala, yaani unafanya kazi masaa 24.

“Kule unafanya kazi kuanzia Jumatatu hadi Jumatatu na hii inatokana na ukweli kwamba, Umoja wa Mataifa unashirikisha nchi ambazo zinatofautiana masaa.

“Kwa mfano, Marekani niliokuwa mimi inawezekana kukawa ni usiku, lakini kule kwa bosi wangu Ban Ki Moon ni asubuhi.

“Kwa maana hiyo, bosi wangu anapokuwa kwao akiamka asubuhi, anataka akutumie nyaraka fulani fulani, au mzungumze mambo ya kikazi, sasa huwezi kulala kwa sababu yeye kule aliko ni asubuhi ingawa wewe huku ni usiku.

“Kitu kingine ambacho ni cha ajabu sana kule ni kwamba hutakiwi kujiuguza, yaani ukisema unaumwa wenzetu kule wanaona ni kitu cha ajabu sana, wanakuchukua haraka haraka wanakupeleka hospitali.

“Sasa kama umejiuguza utagundulika tu maana utapimwa,” alisema Dk. Migiro na kuongeza.

“Kule kamwe huwezi kuwa mzembe, huwezi kusema eti leo nimechoka siwezi kuonana na wageni fulani, huwezi kujificha kamwe kwa sababu mawasiliano yako yote wanayafahamu, kule hakuna visingizio eti useme leo hakuna umeme, umeme upo masaa yote.

“Ila ninachoshukuru ni kwamba unapokuwa kazini unapewa vitu vingi sana vya kukufanya usiwe na mawazo, ingawa kuna wakati unaumia kwani unapofiwa na mtu wako wa karibu huwezi kusema ngoja niondoke, utalazimika kuvumilia tu, yaani inaumiza sana,” alisema Dk. Migiro na kuwachekesha wabunge waliokuwa ukumbini humo.

Pamoja na hayo, alisema kuteuliwa kwake kuwa Naibu Katibu Mkuu, hakukutokana na ujanja wake wala sifa zake, bali kulitokana na heshima ya Tanzania katika nyanja ya kimataifa.

“Tanzania huko nje inaheshimika sana na kuteuliwa kwangu siyo kwa sababu ya ujanja wangu, kwani hata baada ya kufika huko, nilikuwa nikifanya kazi ya kuratibu shughuli za maendeleo za mashirika yaliyo chini ya Umoja wa Mataifa.

“Chombo kile ni kikubwa sana na unapoingia huna muda wa kujifunza, kule ukifika moja kwa moja unaanza kazi na kwa bahati nzuri, kila kitu kiko wazi na ukishaanza kazi unapata ushirikiano kutoka kwa kila mtu,” alisema.

Wakati huo huo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliwataka wabunge wa viti maalum wajiandae kugombea majimbo, kwa kuwa heshima ya ubunge huo,
imeanza kushuka.



anna makinda
Alisema asilimia 30 ya ubunge wa viti maalum iliyopo sasa inatosha na ili ipatikane asilimia 50, asilimia 20 iliyobaki inatakiwa kupatikana kwa wabunge kugombea majimbo.

Katika maneno yake, Spika Makinda alijitolea mfano yeye mwenyewe jinsi alivyokumbana na vikwazo na pia akamtolea mfano Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama na Mbunge wa Busanda, Lolencia Bukwimba ambao walipambana na vikawazo na kuvishinda, wakati walipokuwa wakigombea ubunge.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .