Hillary Clinton apigia debe demokrasia Afrika
Posted in
No comments
Friday, August 3, 2012
By
danielmjema.blogspot.com
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hillary Clinton
amewahimiza viongozi wa kiafrika kuimarisha uhusiano na nchi zinazojali
misingi ya demokrasia , na kuzipa kisogo zile zinazoweka mbele tu
maslahi ya kibiashara.
Ushauri huo wa Bi Clinton kwa viongozi wa Kiafrika, ulitafsiriwa
kuilenga China bila kuitaja kwa jina, ambayo imekuwa ikikosolewa na nchi
za Magharibi kuweka mbele maslahi yake ya kibiashara barani Afrika,
huku ikipuuza masuala mengine muhimu kama vile haki za binadamu na
utunzaji wa mazingira.
Aliitoa kauli hiyo mbele ya hadhara ya wanasheria na wanadiplomasia
katika mji mkuu wa Senegal, Dakar, ambako alianzia ziara yake barani
Afrika. Bi Clinton alisema kuna maeneo mengi barani Afrika ambako
demokrasia inakabiliwa na kitisho, na ambako haki za binadamu
hukanyagwa.
''Waafrika wengi bado wanaishi chini ya utawala wa madikteta ambao kwao
suala lenye kipaumbele ni kung'ang'ania madarakani kuliko kuinua
kiwango cha maisha ya watu wao''. Alisema Hillary Clinton.
Mwisho wa siku za unyonyaji
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton akikutana na kundi la wanawake Senegal
Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Marekani alisema nchi yake
inataka uhusiano na Afrika ambao unazinufaisha pande mbili, na si ule
wenye nia ya kuchukua raslimali za bara hilo.
''Siku za wageni kuja barani Afrika na kuchukua utajiri wa bara hilo, bila kuacha chochote nyuma, zimekwisha'' Aliongeza.
Bi Clinton alisema Marekani itazingatia utawala wa sheria na
demokrasia, kinyume na nchi nyingine ambazo zinayafumbia macho masuala
hayo katika kulinda maslahi yake.
Ushindani wa biashara
Mchambuzi Jackie Cilliers kutoka Taasisi ya Utafiti juu ya Masuala ya
Amani iliyopo nchini Afrika Kusini, anasema mtazamo huu mpya wa Marekani
kuhusu bara la Afrika, una malengo ya ushindani wa kibiashara.
''Hakuna shaka kwamba ushindani kati ya Marekani na China unaweka
ushawishi katika siasa za nje za Marekani. Na ushindani wa kibiashara
kati ya China na Marekani barani Afrika unashika kasi.
Alipokuwa ziarani
nchini Tanzania, Hillary Clinton alisema Afrika inakabiliwa na aina
mpya ya ukoloni, ambao unalenga kunyonya raslimali za bara hilo. Alisema
Cilliers na kuongeza kwamba hiyo haina tofauti na yale yaliyoyafanywa
nchi za magharibi barani Afrika siku za nyuma.'
Nchi za magharibi huishutumu China kupuuza haki za binadamu barani Afrika
Kauli ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani inakuja baada ya
rais wa China Hu Jintao kutangaza mkopo wa dola bilioni 20 kwa nchi za
Afrika, na kusema kuwa China ni rafiki wa Afrika ambaye anajali uhuru wa
nchi za bara hilo kujichagulia njia ya kufuata katika mchakato wa
kujiendeleza.
Katika ziara hii ya siku 11, Hillary Clinton atazitembelea pia Sudan
Kusini, Uganda, Kenya na Malawi. Nchi nyingine atakazozizuru ni Afrika
Kusini, na Ghana.
Mwandishi: Daniel Gakuba/dw.com
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :