Treni za abiria Dawa ya foleni kuanza kutoa huduma Dar es Salaam

Posted in
No comments
Thursday, August 2, 2012 By danielmjema.blogspot.com

Waziri wa usafiri Dkt. Harrison Mwakyembe
USAFIRI wa treni za abiria jijini Dar es Salaam, unatarajia kuanza Oktoba mwaka huu.

Treni hizo zitakuwa zikisafiri katika maeneo ya Ubungo Maziwa hadi Stesheni ya Dar es Salaam na kutoka Mwakanga hadi Kurasini kupitia Stesheni ya Dar es Salaam.

Pamoja na safari hizo, treni nyingine itakuwa katika Reli ya TAZARA ambayo itakuwa ikipita katika maeneo ya Kwa Fundi Umeme, Yombo, Kwa Limboa, Lumo, Kigilagila, Barabara ya Kitunda, Kipunguni B, Moshi Baa, Majohe, Shule ya Sekondari Magnus, Mwakanga, Chimwaga, Maputo, Mtoni Relini, Kwa Aziz Ali Relini hadi Kurasini.

Taarifa hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alipowasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2012/2013.

“Kwa njia ya reli kati ya Stesheni ya Dar es Salaam hadi Ubungo kiasi cha Shilingi bilioni 4.75 zitatumika kwa ajili ya ukarabati wa njia, ukarabati wa injini tatu za treni na mabehewa 14 ya abiria.

“Fedha hizo zimepatikana na kazi ya ukarabati wa njia ya reli injini na mabehewa imeanza na inatarajiwa kukamilika Oktoba, mwaka huu na safari hizo kuanza.

“RAHCO inaendelea kukarabati njia ya reli na mataruma mabovu zaidi ya 1,500 yameshabadilishwa na kazi ya kuweka sawa mataruma ili yakae pembe mraba imeshafanywa kwa umbali wa km 10.5.

“Pia, kazi ya kuimarisha tuta lililoharibika na kufukua mifereji ya kupitisha maji zinaendelea ingawa mradi huu unakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo wananchi kuvamia maeneo ya reli baada ya kutotumika kwa muda mrefu.

“Kwa hiyo, treni hizo zitakapoanza treni moja itaanzia Stesheni ya Dar es Salaam kuelekea Ubungo Maziwa na itakuwa inapishana na nyingine katika Kituo cha Buguruni kwa Mnyamani.

“Treni hizo zitasimama kwenye vituo sita ambavyo ni Stesheni ya Dar es Salaam, Kamata, Buguruni kwa Mnyamani, Tabata Matumbi, Mabibo na Ubungo Maziwa na kila treni itakuwa na mabehewa sita yenye uwezo wa kubeba abiria waliokaa na waliosimama takribani 1,000 kila safari,” alisema Dk. Mwakyembe.

Alisema safari kati ya Stesheni ya Dar es Salaam na Ubungo Maziwa itakuwa ikitumia dakika 35 na treni hizo zitasafirisha abiria wapatao 16,000 kwa siku.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka wafanyabiashara wawekeze katika mradi wa maegesho ya magari eneo la Ubungo kwa kuwa Chuo cha Usafirishaji cha Taifa kimetoa eneo la ekari nne kwa ajili hiyo.

“Eneo hili limetengwa kwa ajili ya maegesho ya magari ambayo yatakuwa yanaachwa na wenye nayo kutoka Kibaha, Kiluvya, Mbezi na Kimara baada ya kupanda treni kuelekea mjini,” alisema.

Kuhusu treni za TAZARA, alisema zinahitajika Sh milioni 838, kwa ajili ya ukarabati wa injini tatu za treni na mabehewa 14 na ukarabati wa injini na mabehewa unaendelea na unatarajia kukamilika Oktoba mwaka huu.

Wakati huohuo, Dk. Mwakyembe aliiagiza Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) kuhakikisha vyombo vya majini havisafiri bila abiria kuwa na mavazi ya kujiokolea.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .