IDDI JUMA: MWENYEKITI MPYA CCM KILIMANJARO ALIYEPANIA KUVUNJA MAKUNDI
Posted in
No comments
Wednesday, December 12, 2012
By
danielmjema.blogspot.com
Na Fadhili Athumani, Moshi
05, Desemba
CHAMA cha Mapinduzi kama tunavyofahamu katika siku za hivi
karibuni ilikuwa katika hekeheka za kufanya uchaguzi wa ndani katika ngazi za
mikoa na ule wa kitaifa uliofanyika katika mkutano mkuu jijini Dodoma na Rais
wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM kwa mara
nyingine tena kwa kishindo.
Katika chaguzi hizo mikoani imetumia fursa na haki yao
kikatiba kwa mujibu wa katiba ya chama tawala kuwachagua watu wanaofaa
kuwaongoza kwa ufanisi mkubwa na wenye uwezo wa kutekeleza sera na ilani ya
chama na mmoja wao ni Mwenyekiti Mpya wa chama cha Mapinduzi mkoa wa
Kilimajaro, Iddi Juma.
Kwa miaka mingi sasa mkoa wa Kilimanjaro umekuwa ukichukuliwa
kama moja ya ngome ya chama cha mapinduzi CCM sifa ambayo hata hivyo kwa miaka
ya hivi karibuni imeanza kutoweka huku majimbo mengine yakitwaliwa na vyama vya
upinzani.
Mzimu huu umekuwa ukikiandama chama tawala katika chaguzi za
hivi karibuni huku upinzani mkubwa ukitoka katika chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) ambayo kwa sasa ndiyo inayoongoza sehemu kubwa ya jimbo la
Moshi ikiwa ni pamoja na Baraza la Madiwani kwa maana ya Manispaa.
Kwa kutambua hilo chama cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Kilimanjaro,
kimeona haja ya kufanya mabadiliko na kufanya maamuzi ya kijasiri na kumchagua Mwenyekiti
mpya na kumpa nafasi Iddi Juma kuwaongoza katika juhudi za kuukomboa mkoa na
shubiri ya upinzani ambayo imeanza kikitishia CCM mkoani Kilimanjaro.
MTANZANIA ilifanya mahojiano na mwenyekiti huyo katika ofisi
zake zilizopo katika jingo la makao makuu ya chama cha Mapinduzi mkoa wa
Kilimanjaro, na hapa Iddi Juma pamoja na mambo mengine mengi anaweka wazi
mikakati yake katika kukiinua na kukiimarisha Chama tawala mkoani hapo.
Juma anainisha baadhi ya malengo yake na kusema moja ya kazi
atakazozifanya ni kusafisha chama hicho kongwe hapa nchini na katika
kuhakikisha hilo linafanyika, katika kikao cha pili cha Halmashauri kuu CCM mkoa
wa Kilimanjaro, Juma aliteua wajumbe watatu katika kamati ya Siasa, ambao ni
Amina Shamba, Dkt.Steven Moria na Zainah Heshima.
Mwenyekiti huyo anasema ili kuweza kufikia malengo ya kuimarisha
chama na kukomboa majimbo ambayo ndiyo kazi kubwa aliyoazimia kuifanya kabla ya
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ni lazima uwepo wa ushirikiano katika kila upande,
kupendana na uwepo wa uwazi lazima uzingatiwe.
Anasema Tatizo kubwa
la CCM mkaoni Kilimanjaro, upo kwa wanachama wenyewe na kuongeza kwamba katika
kipindi kirefu amekuwa akifuatilia mwenendo wa CCM mkoani Kiliamanjaro na
kubaini kinachijitokeza hivi sasa dhidi ya CCM, unatokana na wanachama wenyewe
ambao anasema baadhi yao ni mandumakuwili.
“Unajua kwa muda mrefu sana hata kabla ya kuchaguliwa kuwa
mwenyekiti katika uchaguzi uliomalizika wa Oktoba 18, nimekuwa nikikifuatilia CCM
na kubaini miongoni mwetukuna watu waliojisahau, kuna watu mandumakuwili, wenye
mapenzi ya kinafiki juu ya chama huku mioyo yao ikiendelea kuhusudu pesa na
uongozi.
“Kumekuwa na mjadala kuhusu makundi ndani ya chama, japo
watu wengi wamekuwa wakikana ukweli huu, nataka niweke wazi kwamba na ieleweke
kwamba miongoni mwetu kuna watu wachache wasio waaminifu na ndio hao hao
wanaozunguka kueneza dhana hii potofu ya kuwepo kwa makundi ndani ya Chama.
“CCM tuko shwari, tuko imara na ndio maana hata kwenye uchaguzi
wa hivi karibuni wa udiwani CCM ilifanikiwa kuibuka na madiwani 22 kati ya
nafasi 27 zilizokuwa zikiwaniwa, kinachotakiwa kufanyika ambacho mimi binafsi
nimekuwa nikipigania kila kukicha katika mkoa wetu ni kupembua pumba.
“Lengo letu ni kuona majobmo yote yaliyokuwa chini ya CCM
hapo awali yanarudi katika himaya yetu, nitapigana kwa nguvu zangu zote
kuhakikisha katika uchaguzi ujao wa 2015 tunashinda majimbo yote hasa jimbo la
Moshi mjini, Hai, Rombo na Vunjo,” anasema Juma.
Anasema kwa sasa kinachotakiwa kifahamike a kuheshimika na
wanachama wote, ni ukweli kwamba uchaguzi umepita, muhimu sasa ni kubaini kwa
ufasaha matatizo, vikwazo na changamoto na kuyatafutia ufumbuzi kwa lengo la
kwenda sanjari na kauli mbiu ya Mkutano mkuu wa Nane wa CCM “UMOJA NA USHINDI,
UMOJA NI USHINDI”.
Juma anasema ili kuona hayo yanafikiwa , wanachama na
viongozi wote ndani ya chama Tawala, wanatakiwa kwa nguvu zote kuyakataa
makundi hasi, kukemea na kupinga kwa nguvu zote, unafiki na undumila kuwila na
tabia ya kujengeana chuki ndani ya CCM hasa baada ya Uchaguzi.
“Kumekuwa na matukio ya watu kuingia katika misuguanio mara
baada ya kumalizika kwa uchaguzi, kujengeana chuki, sidhani kama tunahitaji
kuchukiana, kinachotakiwa ni kuwa kitu kimoja, pale inapobidi pafanyike vikao
vya upatanishi na masikizano kwa waliochaguliwa na wasiochaguliwa.
Watanzania tujifunze na kuhimizana kuponya majeraha na
kuziba nyufa zilizosababishwa na chaguzi za ndani ya chama, ya kitaifa na yale
ya kimataifa, mataifa mengine yameweza, Marekani wameza kwa nini sisi
tushindwe?” anasema Juma
Akizungumzia swala la kikao Mwenyekiti huyo anakumbushia na
kunukuuu kauli ya Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama aliyoitoa hivi
karibuni katika kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC), kwamba watamishi na
baadhi ya viongozi katika ofisi za umma wanafanya kazi kwa mazoea.
Juma anasema tatizo hilo haliko katika maeneo ya utendaji na
utumishi tu, bali hata kwenye siasa na hasa Chama tawala, anasema kumekuwa na
tatizo la viongozi wengi kutofanya vikao na hata wanapofanya vikao hivyo, vinafanyika
kinyemela na mara nyingi hata ajenda zinazojadiliwa hazina mashiko na jamii
wala Chama.
“Moja ya mdudu unaotafuna chama chetu ni utabia ya baadhi ya
viongozi kugeuza Maofisi, mikutano ya hadhara na Vikao vya Vyama kuwa vijiwe
vya umbea na Majung, nadhani ifike muda sasa Viongozi tutambue dhima iliyoko
mbele na tutimie vikao kujadili yenye mashiko na jamii na chama.
“Nitafarijika kuona viongozi wa Chama cha CCM, mkao wa
Kiliamanjaro watatumia muda mwingi kuhimiza ufuatiliaji kwa ukaribu wa
ufanyikaji wa vikao vyote vya chama kwa mujibu wa katiba na kuheshimu maadili
na miiko ya chama aliyoiweka Baba wa Taifa, Julius Kambarage Nyerere.
Mwenyekiti huyo hata hivyo anasema kuwa, kwa miaka takribani
18 ambayo nchii imekuwa katika mfumo wa Vyama vingi vya Siasa, kuna vyama
vingine ambavyo vimekuwa ni kama debe tupu ambalo haliachi kupiga kelele,
akitolea mfano Chama cha Chadema.
Anasema sio CHADEMA, TLP, CUF, NCCR-MAGEUZI ambao wana ubavu
wa kumbana na CCM kwa sasa, na wanaojidanganya wajue hawatafanikiwa labda baada
ya miaka 2000 ijayo tena labda endapo watabadili sera zao mbovu.
Anasema chini ya uenyekiti wake, CCM Kilimanjaro, imejipanga
kujibu propaganda zinazotolewa na mahasimu wa CCM, viongozi wake na wanachama
na kusisitiza kwamba kazi hiyo itafanyika kwa ufasaha, kwa wakati na kwa
usahihi tena katika maeneo stahili.
Akiendelea kuanisha baadhi ya kazi muhimu na maeneo ambayo
uongozi wake unadhamiria kufanyia kazi mwenyekiti huyo anasema, kwa saas kazi
kubwa ni kuhakikisha CCM, kinajiendesha chenyewe na amejipanga kuendeleza
miradi na vyanzo vya mapato vilivyopo na vitakavyoibuliwa kwa kutumia wataalamu
wa fani husika.
Pia, anazungumzia swala la kuthamini nguvu na uwezo wa
wanachama, hasa viongozi na kusisitiza katika uongozi wake hakutakuwa na
taratibu wa kuchaguana kwa kutazama sura, kabila wala ukoo.
“Tumejipanga kujiimarisha kwa kuteua na kuchagua watu
madhubuti, sahihi, lengo letu likiwa ni kuunda safu madhubuti ya uongozi na katika
utaratibu huo hata wanachama tutahakikisha wanakuwa watu sahihi na sio kuwa na
idadi kubwa ya watu wasiokuwa na mapenzi na chama.
Mwenyekiti huyo wa CCM mkoa wa
Kilimanjaro, alizaliwa mwaka 1954 na kuchukua stashahada ya juu katika kazi ya
Jamii-NSWTI (1982- 1985), utawala, menejimenti,sheria za kazi mwasiiano na
Menejimenti-London 2004 pamoja na mafunzo ya nje ya nchi- Mauritius 2002.
WASIFU WAKE
Alifanya
kazi katika kiwanda cha Sukari TPC kama meneja Rasilimali kabla ya kustaafu kwa
hiari 2009akiwa katika nafasi ya kiongozi mwandamizi.
Mwenyekiti
huyo amewahi kupata nafasi ya kiongozi ndani ya CCM, ambapo mwaka 1986-1989
alifanikiwa kuwa mjumbe wa kamati ya siasa Tawi la CCM kiwandani, mjumbe wa
kamati ya siasa tawi la langasani, Arusha chini, mwaka 2001-2005, Mwenyekiti wa
CCM kata ya Majengo, manispaa ya Moshi mwaka 2012, Oktoba 18 2012 akachaguliwa
kuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM
Taifa, Mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM mkoa wa Kilimanjaro na Mjumbe wa
mkutano mkuu CCM mkoa wa Kilimanjaro.
0756038214/0654724337
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :