MAANDALIZI YA HARAMBEE YA CHUO CHA MWEKA; PINDA KUCHANGISHA ZAIDI YA BILIONI 6 LEO JIONI

Posted in
No comments
Friday, November 1, 2013 By danielmjema.blogspot.com

Na Mwandishi Wetu, Moshi

Waziri mkuu mstaafu aliyejiuzulu,Edward Lowasa na Mwenyekiti mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk.Regnald Mengi ni miongoni mwa watu mashuhuri walioalikwa jioni hii katika hafla ya uchangiaji wa maendeleo ya Chuo cha Uhifadhi na Usimamizi wa Wanyamapori,Mweka.

Zaidi  ya dola za kimarekani 3.6 bilioni sawa na sh. bilioni sita za Tanzania,zinahitajika kwa ajili ya upanuzi wa chuo hicho, kilichojengwa miaka 50 iliyopita.Katika harambee hiyo pia serikali imewaita wabunge wote wa majimbo ya mikoa ya Kilimanjaro,Arusha,Manyara na Tanga kushiriki uchangiaji huo.

Kaimu Mkuu wa Chuo hicho,Dk.Freddy Manonge, ameiambia Taifa Letu.com, Waziri Mkuu Mizengo Pinda ndiye anayetarajiwa kushuhudia uchangiaji wa chuo hicho ambacho kimepanga kupanua miundo mbinu yake kwa ajili ya kuanza kutoa mafunzo ya namna ya kukabiliana na ujangili katika hifadhi za taifa na maeneo tengefu yanayotishiwa na vita ya ujangili wa tembo na faru.

Juzi,wataalamu wa usimamizi na uhifadhi wa wanyamapori kutoka nchi za Scandinavia,Bara la Ulaya,Amerika na Afrika, walikutana mkoani Kilimanjaro kujadili matumizi ya teknolojia mpya, iitwayo Forensic Science Laboratory ambayo itatumiwa kuondoa utata wa kuwabaini majangili wanaoendesha vitendo vya uharamia vya kuteketeza tembo na faru kupitia taarifa za vinasaba.

Amesema kuwa chuo hicho kipo kwenye mkakati wa kupanua huduma zake katika ukanda wa Afrika ili kuweza kuchukua wanafunzi kati ya 800 hadi 1000 kwa mwaka wa masomo ikiwa ni pamoja na kukiwezesha kumudu gharama za manunuzi ya magari na vifaa vya kisasa vitakavyowawezesha wataalamu na wanafunzi wanaohitimu mafunzo hayo kukabiliana na mbinu chafu za watu wanaoendesha matukio ya ujangili.

Mbali ya ujenzi wa madarasa,miundo mbinu na ununuzi wa magari maalumu ya chuo hicho kikonge barani Afrika,serikali inatarajia kugharamia uingizwaji wa teknolojia hiyo ya Forensic Science Laboratory katika mitaala ya vyuo vyake vya uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori na utalii.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .