HOTUBA YA MHE. LEONIDAS T. GAMA, MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO WA TATU WA WADAU WA HABARI KILIMANJARO TAREHE 13 MEI, 2013
Posted in
No comments
Monday, May 13, 2013
By
danielmjema.blogspot.com
AWALI ya yote, nimefarijika kupewa nafasi hii muhimu ya kufungua Kongamano hili la Tatu
la Wanahabari na wadau wa Habari Mkoani Kilimanjaro
Ni matumaini yangu kwamba Kongamano
hili limekutanisha waandishi wa habari na wadau mbalimbali kutoka hapa Mkoani
na kila mmoja kwa nafasi yake ni kama sehemu ya familia moja katika kusukuma mbele
gurudumu la maendeleo ya Mkoa wetu.
Ndugu
Mwenyekiti,
Ili kufikia lengo la
kuinufaisha jamii ya Wanakilimanjaro na
Taifa kutokana na huduma mbalimbali
zitolewazo na taasisi tofauti, ushirikiano wa pamoja kati ya Serikali,
Wafanyabiashara wa bidhaa na huduma, wananchi pamoja na vyombo vya habari ni
jambo la msingi.
Ndugu
Mwenyekiti,
Napenda
kutumia fursa hii kutoa pongezi kwa wanachama wote wa MECKI chini uongozi wa mwenyekiti wa MECKI Rodrick Makundi na kamati
nzima ya utendaji kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa Klabu yenu inasonga
mbele na kutekeleza majukumu yake kwa kufuata utaratibu mliojiwekea.
Kama mlivyoelezea malengo ya
kongamano hili, naamini kongamano hili litafungua ukurasa mpya wa mahusiano yaliyoboreshwa
baina ya wanahabari na wadau wengine kwa ujumla wake kwani kwa kipindi kifupi
nilichokuwepo mkoani hapa nimeshuhudia mchango mkubwa wa vyombo vya habari
katika kuisadia serikali kutekeleza vyema wajibu wake lakini pia kukosoa pale
ilipokuwa inaonekana inafaa. Kukosoa na siyo kulaumu au kulalamika.
Ndugu
Mwenyekiti ,
Kutafuta
na kutoa habari katika nchi yetu ni haki ya kikatiba kama ilivyobainishwa na
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika Ibara ya 18(b)
inayompa uhuru Mtanzania kufanya shughuli zake katika tasnia ya habari.
Katiba
yetu kupitia Ibara hiyo inatamka wazi kuwa kila mtu anayo haki kutafuta,kupokea
na kutoa habari bila kujali mipaka ya nchi.
Napenda
niwahakikishie wanahabari wa mkoa wa Kilimanjaro kuwa serikali ya mkoa wa
Kilimanjaro inatambua kuwa kazi zinazofanywa na wanahabari ni kazi halali kwa
mujibu wa Katiba na Sheria za nchi yetu. Fanyeni kazi kwa kuzingatia weledi na maadili
ya nchi yetu.
Hivyo
napenda niwatie moyo kuwa mfanye kazi kwa bidii, kujiamini na uhuru kama
wananchi wengine wanavyofanya shughuli halali katika mkoa wetu.
Ndugu
Mwenyekiti,
Katika
nchi yetu kuna tatizo la watu kutumia vibaya nafasi walizonazo ambazo ni kwa
ajili ya kuutumika umma badala yake wanazitumia nafasi hizo kwa maslahi yao wenyewe
au kutumikia makundi ya wachache katika jamii. Napenda nieleweke kuwa tatizo
hili limeshaanza kuingia katika tasnia muhimu ya habari jambo ambali kwa maoni
yangu naona ni hatari kwa uchumi na amani ya nchi yetu.
Tasnia
ya habari ina mchango mkubwa katika kustawisha maendeleo ya nchi katika nyanja
zote muhimu kama itatumika vizuri kwa waandishi wa habari kusimama katika
nafasi yao ya kuutumikia umma wa watanzania.
Lakini
ikiwa kinyume chake tasnia ya habari itatumika kueneza uongo, fitina, chuki na
uhasama kwa wananchi jambo ambalo madhara
yake kwa wananchi ni kukosa nafasi ya kufikiria namna ya kufanya kazi kwa bidii
ili kupambana na umasikini, badala yake watabaki kunyosha vidole kwa kila mmoja
kumuona mwenzie ni adui na si ndugu tena huku taifa likirudi nyuma baadala ya
kusonga mbele.
Madhara
makubwa ya ukiukwaji wa sheria na maadili katika uandishi wa habari ni kuingiza
nchi katika machafuto, jambo ambalo litatugharimu kurudi nyuma katika maendeleo
tuliyofikia, mipango tuliyojiwekea, rasilimali zetu na maisha yetu. Napenda niwatahadharishe kuwa wapo watu wasio
penda mafanikio ambayo tumefikia. Na
wanaweza kuwatumia ninyi wanahabari kupotosha umma na hatimaye nchi yetu
ikaingia kwenye machafuko. Sote ni
mashahidi na tumejionea jinsi vyombo kama hivi vilivyoweza kutumika katika nchi
kama Rwanda na Burundi katika kuchochea fitina, chuki, mifarakano mikongoni mwa
wananchi na hatimaye kusababisha machafuko yaliyogharimu upotevu wa mali na
maisha ya watu.
Ni vyema wanahabari
mkazingatia maadili ya taaluma yenu kwa kuhakikisha mnaandika habari za kweli
na zilizofanyiwa utafiti wa kina, kwani kalamu ni sehemu ya silaha katika
uwanja wa vita.
Ndugu
Mwenyekiti,
Nchi
yetu ni ya kidemokrasia, na kila kwenye demokrasia ya kweli haki za msingi za binadamu
zinazingatiwa na hakuna uhuru usio na mipaka. Napenda niwakumbushe wanahabari
kuwa uhuru wa mtu unaishia pale unapoanzia uhuru wa mtu mwingine.
Uhuru
wa habari unaelezwa wazi katika Ibara ya 18 (a) ya katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Ni kujua kuwa
Katiba hii imeweka mipaka ya uhuru huo katika Ibara ya 16(1) inayompa mtu uhuru
wa kuhifadhiwa nafsi yake, maisha yake pamoja na kuheshimiwa.
Ni
matarajio yangu kuwa wanahabari wa Mkoa wa Kilimanjaro hamtaniangusha kwa
kuandika habari bila ya kuzingatia sheria, haki za binadam na maslahi ya Mkoa
na Taifa.
Ndugu
Mwenyekiti,
Tunaelekea
katika kuandika katiba mpya ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, huu ni wakati
wenu kuwaelimisha wananchi mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa na kuacha
kushabikia masuala yanayoweza kupotosha mchakato mzima. Wengi duniani hawajaweza kupata Katiba katika
hali ya utulivi na amani. Nawapongeza wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Msikubali kwa namna yoyote
kuvuruga misingi imara iliyowekwa na waasisi wa Taifa hili, wakiongozwa na
Hayati baba wa Taifa Mwl Julius Nyerere ambaye kwa kipindi cha uhai wake wote alihubiri na kuamini katika umoja na
mshikamano miongoni mwa watanzania.
Aidha waandishi wa habari si
vyema kujiingiza katika misuguano isiyokuwa na misingi na baadhi ya taasisi
bali ni nyema kila mmoja kwa nafasi yake akatimiza wajibu wake badala ya
kuviziana kwa baadhi ya mambo.
Ndugu
Mwenyekiti,
Pamoja
na waandisi wa habari lakini pia ni wajibu wa wadau kuhakikisha kuwa wanatoa
ushirikiano kwa wanahabari, kwa kuacha kuficha taarifa ambazo zinapaswa kuwafikia
wananchi, kwani jambo hili limekuwa likileta msuguano baina ya wadau na
wanahabari na kufikia hatua ya kuhatarisha mahusiano baina ya pande hizi
mbili.
Mara kadhaa tumemsikia Rais
Jakaya Kikwete akisisitiza taasisi na ofisi za Umma kutoa habari kwa waandishi
ili nao waweze kuihabarisha jamii kulingana na jambo husika
Ndugu
Mwenyekiti,
Nitoe
wito kwa wadau wote wa habari mkoani Kilimanjaro,
itumieni ipasavyo Klabu hii ya waandishi wa habari (MECKI) katika masuala yenu
yanayohusu kuuhabarisha umma mambo mbalimbali, Watumieni waandishi wa habari
kuuhabarisha umma, shirikianeni na wekeni wazi habari kwa maslahi ya umma
kutegemeana na taraibu na sheria za uandishi wa habari.
Fanyeni
kazi kwa karibu na Halmashauri zetu zote katika mkoa wetu kuripoti habari za
maendeleo ya wananchi hasa wa vijini. Katika eneo ambalo serikali inatenga
fedha nyingi za maendeleo ni halmashauri, hivyo basi habari zinazogusa
maendeleo ya wananchi zipo katika halmashauri zetu.
Moja
kati ya matatatizo yaliyomo katika jamii ni watu kutojua kinachoendelea hasa
juhudi zinazofanywa na serikali na taasisi zingine katika kuwawezesha wananchi
kujiletea maendeleo. Kama kuna kiongozi au mtumishi asiyetoa ushirikiano kwa
waandishi mniambie.
Ndugu
Mwenyekiti,
Napongeza
mpango wenu wa maendeleo uliopita na huu mliuiweka wa sasa. Wekeni mipango
madhubuti ya maendeleo na utekelezaji wake.
Sitarajii
kusikia suala la Sacoss likiwasilishwa kama mpango tutakapokutana katika
kongamano lijalo. Nataka kusikia kutoka kwenu juu ya maendeleo ya Sacoss yenu.
Mkiwa na uchumi imara mnaweza kufanya shughuli zenu kwa amani na kujiamini
kutokana na nguvu za kiuchumi zitakazotokana na SACOSS yenu.
Tumieni
kongamano hili kuelezana na kupanga utaratibu mzuri wa kufanya kazi na chombo
hiki, na waandishi wa habari kwa ujumla, ili taarifa zote za maendeleo ziwafikie wananchi
kwa maslahi ya umma.
Mwisho,
kubwa zaidi ni ninyi kama wadau kuwaona wanahabari kama sehemu ya jamii badala
ya kuwaona ni maadui na wenye lengo la kuharibu sifa za taasisi zenu au kampuni.
Vyombo
vya habari vinaweza kujenga kama mtavitumia vizuri lakini pia vinaweza kubomoa
kama hamtaonyesha ushirikiano.
Baada
ya kusema hayo natangaza rasmi kuwa Kongamano hili la Tatu la Wanahabari kuhusu
Maendeleo ya Mkoa wa Kilimanjaro limefunguliwa rasmi.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :