KWA STAILI YA SOKA LA DAVID MOYES FELLAINI LAZIMA ATUE OLD TRAFFORD
Posted in
No comments
Wednesday, May 15, 2013
By
danielmjema.blogspot.com
LIVERPOOL, England
NA mambo ndio yameanza. Ni wiki sita na nusu zimebaki kumwona David Moyes rasmi akichukua mikoba ya Sir Alex Ferguson katika klabu ya Manchester United, lakini vyombo vya habari vimeshaanza kupamba aina ya kikosi kipya cha Mskochi huyo wakati atakapotua Old Trafford.
Nani atakuja? Nani ataondoka? Jinsi gani watajipanga? Nani atakuwa kwenye benchi la ufundi? Sir Alex atakuwa anasaidia?
Tayari kocha huyo ameshapangiwa usajili mkubwa atakaofanya. Usajili wa nyota wawili kwa pamoja, kutoka klabu yake ya zamani ya Everton, Leighton Baines na Marouane Fellaini.
Baines na Fellaini ni wachezaji wawili waliobora kabisa kwenye Ligi Kuu England na wamekuwa mahiri kwa nafasi zao wanazocheza ndani ya uwanja.
Gazeti lisilopitwa na mambo la The Sun tayari lilishatoa ripoti kwamba kiasi cha pauni milioni 39 kimetengwa kwa ajili ya kuwang'oa wakali hao kutoka Goodison Park na kuwafanya watue Old Trafford.
Inaaminika kwamba, Everton hawatakuwa kwenye presha kubwa kwa kuuza silaha zao hizo mbili. Wanaamini kwamba kwa kukusanya fedha za mauzo ya nyota hao na kuongezea pauni milioni 20 za haki za televisheni, wanaamini hawatakuwa na presha katika kumtuliza kocha wao mpya kwa kufanya usajili wa wabadala wa wachezaji hao.
Lakini, kumekuwa na imani kwamba, Everton hawatakuwa na nguvu ya kumzuia Moyes asiwasajili wachezaji hao. Moyes anaonekana wazi kwamba yupo na mpango wa kupeleka ofa ya kuwasajili nyota hao kutoka kwenye klabu yake ya zamani.
Na hata kama Moyes amekubaliana na mabosi wake wa zamani wa Everton kwamba hataruhusiwa kuchukua wachezaji Goodison Park, makubaliano kama hayo yanaweza yasiheshimiwe pia.
Tazama kitu alichokifanya Brendan Rodgers, alikubaliana na Swansea City kwamba asichukue mchezaji yeyote kutoka kwenye klabu yake hiyo ya zamani kwa kipindi cha miezi 12, lakini hakutaka kupoteza muda na kumvuta kiungo Joe Allen kwenye kikosi chake.
Lakini, je, Baines na Fellaini watakubali uhamisho huu? Hebu tuanzie na Baines. Beki huyo wa kushoto tangu alipohamia Everton akitokea Wigan mwaka 2007, amekuwa mchezaji muhimu pia kwa kikosi cha timu ya taifa ya England pindi Ashley Cole asipokuwapo na ameweza kuwamo kwenye Kikosi cha Ligi Kuu England cha wachezaji wa kulipwa kwa misimu miwili.
Baines, 28, kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa na mpango wa kujiunga na Manchester United na hakika atapokelewa kwa mikono miwili kwenye timu ya Moyes.
Lakini, kumekuwa na ripoti kutoka chanzo kingine kwamba Everton hawatakuwa tayari kulifanya hilo litokee japo litakuwa jambo gumu kwao kuzuia uhamisho huo usiweze kutokea kama Moyes ataamua kuufanya.
Kitu kingine ambacho kinaweza kuzuia uhamisho wa Baines kutokea ni kuwapo kwa Patrice Evra. Sawa, Evra anaelekea 'kuzeeka' na kwa muda mrefu Alex Ferguson amekuwa kwenye mchakato wa kumsaka mbadala wake mapema, ambapo alianza na usajili wa Alexander Buttner.
Mfaransa Evra amekuwa akicheza bila kutetereka kiwango chake kwa muda mrefu aliokuwa chini ya Ferguson na kwamba ni nahodha msaidizi, hivyo si kitu rahisi kumwona beki huyo akawekwa kwenye benchi kumpisha Baines.
Hivyo, kama Baines atatua mahali hapo jambo hilo litampa wakati mgumu Moyes wa kuchagua ni mchezaji gani aanze, hasa ukizingatia Evra ana uwezo na Baines ni mchezaji ambaye amekuwa akimtegemea wakati alipokuwa katika kikosi chake cha Everton.
Uhamisho wa Fellaini kuungana na Moyes kwenye kikosi cha Man United ni kitu kisichopingika. Viungo wachache sana kwenye Ligi Kuu England ambao wameonekana kuwa hatari kuliko Mbelgiji huyo, ambaye umahiri wake umemfanya watu waamini kwamba ni mchezaji asiyefunikika.
Fellaini amewekewa kipengele cha pauni milioni 22 kwenye mkataba wake kwamba kama kutakuwa na timu itakayoweza kulipa kiasi hicho, basi itakuwa imefanikiwa kumnasa nyota huyo.
Mkataba wake katika klabu hiyo ya Everton, unamfanya aendelee kuvaa jezi za timu hiyo hadi 2015-16, lakini mambo yanaweza kuwa tofauti kama kutakuwa na timu yenye hadhi ya kucheza Ligi ya Mabingwa barani Ulaya ikaja na ofa ya kutaka kumsajili.
Kwa kuzingatia fedha kiasi cha pauni milioni 120, ambazo alitengewa Ferguson kwa ajili ya usajili wa msimu ujao, jambo hilo linaweza kuondoa ugumu wote wa Moyes na United kuweza kuipata saini ya Fellaini.
Mfumo wa kiuchezaji ambao Moyes amekuwa akiupa nafasi ni kuweka safu ngumu ya ulinzi na kutumia mipira ya juu kwenye safu ya ushambuliaji.
Ni wazi kabisa mfumo huo umekuwa ukiendana na staili ya uchezaji wa kiungo Fellaini, ambapo atakuwa na faida kubwa kwa United kama itamsajili na kumpanga sambamba na Carrick na Cleverly kwenye sehemu hiyo ya katikati ya uwanja.
Moyes, 50, amekuwa na kawaida ya kuwabadilisha washambuliaji na kuwafanya kuwa mawinga (mtazame Nikica Jelavic). Kama atamtumia Wayne Rooney (akiwa amebaki hapo) na Danny Welbeck kwenye wingi, jambo hilo litawapa nafasi kubwa zaidi Fellaini na Van Persie kutawala sehemu ya katikati.
Lakini, kuwasili kwa Fellaini kunaweza kuwa habari mbaya kwa Shinji Kagawa, ambaye amekuwa mchezaji dhaifu kwa mipira ya juu na hata ya chini kutokana na kuwa na nguvu ndoto, licha ya kuwa na ufundi mkubwa wa kuuchezea mpira na kuwahadaa wapinzani.
Wakati suala la usajili wa nyota wote wawili kutoka Everton ukiwa unawezekana, kama mambo yakiwa tofauti basi kuna kila dalili kwamba, mmoja wa wachezaji hao mmoja atafuatana na kocha wake.
Moyes bila shaka atakuwa amewakosea heshima kubwa waajiri wake aliodumu nao kwa miaka 11 kwa kutaka kuwasajili nyota hao wawili, wakati ni wazi kabisa Everton haitakuwa na ulazima wa kuuza silaha zao hizo muhimu.
Kwa kikosi cha sasa cha Everton, mtu pekee ambaye anaweza kuungana na Moyes Old Trafford ni Phil Neville. Nahodha huyo, naye amehitimisha miaka yake ya kuitumia klabu hiyo ya Goodison Park, amekuwa na ndoto za kutaka kuingia kwenye menejimenti.
Moyes alimpa ofa ya kazi ya ukocha wiki chache zilizopita na iliaminika kwamba kazi hiyo mpya angeweza kuendelea kuifanya katika klabu ya Everton.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :