MACHAVA YAITUNGUA MPWAMPWA 2-0 RCL

Posted in
No comments
Monday, May 27, 2013 By danielmjema.blogspot.com

Na Mwandishi wetu, Kilimanjaro
MACHAVA FC ya Kilimanjaro, maarufu kama "mnyama mkali"  imeutumia vyema uwanja wake wa nyumbani wa Ushirika na kuibanjua Mpwapwa Stars 2-0 katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya Ligi ya mabingwa (RCL) uliosukumizwa juzi, jumapili.

Mpwapwa ambao ni mabingwa wa Dodoma, ukiwa ndio mchezo wao wa kwanza baada ya kutinga katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa moja kwa moja, walianza mchezo huo kwa kasi wakilisakama lango la Machava kila mara lakini mashambulizi yao yote katika dakika ya 7 na 13 yalishindwa kuzaa matunda baada ya mashuti ya Kamugisha funugulu na Omary Mselem yakiokolewa na mlinda mlango wa Machava.


Machava walicharuka katika Dakika ya 18 kipindi cha kwanza, wakitumia sehemu ya kiungo kusukuma mashambulizi walifanikiwa kupata bao la kuongoza kupitia kwa muuaji wao yule yule, Reality Lusajo, aliyewapiga chenga  mabeki wawili wa Mpwapwa kabla ya  kutingisha nyavu.


Zikiwa zimesalia takribani dakika tatu timu ziende mapumziko, Lusajo alirejea tena kufanya maangamizi katika lango la timu pinzani na kulipatia timu yake goli la pili na la ushindi katika dakika ya 42 baada ya beki wa Mpwapwa Frank Dimo kuchelewa kuondosha mpira uliokuwa unazagazagaa katika eneo la hatari.


Hilo ni bao la saba kwa Lusajo anayeongoza kwa kufumania nyavu tangu mzunguko wa kwanza wa ligi kuanza ambapo katika mechi mbili zilizopita alifunga mabao matano. Kwenye ligi ya mkoa wa Kilimanjaro pia aliibuka mfungaji bora ambapo katika mechi saba alifunga mabao 8.


Kwa ushindi huo Machava iliyoanza raundi ya kwanza kwa kuiondosha Flamingo ya Arusha kwa jumla ya mabao 6-2, imejiweka katika mazingira mazuri itakapokwenda Dodoma kucheza mchezo wa pili na Mpwapwa stars unaotarajiwa kupigwa Juni 1 ama 2 mwaka huu.


Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama ambaye alikuwa mgeni rasmi akiongozana na Mkuu wa wilaya ya Moshi, Dk. Ibrahim Msengi amewapongeza vijana wake na kuahidi kuendelea kuwaunga mkono

kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi.

Kwa upande wao, chama cha soka mkoa wa Kilimanjaro (KRFA), kupitia kwa afisa habari wake, Yusuph Mazimu kimesema timu hiyo itaendelea kukaa kambini kujiandaa na mchezo wa marejeano dhidi ya Mpwapwa na kuwataka wadau wa soka mkoani humo kuendelea kuiunga mkono.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .