UNDANI KIFO CHA ROBERT OUKO (February 15, 1990.)

No comments
Saturday, April 9, 2016 By danielmjema.blogspot.com

Na Joseph Mihangwa, Toleo la 139
WAKATI wananchi wa Kenya sasa wakikarobia uchaguzi mkuu wa mwaka 2017, kuna baadhi ya mambo ambayo bado yanasubiri kupata majibu.hayo tuyaache kwa sasa, baada ya kukuletea mfululizo wa makala ya kifo cha utata wa mwanamapinduzi na Rais wa zamani wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, Leo SAUTI KUU, inakuletea tafakuri kuhusu kifo cha Robert Ouko, kama ilivyoandikwa na Joseph Mihangwa.
 
Suala la la kifo cha mwanasiasa wa zamani mashuhuri nchini humo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Robert Ouko, kilichotokea Februari 13, 1990, limeanza kuibuka kwa pendekezo kwamba iundwe tume kuchunguza kifo hicho.

Dokta Ouko alikutwa amekufa katika mazingira ya kutatanisha karibu na nyumbani kwake Wilayani Kisumu, na mwili wake kuunguzwa vibaya kwa moto kiasi kwamba iliwachukua wataalamu wiki nzima kuyaunganisha mabaki yaliyoungua. Ingawa Serikali ya Kenya, chini ya Rais Daniel Arap Moi wakati huo, ilileta Tume ya Uchunguzi kutoka Uingereza kubaini sababu za kifo hicho, tume hiyo ilivunjwa ghafla na Moi kabla ya kukamilisha shughuli zake.

Mauaji ya viongozi wa kisiasa; hususan mawaziri na wanaharakati, si utamaduni mgeni nchini Kenya tangu enzi za uhuru hadi sasa ambapo waathirika wa kwanza kama vile mwanasiasa za mrengo wa Ki-Karl Marx, Gama Pinto, Waziri wa Uchumi na Mipango, Tom Mboya. na Mbunge wa Nyandarua, Josiah Mwangi Kariuki, kwa kutaja wachache tu, waliuawa katika mazingira ya kutatanisha. 

Agosti, 1990, Askofu Alexander Muge aliyejipambanua na vita dhidi ya ufisadi na udikteta nchini Kenya, naye alikufa katika ajali ya kupangwa ambapo mwanasiasa mkongwe, Mzee Masinde Muliro, alikufa ghafla katika mazingira ya kutatanisha. Kuna dhana tatu zinazohusishwa na kifo cha Dakta Ouko, lakini zote zenye kukanganya. Moja ni ile inayodai kwamba alijiua kutokana na matatizo binafsi yasiyofahamika; wakati dhana ya pili inaeleza kwamba, aliuawa na mdogo wake, Barack Easton Mbajah kutokana na ugomvi wa muda mrefu wa Kifamilia. Barack alikamatwa na kuteswa sana na Serikali ya Moi akituhumiwa kwa mauaji hayo. 

Dhana ya tatu inainyoshea kidole Serikali ya Rais Moi kwamba ilihusika moja kwa moja na kifo cha mwanasiasa huyo mashuhuri; ambapo kitendo cha Rais Moi cha kukatisha ghafla uchunguzi wa kikosi cha Polisi wa “Scotland Yard” kutoka Uingereza kilionyesha hofu aliyokuwa nayo endapo ukweli ungejulikana.

Je, ni kweli Dakta Ouko alijiua au aliuawa kama ilivyodaiwa? Na kama aliuawa, nani alimuua kama Barack Mbajah aliachiwa huru? Kwa nini Serikali imeficha ukweli juu ya kifo hiki? Kwa hili, tunapata somo gani kuhusu demokrasia, siasa na tabia ya watawala wa Kiafrika? Katika makala hii yenye sehemu mbili, nitajaribu kujibu maswali haya; na kwa kutumia vyanzo mbali mbali vya kisiasa, kiuchunguzi na vya kijasusi, tutaonyesha mipango ya muda mrefu ya “kumwondoa” Dakta Ouko, na jinsi Serikali ya Kenya ilivyohusika na kifo chake. 

Makala haya yatawasaidia pia Wakenya wema wanaotaka kujua jinsi mwana mpendwa huyo wa Afrika alivyouawa kikatili na wanasiasa walafi. Kengele ya kifo ilianza kumwita Dakta Robert Ouko kwa mara ya kwanza alipokwaruzana na kigogo mwenzake na mfanyabiashara kipenzi cha Moi, Katibu Mkuu katika Ofisi ya Rais, Bwana Hezekiah Oyugi ambaye pia alikuwa Mkuu wa Usalama wa Ndani na Tawala za Mikoa; baada ya Ouko kukamilisha (kwa juhudi binafsi) taarifa yenye kuibua hali ya rushwa na ufisadi wa kutisha nchini Kenya, mithili ya ile ya Jaji Warioba hapa kwetu.

Kufuatia mgongano huo, Oktoba 1983, Dakta Ouko alibadilishwa wizara, kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kwenda Wizara ya Kazi kwa ushauri wa Oyugi kwa Rais Moi. Wakati huo huo, Moi na Oyugi walizidisha harakati zao, sio tu kufifisha sifa na umaarufu wa kimataifa wa Ouko; bali pia kuhakikisha kwamba anapoteza kiti chake cha Ubunge cha Jimbo la Kisumu Vijijini kwa njia ya kupandikiziwa upinzani kwa gharama yoyote.

Mtindo wa wanasiasa makini na wanaharakati dhidi ya maovu katika jamii kupandikiziwa wapinzani kwa gharama yoyote ili waangushwe, ni wa viongozi wengi dhaifu na wasiojiamini barani Afrika; na sasa unatunyemelea hapa kwetu Tanzania dhidi ya wanaharakati waliojipambanua na vita dhidi ya ufisadi nchini.

Ouko aomba msaada wa Margareth Thatcher Akiwa pia rafiki kipenzi cha familia ya Bwana na Bibi (Margareth) Thatcher, mama Thatcher, akiwa Waziri Mkuu wa Uingereza wakati huo, Ouko alibaini haraka kwamba pona yake dhidi ya hila za Moi na makuwadi wake ilikuwa mikononi mwa mama huyo wa shoka ambaye hakuficha chuki yake dhidi ya uongozi wa Moi uliokithiri kwa rushwa na ukiukaji wa haki za binadamu.

Kwa hiyo, kampeni za uchaguzi zilipoanza, zikionyesha dalili zote za hila na mizengwe, Dakta Ouko alifunga safari kwenda Uingereza kuonana na Mama Thatcher kumuomba amtake Moi aache kumtilia vitimbwi; na pia amrejeshe kwenye Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, wizara aliyoimudu vizuri na kumjengea jina na heshima kimataifa. 

Ouko, akiwa mgeni wa familia ya Thatcher katika nyumba yao ya shamba (country house), aliweza kumshawishi mama huyo kama alivyotarajia. Mama huyo, kwa kuchukizwa na tabia ya Rais Moi, akachukua hatua kubwa zaidi ya aliyotarajia Ouko ya kutaka kumwondoa madarakani Moi mwenyewe ambaye, hata hivyo, wakati huo alikuwa dhaifu akisumbuliwa na ugonjwa wa lukemia na kansa ya koo.

Ikumbukwe kwamba, Thatcher ndiye aliyemsaidia Moi kuwa Rais wa Kenya; na ndiye pia aliyemfanya aendelee kubakia madarakani hadi wakati huo. Alikuwa anajua pia kwamba (Moi) alikuwa mbioni kumfukuza Makamu wake wa Rais, Mwai Kibaki (Rais wa sasa wa Kenya) katikati ya pingamizi kubwa, kwa kutoelewana naye.

Na ili aweze kutekeleza hilo, angehitaji msaada wa Uingereza kuweka hali sawa nchini. Kwa hiyo, Mama huyo alitumia nafasi tete iliyomkabili Moi kumshinikiza, sio tu kumrejesha Ouko kwenye wizara yake ya zamani; bali pia kumteua kuwa Makamu wa Rais wa Kenya. Moi alitekeleza agizo la kwanza la Thatcher la kumteua Ouko kuwa mbunge licha ya kushindwa katika uchaguzi; na akamteua pia kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa; lakini akakaidi kumteua kuwa Makamu wa Rais, badala yake akamteua Dakta Josephat Njuguna Karanja kuwa Makamu wake.

Kwa nini Moi hakumteua Ouko Makamu wa Rais? Moi alikuwa na mpango wa ‘kumrithisha’ nafasi ya urais mpwa wake, Nicholas Kiprono Arap Biwott, na hivyo kwamba, kama mwanasiasa mashuhuri aina ya Dakta Ouko angeshika nafasi ya Makamu wa Rais, uwezekano wa Biwott kumrithi mjomba wake (Moi) ungekuwa shakani.

Kukataa kwa Moi kumteua Ouko kuwa Makamu wa Rais kulimuudhi sana Mama Thatcher, na akawaambukiza chuki hiyo marais Ronald Reagan (Marekani) na George W. Bush dhidi ya Moi na serikali yake iliyonuka ufisadi kiasi kwamba, mapema Septemba 1989, Moi alipomtuma Dakta Ouko kwenda nchi za nje kuomba misaada, nchi hizo mbili na zingine, zilikataa kusaidia, kwa hofu ya misaada hiyo kufujwa.

 Hata hivyo, Karanja alitumikia nafasi ya umakamu wa rais kwa mwaka mmoja tu; kisha akaondolewa madarakani, na nafasi yake ikashikwa na Profesa George Saitoti. Baadhi ya vinara wa ufisadi waliokingiwa kifua na Serikali ya Moi walitajwa kuwa ni pamoja na mawaziri Biwott, George Saitoti, Arthur Magugu; Hezekiah Oyugi, mtoto wa kiume wa Moi aitwaye Mark Too, na wengine.

Ilikadiriwa kuwa mwanzoni mwa mwaka 1988 pekee, zaidi ya dola za Kimarekani milioni 175 zilikuwa katika akaunti za viongozi nchi za nje; na kadri ufisadi huo ulivyokua kwa kasi kubwa wakati wa utawala wa Moi, hesabu hiyo ilipanda haraka kufikia dola bilioni nne mwishoni mwa 1988.

Oktoba 1989, Dakta Ouko alimwelezea Rais Moi juu ya nchi za Magharibi kukataa kuisaidia nchi yake, lakini hakufurahia taarifa ya Ouko. Na badala ya Moi kuyapa uzito aliyofahamishwa na waziri wake, aliagiza yapuuzwe na akaendelea kumtangaza Ouko kama “adui wa Kenya na Wakenya namba moja”.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .