THE RISE AND FALL OF ABOUD JUMBE MWINYI (sehemu ya kwanza)
BAADA ya kutizama historia ya mwanasiasa nguli nchini Kenya, Robert Ouko, sasa ni zamu ya mwanasiasa na mwanaharakati nguli kutoka katika visiwa vya Zanzibar, Alhaji Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi. Miaka 32 iliyopita, Januari 1984, Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama cha
Mapinduzi (CCM), inayoongoza serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliketi mjini Dodoma.
Kikao hicho kilichokutana kwa dharura kiliazimia kwa kauli moja, kumvua nafasi zote za uongozi, Rais wa Awamu ya Pili wa Zanzibar,
Alhaj Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi kwa kutenda ‘dhambi kuu’ ya kuhoji
muundo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Nyadhifa alizovuliwa kiongozi huyo na kubakia kuwa raia wa kawaida na
kuwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani kwake kwa kipindi kadhaa, ni
pamoja na urais wa Zanzibar, uenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, umakamu
wa Rais wa Tanzania na umakamu Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Mkutano huo ulitawaliwa na kampeni chafu dhidi ya Jumbe, huku kambi
mbili za Zanzibar zikiumana, kwa kambi moja kuunda tuhuma dhidi yake na
nyingine kujibu mapigo, na hivyo kuchonga ufa na uhasama mkubwa miongoni
mwa viongozi wa Zanzibar kati ya kambi mbili hizo kinzani; kambi
iliyojiita ya ‘Wakombozi’ (Liberators), iliyoundwa na waliojiona kama
watetezi halisi wa Mapinduzi ya 1964 na ile ya kambi ya ‘Wanamstari wa
mbele’ (Front liners), iliyotaka mabadiliko ya sera visiwani.
Katika msuguano huo, Kamati ya Wakombozi ilishindwa na Rais Jumbe
akatunguliwa kwa mzinga mzito, akaisha. Jumbe alikuwa mrithi wa Rais wa
kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, aliyeuawa katika jaribio
la mapinduzi ya kijeshi lililoshindwa, Aprili 7, 1972. Kabla ya hapo,
Jumbe alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais,
akishughulikia mambo ya Muungano.
Kuuawa kwa Karume kulifikisha tamati ya utawala wa awamu ya kwanza
kufuatia Mapinduzi ya 1964, utawala uliotawaliwa na vitisho, hofu,
umwagaji damu na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya yeyote
aliyetoa sauti kuhoji utawala huo, na au kwa aliyedhaniwa tu kuwa
mpinzani wa Mapinduzi.
Uporaji huo wa demokrasia, ulitekelezwa na utawala wa Karume kupitia
genge katili lilojulikana kwa jina la ‘The Gang of Fourteen (Genge la
Watu 14), likiongozwa na Kanali Seif Bakari. Kugongewa mlango tu usiku
na genge hilo enzi hizo, kulitosha mtu kupatwa hofu kabla ya kuhojiwa.
Genge hili na sehemu kubwa ya wajumbe wa Baraza la Mapinduzi,
walitaka kuendelezwa kwa sera za Karume, na mtu pekee waliyeona angeweza
kufanikisha hilo kama mrithi halali wa Karume, ni huyo Kanali Seif
Bakari.
Hata hivyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa wakati huo,
Mwalimu Julius Nyerere aliposikia hilo, akaona giza mbele. “Sera za
Karume tena? Ukatili na mauaji ya kutisha kwa watu wasio na hatia?
Hapana!” alisikika Mwalimu aking’aka mbele ya watu wake wa karibu, na
kuamua kutokubaliana na pendekezo la Wazanzibari lililomtaka Kanali
Bakari kumrithi Karume.
Akajenga hoja nzito kupangua kisayansi hoja hiyo
kwa kuhusisha na tukio la kuuawa kwa Karume! Jaribio la mapinduzi lililoshindwa liliandaliwa na wanasiasa makini
wa Kizanzibari kwa kuhusisha baadhi ya wanajeshi wa Jeshi la Zanzibar,
ambalo hadi akiuawa, Karume alikuwa bado Amiri Jeshi Mkuu wake; kwa
kushirikisha pia wanajeshi kadhaa wa Kizanzibari waliokuwa kwenye Jeshi
la Wananchi wa Tanzania (JWT) kwa upande wa Bara.
Muuaji wa Karume, Luteni Hamoud Mohammed Hamoud, alikuwa wa Jeshi la
Zanzibar. Alichukua hatua hiyo yeye mwenyewe baada ya kuhisi kwamba
mpango wa mapinduzi umegunduliwa siku hiyo, na kwamba yeye na wenzake
walikuwa wanatafutwa; na kwa sababu kikosi cha pili cha mapinduzi kutoka
Dar es Salaam kilishindwa kufika Zanzibar muda uliopangwa, baada ya
kuonywa kikiwa baharini juu ya kugunduliwa kwa mpango huo na kurejea
hima Dar es Salaam.
Luteni Hamoud aliona kwa mikasa hiyo miwili, kwa vyovyote vile,
angekamatwa na kuuawa kikatili, akaamua na lolote liwe, na bila kupoteza
muda akaamua kutekeleza mauaji hayo yeye mwenyewe na wenzake wengine
watatu tu.
Imeelezwa kwamba ushiriki wa Luteni Hamoud katika jaribio hilo, mbali
na kubeba hisia (sentiments) za kisiasa, pia alidhamiria siku nyingi
tangu nyuma, kulipiza kisasi kwa Karume kwa kifo cha baba yake, Mzee
Mohammed Hamoud, aliyeuawa kikatili na kiongozi huyo akiwa kizuizini kwa
sababu za kisiasa.
Mwalimu Nyerere hakutaka mauaji ya Rais Karume yatafsiriwe au
yahusishwe na jaribio la mapinduzi, bali alitaka yatafsiriwe kama mauaji
ya kisiasa tu. Akasema, hatua yoyote ya kumteua Kanali Seif Bakari
ambaye ni mwanajeshi, kuchukua nafasi ya Karume aliyeuawa na mwanajeshi
pia, kungetafsiriwa kama Mapinduzi ya Kijeshi. Hapo, Wazanzibari
wakanywea, wakatazamana kwa ishara bila kupata jibu kwa hoja ya Mwalimu
Nyerere. Hawakuwa na namna isipokuwa kufuta pendekezo la uteuzi wa
Kanali Seif Bakari kumrithi Karume.
Ndipo ikawadia zamu ya Mwalimu Nyerere kushawishi na kushauri nani
ateuliwe. Akasema, pamoja na kuuawa kwa Karume, ambaye alikuwa mwasisi
mwenza wa Muungano wa Tanzania, Muungano huo lazima uendelezwe bila
kuyumba; na mtu pekee aliyefaa, kwa maoni ya Nyerere, alikuwa ni Aboud
Jumbe Mwinyi, kwa sababu kuu tatu:-
Mosi, ni msomi na mwanasiasa mkongwe mwenye kuzielewa vyema siasa na migongano ya jamii ya Kizanzibari. Pili, ni mtu ambaye hakuwa na majungu
wala makundi yenye kuhasimiana. Tatu, wadhifa wake wa Waziri wa nchi,
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais (Mambo ya Muungano) kwa muda mrefu,
ilikuwa ni sifa ya ziada iliyompa uzoefu, na uwezo wa kuendeleza na
kudumisha Muungano. Hoja ya Mwalimu ikapita; Jumbe akapaa, akawa Rais
wa Zanzibar wa awamu ya pili.
Jumbe na Mwalimu Nyerere walifanana kwa mengi. Wote walikuwa wasomi
waliosoma pamoja Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda, na kisha wote wakawa
walimu wa sekondari.
Kwa uhusiano mzuri huo, Jumbe alianza kulegeza
mengi yenye ukakasi visiwani ambayo yasingewezekana enzi za Karume
ambaye aligeuka mwiba kwa Mwalimu, akidai mara nyingi wavunje Muungano
kwa kuwa uligeuka koti lililowabana Wazanzibari. Chini ya Jumbe,
misuguano kati ya Bara na Visiwani ambayo kabla yake ilizua kero za
Muungano, ilianza kutoweka.
Jumbe alianza kukubalika haraka kwa wengi Visiwani na Bara; akawa
kipenzi cha Rais wa Muungano, naye akaanza kupaona Bara kama nyumbani
kwake. Akajenga makazi yake eneo la Mjimwema, Dar es Salaam. Akilala
Mjimwema na kila asubuhi aliruka kwa ndege kwenda Ikulu ya Unguja na
kurejea tena jioni baada ya kazi. Ufanisi wake wa kuihudumia Zanzibar
ulipungua kwa sababu ya kuweka nguvu kubwa zaidi kwenye Muungano.
Na
kadri alivyozidisha ziara za kirais Bara na nje ya nchi kumwakilisha
Mwalimu, (majukumu ambayo Mwalimu hakuthubutu katu kumpa Karume), ndivyo
alivyozidi kujiweka mbali na siasa za Zanzibar na Wazanzibari.
Kwa kutumia hali hiyo ya maridhiano, Mwalimu alizidi kuchanja mbuga
kwenda mbele zaidi bila Jumbe kushuku kitu. Katika kikao cha pamoja cha
NEC ya TANU cha Bara na NEC ya ASP cha Zanzibar, kilichofanyika Dar es
Salaam, Septemba 5, 1975, Mwalimu Nyerere alipendekeza vyama hivyo
viungane ili kuimarisha zaidi Muungano.
Jumbe alikubali kimsingi wazo hilo, lakini akataka ASP kipewe muda
kufikiria zaidi. Mwaka mmoja baadaye, Oktoba 1976, maridhiano yakafikiwa
ya kuunda Chama kipya ‘Chama cha Mapinduzi’ (CCM), kilichozinduliwa
Februari 5, 1977, tarehe na mwezi sawa na ilipozaliwa ASP miaka 20
nyuma, mwaka 1957.
Licha ya Wazanzibari kushinikiza tarehe na mwezi wa kuzaliwa chama
chao, yaani Februari 5, walishinikiza pia na kufanikiwa kubakiza neno
‘Mapinduzi’ yaliyoleta uhuru wao Januari 12, 1964, liwe sehemu ya jina
la chama kipya. Kwa maana ya Chama cha Mapinduzi bila kuwa na tafsiri
yake kwa lugha ya Kiingereza.
Na hizo ndizo zilikuwa karata mbili pekee kwa Wazanzibari kukubali
kuunda Chama kipya, chama ambacho kilipewa ukuu wa kikatiba wa kushika
hatamu zote za uongozi wa nchi na kuweza kumng’oa madarakani Jumbe miaka
saba baadaye, mwaka 1984, kama kitanzi alichojitengenezea mwenyewe.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Hati (Mkataba) ya Muungano ya Aprili 22, 1964,
vyama vya siasa si jambo la Muungano kuweza kusimamia mamlaka za
Muungano. Hivyo utaratibu uliotumika kumng’oa Jumbe unahojika kisheria!
Kadri Jumbe alivyozidi kujiona kukubalika kwa Mwalimu Nyerere, ndivyo
alivyojiona pia kama mrithi halali mtarajiwa wa Rais wa Muungano kuliko
mtu mwingine yeyote, Bara na Visiwani. Lakini kutokuwepo kwake Zanzibar
mara kwa mara kulizua ombwe la uongozi kwa kuwa kila kitu kilimsubiri
yeye, hata kama ni idhini ya kukata mti. Na kwa jambo la dharura, Waziri
mwenye dhamana ya dharura hiyo ilibidi amfuate Dar es salaam.
Kana kwamba ombwe hilo halikutosha, hofu ilitanda miongoni mwa
Wazanzibari pale Mwalimu alipopendekeza mabadiliko zaidi ya Katiba
kutaka kuunda Serikali moja badala ya Serikali mbili, wakihofia nchi
yao kumezwa na Tanganyika. Hali hii ilimweka pabaya Jumbe Visiwani juu
ya uswahiba wake na Nyerere, wakimwita ‘msaliti’ wa Mapinduzi ya
Zanzibar na Wazanzibari.
uona hivyo, Jumbe alianza kugeuka nyuma kwa kuchanganyikiwa; akawa
njia panda. Wakati hilo halijapoa, jingine kubwa zaidi lilikuwa njiani
likija. Mwaka 1983, Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi
wa Muungano, aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu. Sokoine alikuwa na mvuto wa
watu, shupavu na mwadilifu kiasi kwamba katika kipindi kifupi tu
alijidhihirisha kuwa chaguo la watu na mrithi halali wa Mwalimu, ambaye
naye alimkubali kwa ishara na kwa vitendo.
Kwa kuridhika na Sokoine, taratibu Mwalimu alianza kumbeza Jumbe kwa
sababu nyingi, lakini itoshe hapa kutaja mbili tu. Kwanza, alimwona
kama kiongozi mpweke asiye na sapoti na aliyepoteza mvuto Visiwani, pia
kama dikteta mkimya asiyeshaurika na watu wa chini yake.
Pili; Mwalimu aliudhika kwa Jumbe kugeuka mhafidhina wa kidini na
mpambanaji wa Kiislamu katika Taifa lisilo na dini. Kwa hili, Jumbe
alizuru nchi nzima akitoa hotuba kwenye misikiti, na Serikali
ikalazimika kutoa Waraka mkali wa Rais, kuwakumbusha na kuwataka
viongozi wa kitaifa kutojipambanua au kuendekeza mambo ya kidini. Jumbe
alipuuza Waraka huo; kwake ndio kukawa kumekucha.
Habari za Mwalimu kupoteza imani na upendeleo kwa Jumbe hatimaye
zilimfikia kiongozi huyo, zikamuuma sana na kumvunja moyo. Hapo uhasama
ukazuka kati yake na Mwalimu kwa njia ya kukomoana. Kwa hasira na kukata
tamaa, Jumbe akaanza maandalizi ya kuumbua Muungano, kwa minyukano na
Mwalimu.
Kuanzisha minyukano hiyo, ilikuwa ni lazima kwanza Jumbe arejeshe
imani yake iliyopotea kwa Wazanzibari, kutokana na hatua yake ya kuhamia
Mji mwema, Kigamboni na kwa kuwatelekeza Wazanzibari. Baada ya
kuridhika kwamba mambo ameyaweka sawa, aliomba mawazo ya Makatibu Wakuu
wa Wizara zote na Watendaji Wakuu wengine wa Serikali, ni aina gani ya
Muungano unaotakiwa.
Wote, isipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Zanzibar, Damian
Lubuva, walikataa muundo wa sasa wa Serikali mbili au wa Serikali moja
uliokuwa umeanza kupigiwa upatu na Mwalimu na baadhi ya wanasiasa. Jumbe
na watendaji wake hao ndani ya Serikali ya Zanzibar wakapendekeza
muundo wa Shirikisho lenye Serikali tatu. Serikali ya Tanganyika,
Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano kwa mambo kumi na moja tu
yaliyoainishwa katika Mkataba wa awali wa Muungano.
Mtizamo huo ndio aliouweka wazi Jumbe baadaye katika kitabu chake
kiitwacho ‘The Partnership,’ yaani ‘Ubia kati ya Tanganyika na
Zanzibar,’ kilichosambazwa mwaka 1984. Kuthibitisha hilo, ananukuu ibara
ya tano ya Mkataba wa Muungano inayosema kwamba kufuatia kuundwa kwa
Serikali ya Muungano, “Sheria za Tanganyika zilizopo na zile za
Zanzibar, zitaendelea kuwa na nguvu katika nchi hizo.” (The Partnership,
uk. 22).
Vivyo hivyo, anathibitisha kwa kunukuu Ibara ya Sita (a) ya Mkataba,
inayotanabahisha kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano, atasaidiwa na Makamu
wawili wa Rais (mmoja kwa ajili ya Tanganyika na mwingine kwa ajili ya
Zanzibar), Mawaziri na Maofisa wengine anaoweza kuwateua kutoka
Tanganyika na Zanzibar ambapo kufuatia uteuzi huo, utumishi wao
utahamishiwa kwenye utumishi wa Serikali ya Muungano.
Anahoji: “Kwa kuwa Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano Namba 22
ya 1964, vinatambua uwapo na kubakia kwa Serikali za Tanganyika na
Zanzibar baada ya Muungano, kwanini Muundo uliokusudiwa usitafsiriwe
kuwa Shirikisho? Kama Tanganyika na Zanzibar zinatajwa kuwa nchi ndani
ya Muungano, lakini kwa vitendo na hulka kuna nchi ya Zanzibar pekee,
Tanganyika ilikwenda wapi?
Hatua iliyofuata na aliyochukua Jumbe, ilikuwa ni kumrejesha kwao
Tanzania Bara, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Damian Lubuva, akimwelezea
kama mtumishi asiyeweza kusimamia maslahi ya Wazanzibari; na badala yake
akamteua rafiki yake wa zamani, raia wa Ghana, Alhaj Bashir K. Swanzy
kuwa Mwanasheria Mkuu.
Kuanzia hapo, madai ya Wazanzibari kutaka mabadiliko ya Katiba, huku
wengine wakitaka warejeshewe Visiwa vyao (Zanzibar), kupitia mihadhara,
magazeti na redio, yalipamba moto ambapo wanajeshi wa Kizanzibari nao
walikuwa na malalamiko yao.
Mashambulizi yenye kashfa nzito nzito na matusi ya kisiasa
yaliongozwa na redio ya ufichoni iliyopachikwa jina la ‘Kiroboto
Tapes,’ hadi ilipogunduliwa na kuharibiwa na wanajeshi kutoka Bara.
Mitafaruku yote hii ilikuwa na ridhaa ya Alhaj, Sheikh Aboud Jumbe
Mwinyi.
Wiki ijayo, tutaona jinsi Jumbe alivyoandaa mashitaka dhidi ya
Jamhuri ya Muungano kwenye Mahakama Maalum ya Katiba, lakini
akatunguliwa kabla ya kufika Mahakamani.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :