UTATA KIFO CHA KARUME, CHUKI AU MAPINDUZI?

No comments
Saturday, April 9, 2016 By danielmjema.blogspot.com


Joseph Mihangwa, Toleo la 237 (sehemu ya Nne)
SEHEMU ya tatu ya makala haya toleo lililopita, tuliona jinsi na namna mipango ya kupindua Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilivyoandaliwa kwa kuhusisha vikundi viwili; yaani kundi la Wazanzibari, wengi wao wakiwa wanajeshi, kutoka Dar es Salaam lililopanga kuwasili Zanzibar usiku wa manane kuamkia Aprili 7 na kundi la Wazanzibari ndani ya Zanzibar, lililojumuisha wanajeshi na raia.


Tuliona, baada ya kundi la Dar es Salaam kutowasili Zanzibar saa iliyopangwa, na Serikali ya Zanzibar kugundua kuibiwa kwa silaha Kambi ya Bavuai ambazo zingetumika katika Mapinduzi, na Luteni Hamoud na Kapteni Ahmada kuanza kufuatiliwa na wakuu wa Jeshi, wanajeshi hao waliamua kutekeleza zoezi hilo wenyewe kwa kumuua Rais Abeid Amani Karume dhidi ya ushauri wa washirika wao wa kuahirisha mapinduzi.

Tuseme, kwa mfano, kwamba kundi la Dar es Salaam lingewasili Zanzibar kwa kazi hiyo kama ilivyopangwa, Mapinduzi yangetekelezwaje? Kwa mujibu wa mkakati wa Mapinduzi uliofikiwa Aprili 2, 1972, Suleiman Mohamed Abdullah Sisi (mwanajeshi wa JWTZ, mkazi wa Ilala Flats, Dar es Salaam) alipangwa kuongoza utekaji wa kambi ya Jeshi, Mtoni, ambapo Kapteni Ahmada, alitakiwa kuteka kambi ya Jeshi, Bavuai, Makao Makuu ya Jeshi na Chuo cha Jeshi cha mafunzo ya Redio, vyote hivi viko eneo la Migombani.

Kituo cha Polisi cha Malindi kingeshambuliwa na kutekwa na kikundi chenye silaha kikiongozwa na Luteni Hamoud ambacho kingeweza kuteka magari yenye Redio za mawasiliano. Askari Yusufu Ramadhan angeongoza kikundi cha maafisa wa Polisi walioingizwa kwenye mpango huo na kuteka Kituo cha Polisi cha Ziwani.

Amour Dughesh (mwanajeshi; Zanzibar), yeye angeteka Ikulu na kumkamata Karume, kisha kumpeleka Kituo cha Redio kumlazimisha atangaze kupinduliwa kwa Serikali yake.  Baada ya hapo, Kituo hicho kingeachwa chini ya udhibiti wa Badawi, Mpatani na Mohamed Said Mtendeni (mwandishi wa habari, gazeti la China, mkazi wa Vuga, Unguja).

Uwanja wa Ndege ungetekwa na kikosi cha wanajeshi na baada ya hapo kingeachwa chini ya udhibiti wa Ali Sultan Issa (meneja wa Shirika la Mafuta, Zanzibar). Mpango huo ulilenga pia kuteka Makao Makuu ya Umoja wa Vijana wa ASP, ambayo yalikuwa pia Makao Makuu ya Idara ya Usalama wa Taifa Zanzibar, ikiongozwa na Kanali Seif Bakari na kuwekwa chini ya udhibiti wa Mohamed Abdullah Baramia, Kapteni Khamis Abdullah Ameir, wa Makao Makuu ya Jeshi, Zanzibar; yeye alipangwa kuzuia mashambulizi kutoka nje kama Mapinduzi yangefanikiwa.

Mapinduzi au mauaji ya Kisiasa?

Mapinduzi ni kitendo cha kutaka kubadili sawia hali, serikali au mfumo fulani wa kijamii kwa matumizi ya nguvu, ikiwa ni pamoja na kuondoa mhimili wa mfumo huo. Mapinduzi yanaweza kuwa kwa njia ya jeshi kama jeshi limetumika au ya kiraia kama raia walitumika, kama yalivyokuwa Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.

Mauaji ya Karume hayawezi kuitwa mapinduzi ya kijeshi wala ya kiraia kwa sababu kifo chake hakikubadili mfumo wala muundo wa serikali.  Haya yanaweza kuitwa mauaji ya kisiasa yenye lengo la kuondoa chanzo au mhimili wa kero katika jamii bila kubadili serikali.

Mwanazuoni mahiri Barani Afrika, Profesa Ali Mazrui, anatafsiri “mauaji ya kisiasa (political assassination) kuwa ni kitendo cha siri cha kutoa uhai wa mtu mashuhuri kisiasa, kinachofanywa na wakala asiye wa serikali; kwa sababu za kisiasa au zisizofahamika.

Naye Profesa William Gutteridge wa Chuo Kikuu cha Aston, anasema mauaji ya kisiasa kuwa ni kitendo cha kutoa uhai wa mtu mashuhuri katika jamii kwa sababu za kisiasa na kinajumuisha pia jaribio la mapinduzi lililoshindwa na watu wengi kuuawa katika kutekeleza kilichokusudiwa.

Kwa mantiki hii, mauaji ya Karume, kama yalivyokuwa mauaji ya Rais Anwar Sadat wa Misri, kwa kupigwa risasi wakati akiangalia gwaride la jeshi lake, yalikuwa na lengo la kuiondolea jamii kero bila umuhimu wa kubadili serikali.  Katika mauaji kama hayo, mlengwa huwa mmoja tu kama chanzo au mhimili wa kero.

Karume aliuawa kwa sababu ya utawala wa kimabavu, ukatili na ukiukaji wa haki za binadamu kama tulivyoona hapo juu; wakati Sadat aliuawa kwa kuisaliti jamii ya Kimisri, kwa kusaini Mkataba wa suluhu kati ya Misri na Israeli uliojulikana kama “Camp David” ili kusitisha harakati za Waarabu dhidi ya Uzayuni wa Kiyahudi.

Sababu nyingine ilikuwa ni kukumbatia sera za kiuchumi za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), hatua iliyoathiri maisha ya Wamisri kiuchumi na matarajio ya kijamii ya Waislamu nchini humo na Jumuiya pana ya Kiarabu kwa ujumla.

Malengo ya mauaji ya Karume yanajidhihirisha kwa vielelezo kwa yale yaliyofuatia chini ya utawala wa mrithi wake, Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi, aliyechukua uongozi Aprili 11, 1972.
Baraza la Mapinduzi lililoketi Aprili 10 – 11, 1972, pamoja na kumthibitisha Jumbe kuanzia Aprili 7, 1972 kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza hilo, pia lilipitisha azimio la kudumisha, kulinda, kutetea na kuendeleza fikra, malengo ya kimapinduzi na sera alizoacha Karume.

Hata hivyo, Wazanzibari wengi walitaka Kanali Seif Bakari amrithi Karume kwa kuwa alikuwa mtu wa karibu zaidi kwa Karume kuliko Jumbe, kwamba ndiye pekee miongoni mwa Wazanzibari ambaye angeweza kuendeleza fikra za mwasisi huyo wa Taifa la Zanzibar.

Nyerere aliingilia kati akiwa na hoja kwamba, kwa kuwa Rais Karume aliuawa na mwanajeshi, kumteua Bakari ambaye alikuwa mwanajeshi kumrithi kiongozi wa kiraia, kungetafsiriwa kuwa mapinduzi ya kijeshi yaliyoweka mwanajeshi madarakani.  Hoja ya Nyerere ikashinda.

Kwa kuanzia, Jumbe alifuta Amri ya Karume ya kutoagiza chakula na bidhaa nyingine kutoka nje; akaruhusu akiba ya fedha za kigeni kutumika kuagiza chakula kumaliza tatizo la njaa na upungufu wa vitu, jambo lililokuwa mwiko wakati wa Karume.

Vivyo hivyo, kwa mara ya kwanza, Serikali ya Zanzibar iliruhusu wanafunzi 17 kutoka Zanzibar, kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuahidi kupeleka wengi zaidi.
Desemba 1972, ASP kilifanya Mkutano Mkuu wake wa kwanza tangu 1962 uliohudhuriwa na wajumbe zaidi ya 900 kutoka Visiwani, Mwalimu Nyerere na viongozi wengine wa TANU, pamoja na wageni wengine kutoka nchi 12 za Kiafrika, wakiwamo wawakilishi wa chama cha MPLA cha Angola.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Jumbe alilaani tawala za kimabavu na ubabe, ukandamizaji na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya raia, alisema: “Viongozi lazima wawatumikie watu, na si watu wawatumikie viongozi…..”Kwa maneno hayo, alikuwa amefungua milango ya demokrasia Visiwani, utawala bora, uwajibikaji na kuongoza kwa mifano, tofauti na enzi za Karume.

Februari 5, 1977, Nyerere na Jumbe waliunganisha vyama vyao, TANU na ASP, kuunda Chama cha Mapinduzi – CCM, jambo ambalo lisingewezekana wakati wa Karume ambaye hata Muungano wenyewe aliweza kuusigina kwa kisigino cha nguvu.  Vivyo hivyo, mwaka 1979, Zanzibar ilijipatia Katiba yake ya kwanza baada ya Katiba ya Uhuru ya 1963, chini ya Serikali ya Mseto wa Zanzibar Nationalist Party (ZNP) na Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP).
 
Ni wakati wa utawala wa Jumbe, Zanzibar ilipata Bunge (Baraza la Uwakilishi) lake la kwanza kwa njia ya uchaguzi, wakati kabla ya hapo, Karume aliapa pasingekuwa na uchaguzi Zanzibar kwa miaka 50, kuanzia 1964 hadi 2014.

Chini ya Jumbe, kwa mara ya kwanza tangu 1964, wanasheria waliruhusiwa kufanya kazi Zanzibar; watu hawakugongewa tena milango usiku na kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Na tazama, yote yalifanywa kuwa mapya, ambapo isingewezekana chini ya utawala wa Rais Karume.

Source: http://www.raiamwema.co.tz/utata-kifo-cha-karume-chuki-binafsi-au-mapinduzi-iv#sthash.7LLhjuwu.dpuf

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .