CONTE MAGUFULI: AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA KATIKA UWANJA WA MAZOEZI YA CHELSEA

Posted in
No comments
Saturday, April 9, 2016 By danielmjema.blogspot.com

KUMBE hata wazungu wameanza kumuiga Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli. Ndivyo ilivyotokea juzi jijini London baada ya kocha mpya wa Chelsea, Antonio Conte kufanya ziara ya ghafla katika uwanja wa mazoezi wa timu hiyo.

Conte hakutarajiwa kufanya ziara hiyo licha ya kutangazwa kuwa kocha mkuu wa Chelsea Jumatatu kutokana na ukweli kwamba kocha wa muda wa sasa, Guus Hiddink alikuwa mazoezini na wachezaji wake wakijiandaa na mechi zinazofuata.

Conte alitambulishwa kwa wachezaji wote wa Chelsea juzi na anatazamiwa kufanya vikao vya siri na kila mchezaji ambaye anataka kuondoka katika kikosi hicho kilichovurunda msimu huu kwa ajili ya kuwapa maoni yake.

Wachezaji walishangazwa na ujio wa Conte, ambaye mpaka sasa ni kocha wa timu ya taifa ya Italia na anatazamiwa kukiongoza kikosi hicho katika michuano ya Euro 2016 nchini Ufaransa. Aliwasili katika uwanja wa mazoezi wa Chelsea, Cobham akiwa na Mkurugenzi wa ufundi wa Chelsea, Michael Emenalo.

Conte anataka kujua wachezaji wanaotaka kuondoka kabla ya kukijenga upya kikosi chake na anatazamiwa kukutana na mastaa Eden Hazard, John Terry, Nemanja Matic na Diego Costa ambao hatima zao zipo shakani Stamford Bridge.

Hazard, ambaye anaendelea kujitibu na tatizo la nyonga, hana uhakika na hali yake ya baadaye Stamford Bridge huku akiwa anahusishwa na klabu za Paris Saint-Germain na Real Madrid ambazo zimedaiwa kumtaka.

Matic amekuwa akikerwa na maendeleo yake msimu huu baada ya kung’ara msimu uliopita ambapo alisaidia kwa kiasi kikubwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England na amekiri kwamba yupo tayari kuondoka huku Diego Costa akivutika na uhamisho wa kurudi Atletico Madrid.

Nahodha John Terry amerudisha matumaini ya kubaki klabuni licha ya kuonyeshwa mlango wa kutokea Januari mwaka huu baada ya Chelsea kuthibitisha kwamba haitampa mkataba mpya. Hata hivyo Conte anaweza kuamuru kuwa Terry mwenye umri wa miaka 35 aendelee kwa msimu mmoja zaidi.

Vile vile kumeanza kuwa na wasiwasi na hali ya baadaye ya golikipa namba moja wa Chelsea, Thibaut Courtois ambaye inadaiwa kuwa klabu za Barcelona na Real Madrid zimeanza kumfukuzia kipa huyo wa kimataifa wa Ubelgiji.

Baadhi ya wafanyakazi wa uwanja huo wa mazoezi pamoja na benchi la ufundi la Chelsea walishangazwa na ujio huo licha ya kocha Hiddink kuendelea kukiweka sawa kikosi chake kwa ajili ya pambano lijalo dhidi ya Swansea.

Hata hivyo inadaiwa kuwa Conte alikuwa anataka kupata picha halisi ya kikosi hicho kabla ya kujikita zaidi katika majukumu yake ya timu ya taifa nchini Ufaransa katika michuano ya Euro 2016 ili awe na sehemu ya kuanzia mara baada ya kumalizika kwa michuano hiyo.

Inadaiwa kuwa tayari ameanza kuwaandama wachezaji wa kukiimarisha kikosi cha Chelsea ambapo mmoja kati ya wachezaji anaowasaka ni kiungo wa nguvu wa AS Roma na timu ya taifa ya Ubelgiji, Radja Nainggolan.

Conte alipaa kwenda England katika siku ambayo waendesha mashkata nchini Italia wakitaka afungiwe miezi sita na kutozwa faini ya Pauni 6,000 kama akipatikana na hatia ya kupanga matokeo katika kipindi chake alichokuwa kocha wa Siena nchini humo.

Amekubali kusaini mkataba wa miaka mitatu na nusu Chelsea huku akilipwa dau la pauni 6.5 kwa mwaka akichukua jumla nafasi ya kocha wa zamani wa Chelsea, Jose Mourinho ambaye alitimuliwa Desemba mwaka jana kufuatia matokeo mabovu ya Chelsea katika michuano mbalimbali.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .