UTATA KIFO CHA KARUME, CHUKI AU MAPINDUZI?

No comments
Friday, April 8, 2016 By danielmjema.blogspot.com


Joseph Mihangwa, Toleo la 236 (sehemu ya tatu)
KATIKA sehemu ya pili ya makala haya wiki iliyopita, tuliona jinsi Rais Abeid Amani Karume alivyotawala kwa mkono wa chuma bila kufuata katiba wala utawala wa sheria, na hivyo kujitengenezea maadui wengi katika jamii ya Kizanzibari na kwa makada wenzake wa ASP wenye siasa za mrengo wa kushoto ambao, alianza kuwatimua kazi au kuwahamishia kwenye Serikali ya Muungano.

Tulimaliza kwa kuona kwa sehemu tu, jinsi alivyogeuka kuwa adha na kero kubwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kwa Muungano wenyewe, kiasi cha kuuweka Muungano huo kwenye hati hati ya kuvunjika.  Tuendelee na sehemu ya Tatu, kuona kilichofuata.

Karume alikuwa mwiba kwa Nyerere

Mbali ya Karume kuweka wazi kwa kusema kwamba, “Muungano ni kama koti tu; likikubana au kukuzidishia joto unalivua na kuendelea na safari yako”, pia alijipa ujasiri usio wa kawaida kwa kumkatalia Nyerere hadharani kila mara juu ya baadhi ya mambo ya Muungano akisema: “…..kama ni hivyo, sikubali, bora tuvunje Muungano”.

Ni ujasiri huu wa Karume usio wa kawaida juu ya jambo nyeti kama hili, uliofanya Nyerere atoe tamko lake maarufu juu ya hatima ya Muungano akisema:  “Kama watu wa Zanzibar, bila ya ulaghai kutoka nje, wataona ni bora kuvunja Muungano, mimi siwezi hata kidogo kuwapiga mabomu na kuwaua wananchi wa Zanzibar. 

Kama waliingia katika Muungano kwa hiari yao, vivyo hivyo wanaweza pia kujitenga kwa hiari yao.  Hatukuishinda Zanzibar (kuwafanya mateka) vitani” (Soma:  William Edgett Smith, “Mwalimu Julius K. Nyerere”, tafsiri ya Kiswahili na Paul Sozigwa, uk. 154).

Wakati Mwalimu alikuwa mstari wa mbele katika kupinga ubeberu wa Marekani wakati wa vita ya Vietnam, na kwa ukombozi wa nchi za dunia ya tatu kwa ujumla, Karume alimbeza na kutangaza adhabu kali Visiwani kwa yeyote aliyelaani na kupinga ubeberu, au kuimba nyimbo za kuikashifu Marekani.

Mwalimu alipokosana na Uingereza kwa nchi hiyo kuukingia kifua utawala wa kidhalimu, kibaguzi na wa mabavu (UDI) wa Ian Smith nchini Rhodesia Kusini (sasa Zimbabwe), na kwa sababu hiyo uhusiano wa Mwalimu na Balozi wa Uingereza nchini, Sir Horace Phillip kuingia mkwara, Karume alionyesha hadharani kila mara kusuhubiana na Balozi huyo kwa kicheko cha bashasha na uswahiba kwa chukizo kwa Nyerere.

Tunaweza kutua kidogo hapa kuangalia nyuma mazingira aliyokuwamo Karume, miezi michache kabla ya kifo chake; bila shaka tutabaini kuwa, kiongozi huyo alikuwa katikati ya uhasama na uadui wa kujitakia.

Kwanza alikuwa na uhasama mkubwa na jamii pana ya Kizanzibari kwa udikteta wake uliokithiri uliosababisha mauaji, watu kutiwa kizuizini au kuhamishiwa Bara. Pili, kulikuwa na tatizo la njaa na mlipuko wa malaria; mambo ambayo hakuonekana kujali.

Tatu, kulikuwa na uhasama mkubwa wa kisiasa kati yake na makada wenzake wenye siasa za Ki-Karl Marx ndani ya ASP waliomtuhumu kushindwa kuongoza, achilia mbali jamii ya Kiarabu aliyoitimua kikatili Zanzibar na iliyoendelea kutema laana kwake ughaibuni.

Nne,  kulikuwa na Nyerere ambaye alianza kumuona kama mzigo na kero kwa Serikali ya Muungano na kwa siasa za kimataifa.  Yote haya yalikuwa baruti tosha kuweza kulipuka na kumdhuru Karume kwa namna yoyote iwayo.

Ni nani huyu Luteni Hamoud?

Luteni Hamoud Mohamed Hamoud, alikuwa mtoto wa mzee Mohamed Hamoud ambaye alikamatwa na kutiwa kizuizini na Karume miezi kadhaa baada ya Mapinduzi ya Januari 1964, na hatimaye kufariki dunia akiwa kizuizini.

Miaka kadhaa baadaye, wakati Hamoud Hamoud akichukua mafunzo ya kijeshi huko Tashkent nchi iliyokuwa katika  Shirikisho la Urusi ya zamani, alifahamishwa na mmoja wa wanafunzi wenzake juu ya kuuawa kwa baba yake.  Kwa uchungu mkubwa, aliapa sawia na baadaye, kwamba angemuua Karume kulipiza kifo cha baba yake.

Mfumo wa Usalama wa Zanzibar ulioenea kila mahali, ulijulishwa haraka na mmoja wa ma-ofisa usalama waliokuwa kwenye mafunzo pamoja na Hamoud, juu ya kusudio hilo la Hamoud.

Lakini cha kushangaza ni kwamba, Hamoud aliporejea Zanzibar baada ya mafunzo hakukamatwa wala kuwekwa kwenye uangalizi; badala yake alipandishwa cheo kuwa luteni usu, katika sherehe iliyohudhuriwa na Karume mwenyewe kama Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Zanzibar.

Ikumbukwe kuwa, suala la Usalama wa Taifa halikuwa jambo la Muungano; liliongezwa kwenye orodha mwaka 1984 kufuatia kadhia ya Aboud Jumbe ya kuchafuka kwa hewa ya kisiasa Zanzibar, likaunganishwa kusomeka kwa pamoja na jambo la Ulinzi kuwa “Ulinzi na Usalama”.

Pale risasi ya Hamoud ilipochukua uhai wa Rais Karume miezi kadhaa baadaye, Serikali ilisisitiza kwamba, mauaji hayo yalikuwa sehemu ya njama kubwa ya kuangamiza Mapinduzi ya 1964, kutokana kwamba, Hamoud na wauaji wenzake walikuwa wanachama wa zamani wa Umma Party, kilichokiunga mkono ASP huko nyuma, na kukipa [ASP] mwelekeo bora wa kiitikadi [Ukomunisti] na kuheshimika kisiasa.

Kufuatia mauaji hayo, watu 1,100 walikamatwa na kuhojiwa.  Babu alikamatwa na kutiwa kizuizini Tanzania Bara kwa tuhuma za kuongoza mpango mzima; nao maofisa wa ngazi za juu wa Kizanzibari Jeshini Bara, kama Ali Mahfoudh na wengine, nao walishukiwa na kuondolewa kwenye utumishi wa Jeshi Tanzania Bara bila kurejeshwa Zanzibar.

Mgongano dhana ya mauaji

Kuna dhana mbili zinazogongana, lakini zote zenye nguvu; juu ya sababu za kuuawa kwa Karume. Dhana ya kwanza ni hii ya Hamoud kulipiza kisasi. Lakini suala la kulipiza kisasi linakoma pale tunapoona watu kama Kapteni Ahmada na raia Ali Chwaya ambao hawakuwa na uhusiano wa kifamilia na marehemu Mohamed Hamoud aliyeuawa, kujiingiza katika kulipiza kisasi.

Lakini, kama tutakavyoona baadaye, Kapteni Ahmada alijiingiza kama hatua tu ya kujisafisha kwa kujutia ushahidi wa uongo aliotoa dhidi ya Hanga na wenzake 18 waliouawa mwaka 1969, na yeye kuonekana kama adui na msaliti wa umma wa Kizanzibari.  Inapofikia hapo, inakuwa dhahiri kwamba mpango huo ulibeba hasira za jamii pana ya Kizanzibari.

Dhana ya pili ambayo ndiyo msimamo wa Serikali ni kwamba, mauaji hayo yalikuwa mpango mpana wa kupindua Serikali.  Dhana hii inapata nguvu kutokana na watu wengi kuhusishwa na tuhuma hizi, lakini kama tu tuhuma dhidi yao zilikuwa za kweli; vinginevyo dhana ya kwanza inashinda.

Mipango ilivyopangwa na kupangika

Chuki binafsi?  Hapana, Hamoud hakuwa peke yake; ilikuwa ghadhabu ya umma kwenye jamii pana ya Kizanzibari, kila kundi au sehemu ya jamii na malalamiko yake. Kwa mujibu wa taarifa za Usalama wa Taifa Zanzibar, mipango ya kupindua Serikali ya Karume ilianza kusukwa tangu 1967 – 1972 ndani ya Zanzibar na Tanzania Bara, ambako nyumba ya Abdulrahman Babu ilikuwa kituo cha mikutano ya Wazanzibari ya kupanga Mapinduzi hayo.

Kama hivi ndivyo, Karume alikuwa na sababu tosha kumtaka Nyerere kumrejesha Babu Zanzibar “kuhojiwa”, Februari 1972. Mkutano wa mwisho ulifanyika Aprili 2, 1972, ambapo ilikubaliwa Mapinduzi yatekelezwe Aprili 7, 1972, yakihusisha makundi mawili: kundi la Wazanzibari kutoka Bara, wengi wao wakiwa wanajeshi, na kundi la Wazanzibari ndani ya Zanzibar, likihusisha raia na wanajeshi wachache.

Pamoja na uamuzi huo, kikao kilitoa majukumu mazito kwa baadhi ya washiriki, ikiwa ni pamoja na Hamoud na Ahmada kupewa jukumu la kuiba silaha kutoka kambi ya kijeshi, Bavuai. Ilikubaliwa kuwa, Babu na wafuasi wake kutoka Bara wasafiri kwa mtumbwi kwenda Zanzibar Aprili 6 kuamkia alfajiri ya Aprili 7, na kufikia eneo lililopo kati ya mitambo mikuu ya mawasiliano [Cable and Wireless] na Klabu Starehe.

Baada ya hapo, Babu abakie amejificha kwenye nyumba ya Hamoud Hamoud, iliyotizamana na Klabu Starehe eneo la Shangani, kusubiri saa ya mapambano kuwadia. 

Kwa mujibu wa taarifa, Babu aliondoka Dar es Salaam kwa mtumbwi uliofungwa redio mbili za mawasiliano, jioni ya Aprili 6, safari iliyoelezwa kuwa ya “kuvua samaki”; wakati madhumuni halisi yalikuwa ni kuwafikisha Babu na wafuasi wake Visiwani usiku wa Aprili 6, kwa maandalizi kamili ya kupindua Serikali Jioni hiyo, Aprili 6, Uongozi wa Jeshi uligundua upotevu wa silaha nyingi Kambini Bavuai.  Na ingawa uongozi ulikuwa bado haujamhusisha mtu yeyote, lakini Hamoud, Hamada na askari wengine walianza kufuatiliwa kwa siri.

Yaelekea kufikia hapo, Babu alijulishwa na kuonywa kwa njia ya redio akiwa baharini, juu ya kugunduliwa kwa mpango mzima wa Mapinduzi; akakatiza safari na kurejea haraka Dar es Salaam hima.  Haijulikani kama wafuasi wake walikuwa wamekwishafika Zanzibar au la; au kama nao walijulishwa na kurejea Dar es Salaam. 

Lakini kuwapo Visiwani wanajeshi kama Kanali Mahfoudh  (Mkurugenzi wa Operesheni JWTZ, Dar es Salaam) na Luteni Hashil Seif (Kikosi cha Wanamaji, Ukonga, Dar es Salaam) saa ya kuuawa Karume, kunaonyesha baadhi yao tayari walikuwa Zanzibar kusubiri wenzao.

Saa 12.00 asubuhi, Aprili 7; Ali Khatibu Chwaya (raia) alikwenda kwa Ali Mshangama Issa (afisa wa tatu, meli M.V. Afrika, mkazi wa Zizi la Ng’ombe, Zanzibar), kumweleza juu ya kutowasili kwa kundi la Dar es Salaam. 

Baadaye asubuhi hiyo, Ali Mshangama, Chwaya, Miraji Mpatani  (karani wa shirika moja, Zanzibar), Mohammed Abdullah Baramia (Mtunza Bohari, Idara ya Elimu), Ahmada na Hamoud, walikutana nyumbani kwa Hamoud na kuonyesha kukerwa na kusikitishwa kwa kutowasili kwa wapanga mapinduzi kutoka Dar es Salaam, hasa wakijua pia kwamba, silaha zilizoibwa bado zilikuwa nyumbani kwa Hamoud, na hatari ya kuweza kugunduliwa.

Ilipofika saa 6.00 adhuhuri siku hiyo, Mshangama, Hashil Seif, Amar Saad Salim, maarufu kama “Kuku” (afisa usafirishaji, Idara ya Siha, Zanzibar) na Chwaya, walikutana nyumbani kwa Amar Saad ambako Mshangama, Hashil Seif na Baramia walipendekeza mpango wa kupindua Serikali uahirishwe hadi watakapopata taarifa tofauti kutoka Dar es Salaam.

Kwa hiyo, saa 9.00 mchana siku hiyo, saa mbili tu kabla ya kuuawa kwa Karume, Baramia alikwenda nyumbani kwa Hamoud eneo la Shangani kuwasilisha pendekezo hilo.

Alimkuta Miraji Mpatani nje ya nyumba na kumweleza Baramia kwamba, pamoja na kundi la Dar es Salaam kutowasili, Ahmada na Hamoud walishikilia Mapinduzi yafanyike tu siku hiyo, kwa sababu Ahmada alikuwa anatafutwa na maafisa wa Jeshi.

Je, ni kwa sababu hii Luteni Hamoud, Kapteni Ahmada na Chwaya waliamua kufanya Mapinduzi, licha ya wenzao kutaka yaahirishwe?.


Source: http://www.raiamwema.co.tz/utata-kifo-cha-karume-chuki-binafsi-au-mapinduzi-iii#sthash.gQoh2nhI.dpuf

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .