RAIS UHURU KENYATTA WA KENYA AAPA KUONGOZA KAMPENI DHIDI YA ICC

No comments
Friday, April 8, 2016 By danielmjema.blogspot.com

SIKU chache baada ya Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa (ICC), yenye makao makuu yake, The Hague, Uholanzi kutupilia mbali kesi dhidi ya Makamu wa Rais, William Ruto na Mwanahabari Joshua Arap Sang', Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta sasa ameapa kuendelea kuongoza kampeni ya kuifanyia mageuzi Mahakama hiyo.

Kauli hiyo ameitoa katika mahojiano maalum aliyofanyiwa na mwandishi wa DW, Daniel Pelz wakati wa ziara yake nchini Ujerumani. Alipoulizwa kama amezungumza na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel kuhusu kampeni yake ya kutaka mageuzi dhidi ya ICC au nchi za Afrika zijiondoe katika mahakama hiyo, Rais Kenyatta amesema hawakuligusia kabisa suala hilo. 

Amesema suala hilo halikuwa katika ajenda ya kuzungumzwa kwenye ziara yake ya sasa barani Ulaya. Kuhusu hatua ya kuungwa mkono na nchi kama vile Ujerumani na Ufaransa katika mchakato wa mageuzi hayo ya ICC, Rais Kenyatta amesema wanashinikiza na kuelezea kwa ufasaha kuhusu kesi yao kupitia nchi zilizosaini Mkataba wa Roma uliyoianzisha mahakama hiyo na kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambavyo ni vyombo muhimu kwa Kenya kushinikiza hoja yao.

Msimamo wa Kenya kuhusu ICC

Rais Kenyatta amesema wameelezea msimamo wao kuhusu mageuzi ya ICC kwa uwazi na wataendelea kufanya hivyo. Alipoulizwa kuhusu msimamo wa Kenya kama inataka mageuzi ya ICC au wanakubaliana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo, ambaye aliiambia DW kwamba ni bora nchi za Afrika ziondoke ICC, Rais Kenyatta alikuwa na haya ya kusema.
 
''Tunataka mageuzi, lakini pia tumejiandaa kuondoka ICC iwapo hatutafanikiwa kupata mageuzi muhimu tunayohitaji. Tunaiona mahakama hiyo kama isiyotekeleza mamlaka yake kama ilivyopaswa kufanya hivyo, wakati mkataba wa Roma ulivyoanzishwa kwa mara ya kwanza,'' alisema Kenyatta.

Pia Rais Kenyatta amezungumzia kuhusu wawekazaji wa Kijerumani ambapo amesema ni eneo muhimu la ziara yake kwa sababu anaamini Kenya ina uhusiano imara na Ujerumani. Amesema tayari kuna idadi kubwa ya makampuni ya Kijerumani yaliyowekeza Kenya na yanafanya biashara nzuri kabisa nchini humo, ingawa wanataka idadi hiyo iongezeke.
 
Rais Kenyatta na Angela Meikel

 Katika suala la rushwa iliyokithiri, ambalo wawekezaji wengi wa Kijerumani wana wasiwasi nalo, kiongozi huyo wa Kenya amesema nchi yake inasonga mbele haraka katika suala la kuleta mageuzi kwenye biashara.

Amesema wanalichukulia suala la rushwa kwa umakini mkubwa, kwani wanaimarisha sheria na kuanzisha muswada mpya unaomuhusu mtoaji na mpokeaji rushwa. Aidha, amebainisha kwamba baadhi ya mawaziri na watumishi wa umma kadhaa wamekamatwa.

Mahojiano hayo yalihitimishwa kwa kuzungumzia kitisho cha wanamgambo wa Al-Shabaab, ambapo Rais Kenyatta amesema ugaidi sio vita vya kitaifa, bali vya kimataifa. Amesema wanahitaji msaada na ushirikiano mkubwa kutoka Ujerumani na Ulaya kwa ujumla, kwenye maeneo kama ya kupeana taarifa za kijasusi, kupambana na itikadi kali na kukabiliana na chanzo cha siasa kali.

Mwandishi: Daniel Pelz/DW

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .