Mwandishi Wetu, Moshi
MAHAKAMA ya Hakimu mkazi Moshi, Leo imeahirisha Kesi ya Mauaji ya Bilionea wa Madini ya Tanzanite Jijini Arusha,Erasto Msuya (43), hadi Desemba 11 mwaka huu.
Kesi hiyo iliyotajwa katika Mahakama hiyo kwa mara
kwanza, Agosti 21, mwaka huu, mbele ya Hakimu Mkazi, Munga Sabuni, inawakabili
watuhumiwa 8 wanaodaiwa kuuwa kwa kukusudia kinyume cha Sheria ya Makosa ya
jinai, Kanuni ya 16, Kifungu cha 196.
Pamoja na idadi ya Watuhumiwa wanaodaiwa kuhusika na
Mauaji hayo ya kikatili, yaliyotokea Agosti 7, katika maeneo ya Mjohoroni,
wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, kukamilika, Upande wa Mashtaka, ukiongozwa
na Wakili, Janet Sekule, uliwasilisha Maombi ya kutaka Kesi hiyo ipangiwe Tarehe
mpya ili kupisha Upepelezi kukamilika.
Wakili Sekule, alisema kuwa kutokana na uzito wa Kesi
hiyo, Jamhuri ingependa kupatiwa muda wa kukusanya ushahidi wa kutosha ambao
utawasaidia katika kesi hiyo, ombi ambalo halikupata pingamizi lolote kutoka
upande wa Washtakiwa.
“Mheshimiwa
Hakimu, kutokana na uzito wa shauri la kuuwa kwa makusudi kinyume na kanuni
namba 16, kifungu cha 196 ya sheria za makosa ya jinai, inayowakabili washtakiwa
namba 1 hadi 8, Jamhuri inaiomba Mahakam yako tukufu, kupewa muda wa
kukamilisha ushahidi,” alisema Sekule.
Baada ya kuridhika na maelezo ya Maombi ya Upande wa
Jamhuri, Mahakama ya Hakimu Mkazi Munga Sabuni, iliahirisha Kesi hiyo hadi
Desemba 11, mwaka huu itakapofikishwa mbele ya Mahakama hiyo kwa ajili ya
kutajwa.
Katika Kesi hiyo, Mshtakiwa namba Tano, Joseph Damas
Mwakipesile “Chusa” (36), ambaye ni Mfanyabiashara Maarufu wa Madini anadaiwa
kuwa alishirikiana na Mshtakiwa Ally Mussa “Majeshi”, anayedaiwa kuwahi
kulitumikia Jeshi la kujenga Taifa (JKT), kabla ya kufukuzwa pamoja na wengine
6 kumuua kwa kumpiga Risasi 13, Bilionea wa Madini, Erasto Msuya (43).
Watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa mnamo, Agosti
7, mwaka huu majira ya6:30 mchana walifanya kitendo hicho kando ya barabara kuu ya Arusha– Moshi katika
eneo la Mjohoroni, Wilaya ya Hai, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Kilimanjaro (KIA).
Washtakiwa wengine ni, Sharif Mohamed Athuman (31), mchimbaji mdogo wa madini
na mkazi wa Kimandolu mkoani Arusha, Shaibu Jumanne Saidi maarufu kama Mredi
(38), mkazi wa Songambele, Wilaya ya Simanjiro, Jalila Zuberi Said (28), mkazi
wa Babati, Sadiki Mohammed Jabir ‘Msudani’ au ‘Mnubi’(32), mkazi wa Dar es Salaam
na Lang’ata wilayani Hai, Karim Kihundwa (33) mkazi wa Kijiji cha Lawate Wilaya
ya Siha na Mussa Juma Mangu (30), mkazi wa Shangarai kwa Mrefu mkoani Arusha.
|
0 MAOINI :