Na Mwandishi wetu, Kilimanjaro
MACHAVA FC ya Kilimanjaro, maarufu kama "mnyama mkali" imeutumia
vyema uwanja wake wa nyumbani wa Ushirika na kuibanjua Mpwapwa Stars
2-0 katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya Ligi ya mabingwa
(RCL) uliosukumizwa juzi, jumapili.
Mpwapwa ambao ni mabingwa wa Dodoma, ukiwa ndio mchezo wao wa kwanza
baada ya kutinga katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa moja kwa
moja, walianza mchezo huo kwa kasi wakilisakama lango la Machava kila
mara lakini mashambulizi yao yote katika dakika ya 7 na 13 yalishindwa
kuzaa matunda baada ya mashuti ya Kamugisha funugulu na Omary Mselem
yakiokolewa na mlinda mlango wa Machava.
Machava walicharuka katika Dakika ya 18 kipindi cha kwanza, wakitumia
sehemu ya kiungo kusukuma mashambulizi walifanikiwa kupata bao la
kuongoza kupitia kwa muuaji wao yule yule, Reality Lusajo, aliyewapiga
chenga mabeki wawili wa Mpwapwa kabla ya kutingisha nyavu.
Zikiwa zimesalia takribani dakika tatu timu ziende mapumziko, Lusajo
alirejea tena kufanya maangamizi katika lango la timu pinzani na
kulipatia timu yake goli la pili na la ushindi katika dakika ya 42
baada ya beki wa Mpwapwa Frank Dimo kuchelewa kuondosha mpira uliokuwa
unazagazagaa katika eneo la hatari.
Hilo ni bao la saba kwa Lusajo anayeongoza kwa kufumania nyavu tangu
mzunguko wa kwanza wa ligi kuanza ambapo katika mechi mbili zilizopita
alifunga mabao matano. Kwenye ligi ya mkoa wa Kilimanjaro pia aliibuka
mfungaji bora ambapo katika mechi saba alifunga mabao 8.
Kwa ushindi huo Machava iliyoanza raundi ya kwanza kwa kuiondosha
Flamingo ya Arusha kwa jumla ya mabao 6-2, imejiweka katika mazingira
mazuri itakapokwenda Dodoma kucheza mchezo wa pili na Mpwapwa stars
unaotarajiwa kupigwa Juni 1 ama 2 mwaka huu.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama ambaye alikuwa mgeni rasmi
akiongozana na Mkuu wa wilaya ya Moshi, Dk. Ibrahim Msengi
amewapongeza vijana wake na kuahidi kuendelea kuwaunga mkono
kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi.
Kwa upande wao, chama cha soka mkoa wa Kilimanjaro (KRFA), kupitia kwa
afisa habari wake, Yusuph Mazimu kimesema timu hiyo itaendelea kukaa
kambini kujiandaa na mchezo wa marejeano dhidi ya Mpwapwa na kuwataka
wadau wa soka mkoani humo kuendelea kuiunga mkono.

No comments:
Post a Comment