UKOSEFU WA MADAWA YA MAGONJWA YA AKILI CHANZO CHA KUONGEZEKA VICHAA KILIMANJARO
Posted in
No comments
Wednesday, May 1, 2013
By
danielmjema.blogspot.com
UKOSEFU wa dawa za magonjwa ya akili katika hospitali
na vituo vya afya mkoani Kilimanjaro, umeelezewa kuwa tatizo kubwa
linalosababisha kasi ya ugonjwa huo
kuzidi kuongezeka, na kuwatesa wananchi wengi wa mkoa huo.
Takwimu zinaonyesha kuwa watu wanaougua ugonjwa huo
wameongezeka kutoka 10,286 katika kipindi cha waka 2011 hadi kufikia 15,838
mwaka 2012.
Hayo yalibainishwa jana na kaimu mratibu wa magonjwa
ya akili mkoani Kilimanjaro Bi. Ester Maro, wakati akizungumza na gazeti hili
ofisini kwake kuhusiana na hali ya ugonjwa huo na jitihada ambazo zimekuwa
zikichukuliwa na serikali katika kukabiliana na tatizo hilo.
Bi. Maro ambaye ni afisa muuguzi kitengo cha
magonjwa ya akili katika hospitali ya
mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi, alisema pamoja na ugonjwa huo kuwatesa wananchi
wengi, dawa bado ni tatizo kubwa ambalo linakwamisha jitihada za mkoa za
kumaliza tatizo hilo.
“Hali ya magonjwa ya akili katika mkoa huu bado si
ya kuridhisha,na wagonjwa wanaougua ugonjwa huu wamekuwa wakiongezeka kwa kasi
sana kila kukicha,lakini pamoja na tatizo hili kuendelea kuwa kubwa upatikanaji
wa dawa umekuwa wa shida sana hali ambayo imekuwa ikiwafanya wananchi wengi
hasa wa kipato cha chini kukata tama kutokana na kukosa fedha za kununua dawa hizo
kwenye maduka ya dawa ya binafsi”alisema Bi. Maro.
Aidha alisema kukosekana kwa dawa kwenye hospitali
kunatokana na bohari ya dawa MSD nayo kukosa dawa hizo hali ambayo imekuwa
ikiwafanya madaktari na wauguzi katika vitengo vya magonjwa ya akili kuwaagiza
wagonjwa kwenda kununua dawa kwenye maduka ya dawa.
“Dawa za magonjwa ya akili zinauzwa kwa gharama
kubwa katika maduka ya dawa,hali hii huwakwaza wagonjwa wengi na kuwafanya
waache kutumia dawa na kuishia mitaani,lakini pia tatizo hili la ukosefu wa dawa
limezifanya familia nyingi kuwatenga wagonjwa wa akili kwa kuona hawawezi
kuwahudumia hivyo kuishia kuishi mitaani na kula majalalani”alisema
Kutokana na hali hiyo Bi. Maro aliishauri serikali
kuangalia uwezekano wa kuongeza bajeti ya dawa ili kupunguza tatizo hilo ambalo
limekuwa kero na kikwazo kikubwa kwa wagonjwa.
Akizungumza na TAIFA LETU.com, mganga mfawidhi wa Hospitali ya mkoa wa
Kilimanjaro Mawenzi Dkt.Saganda Kapalala alikiri kuwepo kwa tatizo kubwa la ukosefu wa
dawa za magonjwa ya akili na kusema kuwa hali hiyo imekuwa ikiwasumbua na
kuwaumiza kichwa madaktari na wauguzi wa kitengo hicho.
Alisema kutokana na tatizo hilo Hospitali imekuwa
ikijitahidi kununua dawa zamagonjwa hayo ili kupunguza tatizo na kuwasaidia
wagonjwa ambao wengi wao hawamudu gharama za dawa.
“Tatizo la dawa za magonjwa ya akili linaninyima
usingizi,kwani limekuwa tatizo kubwa na wagonjwa wanapofika hospitali na
kuagizwa wakanunue dawa huwa wanaona kama wanaonewa kutokana na kwamba
hospitali dawa hizi huwa zinatolewa bure,niwaombe MSD wajitahidi kuagiza dawa
hizi ili kutupunguzia mzigo na tatizo”alisema
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :