WABUNGE WAZICHAPA;FUFUKA RAIS WANGU NYERERE
Posted in
No comments
Friday, September 6, 2013
By
danielmjema.blogspot.com
UKUMBI wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma, jana uligeuka ulingo wa masumbwi, baada ya wabunge wa kambi ya upinzani kupigana hadharani na askari wa Bunge.
Wabunge hao walichapana ndani na nje ya ukumbi, hali iliyosababisha tafrani kubwa, huku maofisa usalama na askari polisi kutoka kituo kikuu mjini Dodoma, wakilazimika kuitwa kwenda kuongeza nguvu ili kukabiliana na hali hiyo.
Hatua ya vurugu hizo, ilikuja baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kunyanyuka ili kutaka kutoa hoja, ambapo Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alimtaka kukaa chini hali iliyowafanya wabunge wote wa upinzani kunyanyuka wakiashiria kumuunga mkono.
Sugu akatwa mtama, ajibu mapigo
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
Freeman Mbowe, akizungukwa na wabunge wa vyama vya upinzani kwa lengo la
kumlinda asitolewe nje kwa nguvu na polisi na maofisa wa usalama wa
Taifa, baada ya kutokea vurugu Bungeni mjini Dodoma jana.Kuchapana ngumi na mateke ndiyo ilikuwa sura mpya ya
Bunge jana mjini Dodoma, hali ambayo imeandika historia mpya ya chombo
hicho cha kutunga sheria tangu uhuru Desemba 9, 1961.
Pengine dalili za mvua ni mawingu, ndiyo maana baada ya hali kuanza kuwa tete ndani ya ukumbi wa bunge, Kiongozi wa Shughuli za Serikali bungeni ambaye pia ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliondoka katika ukumbi huo kimya kimya kabla hali haijafikia ilikofika kutokana na upinzani mkali wa kambi ya upinzani kupinga uamuzi wa Naibu Spika, Job Ndugai, kuamuru askari kumtoa nje Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Sakata la jana liliufanya ukumbi wa Bunge na nje ya viunga vyake, kuwa uwanja wa mapambano. Tukio hilo lililoanza saa 6:30 mchana muda mfupi baada ya wabunge kumaliza kupiga kura za kuamua kama Muswada wa Sheria wa Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba usitishwe kujadiliwa na wabunge hao ama uendelee, linaongeza harakati za mapambano bungeni katika hatua mpya zaidi kutoka kauli hadi vitendo vya kutwangana.
Kura hizo zilipigwa baada ya kutokea malumbano makali ndani Bunge kati ya kambi ya upinzani na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa upande mmoja na Serikali kwa upande mwingine. Awali kabla ya kupigwa kwa kura hizo, Naibu Spika Ndugai, aliwahoji wabunge wanaotaka muswada huo uendelee kujadiliwa waseme ‘Siyo’ na wasiotaka uendelee kujadiliwa wasema ‘Ndiyo’.
Katika upigaji kura ya namna hiyo, ilionekana kwamba wabunge waliosema ‘Siyo’ kwa maana uendelee, walikuwa ni wengi na wale waliosema ‘Ndiyo’ kwa maana usiendelee kujadiliwa walikuwa wachache.
Hata hivyo, Ndugai alipotaka Bunge liendelee kuujadili muswada huo, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, aliomba suala hilo liamriwe kwa kuulizwa mbunge mmoja mmoja.
Baada ya kuhojiwa mbunge mmoja mmoja, wabunge waliotaka muswada huo uendelee kujadiliwa bungeni, walishinda dhidi ya waliotaka uondolewe bungeni. Kwa mujibu wa matokeo ya kura hizo waliotaka muswada uendelee ni 156 na waliotaka uondolewe ni 59. Lakini Spika Ndugai alipomruhusu Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema, aendelee kuchangia hoja hiyo Mbowe alisimama akimuomba Naibu Spika ampe fursa ana jambo la muhimu la kuzungumza.
Hata hivyo, Ndugai alisisitiza kuwa katika hatua hiyo hataruhusu tena taarifa ama mwongozo kutoka kwa wabunge. Mbowe naye kwa upande wake, aliendelee kusimama na Naibu Spika alisisitiza kauli yake ya kumtaka Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akae katika kiti chake ili Bunge liendelee na kujadili hoja iliyokuwa mezani.
“Mheshimiwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, nakuomba kaa chini,” alisisitiza Ndugai, lakini Mbowe alimjibu: “Mheshimiwa Naibu Spika, nina hoja muhimu, naomba unipe fursa nizungumze.”
Ndipo Ndugai alipowaarifu askari wa Bunge wajiweke tayari kwa lolote linaloweza kutokea wakati wowote.
“Askari wa Bunge popote pale mlipo, jiwekeni tayari,” alisema na kurudia rudia kauli hiyo mara kadhaa na kumsisitiza Mbowe akae katika nafasi yake, lakini naye aliendelea kushikilia msimamo wake wa kusimama.
Baada ya hatua hiyo, Naibu Spika aliwaamuru askari wa Bunge wamtoe nje Mbowe ili shughuli za Bunge ziendelee, lakini wabunge wengine wa Chadema waliposikia amri hiyo ya Ndugai, walihama katika viti vyao haraka na kwenda kukaa jirani na Mbowe kuhakikisha kila upande analindwa.
Kitendo hicho kiliwafanya askari wa Bunge washindwe kutekeleza kwa haraka kitendo hicho kutokana na kupata upinzani mkubwa kutoka kwa wabunge wa Chadema, NCCR-Mageuzi hususan Moses Machali (NCCR-Mageuzi) na wa CUF.
Wakati hayo yakiendelea, yalijitokeza matukio kadhaa likiwamo la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuamua kutoka nje ya ukumbi wa Bunge huku baadhi ya maofisa wengine wa chombo hicho wakionekana kushauriana na Naibu Spika Ndugai, pengine kujaribu kumshawishi, aangalie namna nyingine ikiwamo ya kuahirisha Bunge ili kumaliza kadhia hiyo, lakini Ndugai alionekana kushikilia msimamo wake wa kuhakikisha kwamba Mbowe anatolewa nje ya ukumbi wa Bunge.
“Askari wa Bunge, ina maana mmeshindwa kumuondoa ndani ya ukumbi Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani? ...Nauliza kiongozi wa hawa askari ni nani?” alihoji Ndugai.
Baada ya dakika chache, kiongozi wa askari hao alikwenda kuzungumza na Ndugai na baadaye kwenda kwenye msongamano walipokuwapo askari wa Bunge waliokuwa wakitaka kumtoa Mbowe nje.
Yalitokea mabishano makali ndani ya Bunge kati ya wabunge wa Chadema na askari hao wa Bunge kwa takribani dakika 15 na ndipo walipoamua kutumia nguvu za ziada kuwakabili wabunge waliokuwa wakimzuia Mbowe kukamatwa.
Katika purukushani hizo, ndipo askari wa Bunge pamoja na baadhi ya askari kanzu na wa kawaida ambao jana walionekana kuongezeka katika viwanja vya Bunge, walipofanikiwa kuuvunja ‘ukuta’ wa wabunge uliokuwa umemzingira Mbowe.
Lakini katika kufanya hivyo, mmoja wa askari hao alimpiga teke Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu, wakati wakimuondoa kundini na kumdondosha chini kisha wakamsomba mzobe mzobe na kumtoa nje ya ukumbi wa Bunge huku wabunge wa CCM ambao kwa wakati wote huo walikuwa wametulia kwenye nafasi zao bungeni, wakishangilia.
Kitendo cha askari huyo ambaye hakufahamika jina lake mara moja kumpiga teke Mbilinyi, kilionekana kuwakera wabunge wengi wa Chadema na wa upinzani kwa ujumla.
“Wanampiga teke Mheshimiwa Mbunge aliyechaguliwa na wananchi, hii hapana haikubaliki.
Hawa si Usalama wa Taifa bali ni Usalama wa CCM na wapo kwa ajili ya kuilinda CCM,” alisikika mmoja wa wabunge hao wa upinzani akilalamika, kauli iliyorudiwa rudiwa na wabunge wengine wa kambi hiyo.
Aidha, wakati wa vurugu hizo, kulikuwa na madai kwamba Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Moza Said, mmoja wa askari alimvua vazi la hijab ambalo huvaliwa na waumini wa kike wa dini ya Kiislamu, kitendo kilicholalamikiwa sana na baadhi wabunge wanawake hasa wa Kiislamu.
Baada ya Sugu kutolewa nje ya ukumbi wa Bunge, ndipo askari wa Bunge, polisi, askari kanzu na wa usalama, walipofanikiwa kumsogelea Mbowe na kuanza kuondoka naye taratibu kutoka ndani ya ukumbi wa Bunge mithili ya watu wanaomsindikiza bibi harusi hadi kwenye viwanja vya Bunge jirani na kantini ya Bunge.
Mbowe alikuwa akisindikizwa na askari hao huku wabunge Sylivester Kasurumbayi (Chadema-Maswa Mashariki), John Mnyika (Chadema- Ubungo) na Machali (NCCR-Mageuzi - Kasulu Mjini), wakiwa karibu kabisa naye wakati wote.
NJE YA UKUMBI WA BUNGE
Wakati kundi kubwa la askari hao, wabunge na watu mbalimbali wakiwamo waandishi wa habari wakimfuatilia Mbowe kujua hatma yake, ghafla Mbunge Sugu aliwaponyoka askari aliokuwa nao jirani na ukumbi wa Pius Msekwa, na kwenda kwa kasi kisha akampiga teke na ngumi mmoja wa askari waliokuwa wamemzunguka Mbowe.
Baadhi ya wabunge wa upinzani walidai kuwa askari aliyepigwa ngumi na Sugu, ndiye aliyekuwa amempiga teke wakati wakimtoa ndani ya ukumbi wa Bunge, kwa hiyo kitendo hicho kilitafsriwa kama alikuwa akijibu mapigo.
Hata hivyo, Sugu aliyekuwa amefura kwa hasira, alidhibitiwa na askari waliokuwapo eneo hilo na kumweka pembeni kisha akapandishwa ndani ya gari la Kiongozi wa Kambi Rasmi Bungeni, Mbowe na kuondolewa haraka kutoka katika viunga vya Bunge na kupelekwa kusikojulikana.
Aidha, Mbowe ambaye muda mwingi akiwa na askari hao alionekana akitabasamu na asiye na wasiwasi, naye aliondoka taratibu bila kusukumwa na kwenda moja kwa moja hadi katika ofisi yake iliyopo bungeni hapo.
Vile vile, baada ya hali kutulia kidogo, wabunge wa Chadema na wengine wa upinzani, walionekana wakihamasishana waingie ndani ya ukumbi wa Pius Msekwa, kwa majadilianio kuhusiana na tukio hilo.
Hakukuwa na taarifa yoyote kutoka kwa wabunge hao kuhusu walichoafikiana baada ya kukaa ndani ya ukumbi huo kwa dakika zisizozidi 20 na kutoka.
Hata hivyo, baadaye zilipatikana taarifa kwamba walipanga kwenda kukutana eneo lingine nje ya Bunge na viunga vyake kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kuwakwepa maofisa wa Usalama wa Taifa kupata kile watakachoafikiana.
Vurugu hizo zilionekana kuwavuta hata watu waliokuwa nje kabisa ya uzio wa Bunge na wapita njia katika barabara kuu ya Dodoma-Dar ambao walisitisha shughuli zao na kuendelea kuangalia `sinema' ya bure iliyokuwa ikiendelea kwa wakati huo, katika viunga vya Bunge.
Wakati vurugu hizo zikiendelea nje ya ukumbi wa Bunge, Naibu Spika aliongeza muda wa dakika 30 ili wabunge ambao wengi wao walikuwa wa CCM, waendelee kuchangia hoja hiyo.
POLISI WAMSAKA SUGU
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi mkoani Dodoma, limesema linamsaka Mbunge Sugu kwa madai ya kumpiga kichwa mmoja wa askari wa Bunge na kunyofoa kipaza sauti ndani ya ukumbi wa Bunge.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Susan Kaganda, akizungumza na Mwandishi wetu kwa njia ya simu, alithibitisha kusakwa kwa mbunge huyo na kueleza kuwa askari wanaendelea kumtafuta ili aweze kuhojiwa juu ya ukweli wa madai hayo.
“Ni kweli vijana wangu wako kazini wanamsaka Mbunge Mbilinyi, tunataka kumuhoji juu ya madai hayo…tunaamini kwa kuwa ni Mbunge akipata taarifa kuwa tunamtafuta atakuja bila usumbufu,” alisema.
Hata hivyo, alivyoulizwa juu ya kuwapo kwa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa magari sita ya polisi yamesambazwa mtaani kwa ajili ya kumsaka Mbunge huyo, alisema kazi ya polisi ni kulinda raia na mali zao magari hayo yapo kwenye kazi kama kawaida na siyo kwa ajili ya kumsaka Mbunge.
PINDA: MUSWADA UTAJADILIWA
Wakati huo huo, Serikali imesisitiza kuwa haitauondoa bungeni muswada huo kwa kuwa kila kilichomo ndani yake kinazungumzika. Msimamo huo ulitolewa bungeni jana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu bungeni.
Pinda alikuwa akijibu swali la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe. Mbowe aliitaka serikali kuuondoa bungeni muswada huo kwa maelezo kwamba kama utaachwa ujadiliwe na wabunge na kupitishwa, utaleta ufa mkubwa kwa taifa kwa kuwa hauna tija.
“Jambo la Katiba si jepesi kama baadhi ya wabunge wenzagu (wa CCM) wanaopiga makofi wanavyotaka kuliona...Yapo maeneo mengi yasiyo na tija na kwa sababu tuna dhamira njema, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri serikali kuuondoa muswada huu ukafanyiwe kazi na kuuleta tena bungeni wenye maslahi kwa pande mbili za Muungano ili ujadiliwe,’’ alisema Mbowe.
Akijibu maswali hayo, Waziri Mkuu alisema Bunge hilo ndilo lilopewa mamlaka ya kutunga sheria na kuwa serikali inachokifanya ni kupeleka bungeni mapendekezo.
“Yanaweza kuwa ni mapendekezo ya marekebisho na mapendekezo hayo ndiyo maana yanapita katika hatua mbalimbali ikiwamo ya ushirikishwaji wa wananchi ama mikutano ya hadhara,’’ alisema.
“Matarajio ya wananchi wabunge tutaujadili muswada huu kikamilifu na maeneo yote yanayodhaniwa kuwa yanaweza kuwa hayana tija au neema kwa nchi yetu ni jukumu letu sisi wabunge kujadili kwa uwazi, uaminifu na kazi kubwa ya serikali katika mjadala ule ni kuangalia kuona mahali gani tulipitiwa hili tunalikubali na hatimaye tutafikia uamuzi wa pamoja,’’ alionmgeza Pinda.
KAMBI YA UPINZANI YATOA MSIMAMO
Katika hatua nyingine, upinzani umesema haitashiriki katika mjadala wa muswada huo utakaohitimishwa leo kwa kuwa CCM ina ajenda ya siri na kwamba misingi ya katiba imechakachuliwa, hivyo wakishiriki watakuwa wamewanyima haki wananchi.
Katika mkutano wa waandishi wa habari jana jioni, Mbowe ambaye aliongozana na Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohamed Habibu Mnyaa (na Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, alisema kuwa CCM walishaamua kuupitisha muswada huo kwa gharama yoyote.
Imeandikwa na Boniphace Luhanga; Beatrice Shayo, Dodoma na Salome Kitomari, Dar.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :