MWIDAU CUP KURINDIMA WILAYANI PANGANI MKOANI TANGA; ZAIDI YA MILIONI 20 KUTUMIKA
Posted in
No comments
Sunday, October 27, 2013
By
danielmjema.blogspot.com
Mbunge Amina Mwidau, akikagua timu huku akiwa na viongozi wa timu ya Black burn kabla ya mchezo kuanza. |
Mbunge Amina Mwidau, akikagua timu huku akiwa na viongozi wa timu ya Black burn kabla ya mchezo kuanza. |
Mgeni rasmi Amina Mwidau, akizindua mashindano ya soka ya Mwidau CUP kwa kupiga mpira. |
Mbunge Amina Mwidau akikabidhi jezi kwa nahodha wa timu ya soka ya wanawake ya Sawaka Sport Club, Monica Frank Mbaruk. |
Na Mwandishi Wetu,Tanga
MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga, Amina Mwidau kupitia
Chama cha Wananchi(CUF), amezindua rasmi
ligi ya Mwidau Cup inayoshirikisha timu 45 za Wilaya ya Pangani yenye kata 13
huku zaidi ya sh.milioni 20 zikitarajiwa kutumika hadi kumalika kwa ligi hiyo.
Kwa mujibu wa Mwidau lengo la mashindano hayo si kupata tu
mshindi kwa ajili ya kuchukua zawadi, bali anataka kuona vipaji vya soka
vinaibuliwa kwa kuwa soka ni ajira na wakati huo huohuwaunganisha wananchi
pamoja na hiyo ndio dhamira yake kwa Wilaya ya Pangani na Tanga kwa ujumla.
Akizungumza katika Uwanja wa Kumba Wilayani Pangani wakati
akizindua ligi hiyo, Mwidau alisisitiza umuhimu kwa timu ambazo zinashiriki kuonesha
uwezo wao wa kusakata soka na anatamani
kuona Wilaya ya Pangani inakuwa chachu katika maendeleo ya soka kwa mkoa wa
Tanga.
“Malengo yangu ni kuona tunapata vipaji vya soka kwa vijana
wetu maana uwezo wanao. Hivyo nimeamua kuanza na Wilaya ya Pangani kwa
kudhamini ligi hii nikiwa na maana ya kupata sehemu ya kuanzia katika
kuhakikisha Mkoa wa Tanga unakuwa na ligi ya aina hii,”alisema.
Alifafanua yeye ni mdau mkubwa kwenye michezo na amekuwa
akitoa vifaa vya michezo kwa timu za mpira wa miguu na mpira wa wanawake lakini
ni wakati muafaka wa kudhamini ligi na ndio maana ameamua kutoa sh.milioni 20
kuona michezo inapewa nafasi kwa kuwa na mashinano ya Mwidau CUP.
Akizungumzia zaidi kuhusu ligi ya Mwidau Cup, alisema kuwa
ametoa vifaa ya michezo kwa timu zote zinazoshiriki ligi hiyo na jumla ya
thamani yake kuanzia vifaa na mambo mengine ya udhamini jumla ya sh.milioni 20
zitatumika lakini jambo la msingi kwake kuona michezo ndani ya mkoa huu inapewa
kipaumbele.
Aliongeza kuwa yeye ni mbunge wa Mkoa wa Tanga , hivyo
anayo fura ya kushirikiana na wadau wa michezo katika kuleta maendeleo na
kuweka wazi historia inaonesha mkoa huo umekuwa maarufu katika michezo kutokana
na wachezaji wengi maarufu kutoka mkoani hapa.
Hata hivyo alisisitiza nidhamu kwa vijana katika suala la
michezo kwani, ndio njia pekee ya kufikia kwenye mafanikio na kwamba hata
katika suala la maendeleo ili liweze kufanikiwa linahitaji nguvu ya wananchi
kwa ujumla wao bila kujali itikadi za vyama vya siasa, hivyo mashindano hayo
yatawaunganisha katika burudani lakini pia katika kufanya kazi kwa ushirikiano.
Mwidau , mbali ya kutoa vifaa vya michezo kwa timu za mpira
wa miguu, pia alitumia nafasi hiyo kutoa vifaa vya michezo kwa timu ya mpira
wa Netball kwa Wilaya ya Pangani huku
akisisitiza kuwa amefanya hivyo kwenye maeneo mengine ya mkoa wa Tanga.
Katibu Msaidizi wa Chama cha Soka Wilaya ya Pangani,
Mohamed Swazi, alisema kuwa mashindano hayo yatakuwa chachu kwa vijana kutumia
muda mwingi kujihusisha na michezo huku akitumia nafasi hiyo kufafanua
changamoto iliyopo kwenye timu yao timu nyingi hazina vifaa vya michezo, lakini
kwa uamuzi wa mbunge wa Mwidau wanaamini wamepata mwanzo nzuri wa kuendeleza
michezo kwa kasi.
Ofisa Utamaduni wa Wilaya ya Pangani Kemmy Anatori, alisema
kuwa anatambua umuhimu wa michezo na kwa upande wake akiwa mwakilishi wa
Serikali anaunga mkono juhudi za Mwidau za kuhamasisha michezo kwenye wilaya
yake kwani faida ni nyingi kuliko hasara.
Kwa timu ambazo zimefungua pazia ya ligi hiyo, timu ya soka
ya BlackBurn imefanikiwa kuibuka mshindi baada ya kuibamiza timu ya soka ya
Nondo mabao 4-0.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :