WATAALAMU WAJIFUNGIA KILIMANJARO KUJADILI CHANGAMOTO DHIDI YA MALIASILI NA SWALA LA UJANGILI

Posted in
No comments
Wednesday, October 30, 2013 By danielmjema.blogspot.com


Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro
Dkt.Freddy Manongi-Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mweka

WATAALAMU wa maswala ya Uhifadhi na usimamizi wa Wanyama pori kutoka katika nchi zipatazo 20 wamekutana Mkoani Kilimanjaro katika Kongamano la kujadili mbinu za kukabiliana na Changamoto ya Ujangili inayohatarisha usalama wa Wanyama hasa Tembo na Faru.

Wataalamu hao kutoka katika nchi za Afrika, Ulaya na Amerika wanakutana kuangalia mbinu za kisasa za kukabiliana na Ujangili ambayo kwa sasa inaonekana kutia fora katika masoko mengi na ikidaiwa kuwa na Faida nzuri hasa katika bara la Mashariki ya Mbali.

Katika kongamano hilo la siku 5 linalofanyika katika chuo cha chuo cha Uhifadhi na usimamizi wa Wanyamapori (MWEKA), wilayani Moshi, mkoani Hapa, wadau hao kwa pamoja walikubaliana kuwepo kwa umuhimu wa kuangalia upya au kubadilisha mitaala ya kufundishia katika vyuo vya wanyapori kama njia ya kukabiliana na janga la ujangili duniani.

Sehemu ya wadau wa Uhifadhi wa Wanyapori kutoka katika nchi 20 duniani, wakifuatilia mafunzo katika Kongamano la kujadili changamoto na mbinu za kukabili ujangili duniani, iliyofanyika katika ukumbi wa chuo hicho leo kama sehemu ya Maadhimisho ya miaka 50 ya chuo cha Mweka.
Wakizungumza na Rai kwa nyakati tofauti, baadhi ya wataalamu waliohojiwa na gazeti hili, walisema kuna haja ya serikali, wafanyabishara na wananchi kuelimishwa juu ya madhara ya kuwakumbatia majangili huku wajkibainisha kuwa endapo uthubutu utakuwepo miongoni mwa wahusika wa udhibiti wa tatizo hili, vita dhidi ya ukatili huu utatokomezwa.

Akizungumzia swala la utoaji wa elimu sahihi, Mkuu wa chuo cha uhifadhi na usimamizi wa Wanyama pori Mkoani Kilimanjaro (Mweka), Dkt. Freddy Manongi alisema chuo chake kimeanza mikakati ya kuboresha mitaala inayotumika katika kuandaa maaskari na wataalamu wa uhifadhi wa Wanyapori kama njia ya kuwaongezea mbinu za kupambana na ujangili nchini.

Dkt. Manongi katika uzinduzi wa Kongamano ya siku tano inayoshirikisha wadau wa hifadhi ya Nyamapori kutoka nchi zaidi ya 20 duaniani, kujadili changamoto zinazokabili sekta hiyo pamoja na kujifunza mbinu mpya za kisasa za kukabiliana na ujangili.

“Katika kutafuta njia mwafakawa kukabiliana na Ujangili, hasa ukatili dhidi ya Tembo na Faru, chuo chetu kimeanza mchakato wa kupitia upya mtaala wetu na katika hilo tunafikiria kuibadilisha ili kutumia mtaalamu wa kisasa ambayo itatoa uwezo kwa Wahitimu wetu kupata mbinu za kisasa za kukabiliana na ujangili huo,” alisema Manongi

Dkt. Manongi alisema kwa sasa kutokana na changamoto kubwa la Ujangili ambalo linatishia usalama wa Wanyama hususan katika nchi za bara la afrika, chuo hicho kimejiwekea mikakati ili kujaribu kuwandaa wahitimu wa maswala ya uhifadhi wa wanyamapori ili kuwapa mbinu mipya ya kupambana na Majangili wanaohatarisha uhai wa Wanyama.

“Kuna tatizo la ujangili, tumeamua kuangalia upya mtaala wetu, kama mnavyofahamu sdwala la ujangili ni swala usiri mkubwa, ni vigumu kumbaini Jangili hivyo tunaangalia namna ya kuweza kuwapa wanafunzi wetu mbinu za kisasa za kupambana na Majangili hao,” alisema Manongi.


Alisema kwa sasa wameshaanza kushauriana na wenzao kuhusu technolojia ya Kisayansi (Forensic Science) ambayo inawezesha Askari na wataalamu wa msawala hayo kuwagundua majangili kupitia taarifa za vinasaba (DNA) kwa kupima damu za mnyama, alama za nyayo za majangili pamoja na alama za vidole vya majangili katika mwli wa mnyama aliyeuwawa na kama wataona inafaa kutumika wataingiza utaalamu huo katika mitaala mipya ya kufundishia.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Wanyapori nchini Kenya (KWS), Dkt. George Otiang alisema kuna haja ya kufanya gharama za vitendo vya ujangili kuwa kubwa kuliko faida zinazopatikana kutokana na vitendo hivyo kwani mazingira yaliyoko sasa hivi yanavutia kwa Ujangili.

Alisema ipo haja kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia upya Faini zinazotolewa kwa majangili kwani ni ndogo sana kuliko faida anayoipata Jangili jambo ambalo limesababisha Majangili kutojali kukamatwa.

Naye Mshiriki wa Kongamano hilo ambalo ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka Hamsini ya Chuo cha Mweka, Dkt. David Manyanza ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Chuo hicho, alisema Vita dhidi ya ujangili vinaonekana kuwa ngumu kutokana na usiri unaotumika katika biashara hiyo pamoja na kuwepo kwa mkono wa watu mashuhuri wakiwemo viongozi ndani ya serikali.

Alisema ikiwa kutakuwa na utashi wa dhati katika mapambano haya kutoka kwa wananchi wenyewe, serikali pamoja na wafanyabiashara, tatizo la ujangili unaweza ukatatulika lakini kama vita hiyo itaachwa mikononi mwa wizara tu kumaliza ujangili itakuwa ni ndoto.

“Tatizo la ujangili linaonekana kuwa kubwa kutokana utaratibu mbovu unaotumika kupambana nao, Serikali inawakumbatia majangili, ujangili sio sawa na biashara nyingine ambapo mtu atajitangaza hadharani, kuna haja ya kuweka wazi majina ya watuhumiwa bila kuangaliana  usoni, kama haya yatafanyika na wananchi na wanasiasa nao wakafahamu majukumu yao vita hivi tutavishinda, ” alisema Dkt. Manyanza.

Aidha Dkt. Manyanza aliwataka Wananchi kususia bidhaa zinazotengenezwa kutokana na pembe za ndovu, Faru pamoja na bidhaa nyingine kama vile ngozi zinazotokana na Wanayama ili kunusuru maliasili ya Nchi hii.

Kongamano hilo linafanyika kwa siku tano na kilele chake kitakuwa ni Novemba 2 katika Maadhimisho ya miaka 50 ya chuo cha Uhifadhi na usimamizi wa Wanyamapori mkoani Kilimanjaro Mweka, sherehe zitakazotanguliwa na Harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya maboresho ya majengo ya chuo hicho, itakayoongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Mwisho.


Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .