MAZUNGUMZO YA AMANI YA SYRIA HATIHATI KUVUNJIKA
Posted in
Kimataifa
No comments
Saturday, February 15, 2014
By
danielmjema.blogspot.com
Hatua za amani nchini Syria ambazo zinalegalega zimefikia hatua za
mkwamo kamili jna Ijumaa(14.02.2014) huku kukiwa na wasi wasi wa
kuvunjika kabisa licha ya mbinyo wa kimataifa.
Wakati huo huo nchini Syria kwenyewe idadi ya vifo inaongezeka. Katika siku ya mwisho ya duru hii ya mazungumzo ya amani yanayosimamiwa
na Umoja wa Mataifa , pande zinazopigana nchini Syria zinaonekana kuwa
mbali katika mtazamo wao kuliko wakati wowote ule, wakikubaliana tu
katika suala moja, ambalo ni kwamba mazungumzo hayo hayaelekei kokote.
"Tunasikitika sana kwamba duru hii ya mazungumzo haijapiga hatua,"
amesema naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Syria Faisal Muqdad, baada ya
kukutana na mpatanishi wa Umoja wa Mataifa Lakhdar Brahimi.
Kwa upande wao, msemaji wa upinzani Louay Safi amelalamika juu ya
kushindwa kwa serikali kuonesha ushirikiano, na kukiri kuwa " mazungumzo
yamefikia hatua ya mkwamo."
Duru ya mwisho
Umoja wa Mataifa umetangaza siku ya Ijumaa kuwa Brahimi amezialika pande
hizo mbili kurejea katika meza ya majadiliano kwa ajili ya duru ya
mwisho ya mkutano wao wa pamoja leo Jumamosi asubuhi.
Wakati pande hizo zimeshindwa kupata makubaliano mjini Geneva hata
katika ajenda zilizopo katika mazungumzo yao, idadi ya vifo ndani ya
Syria inaendelea kupanda.
Kundi linaloangalia hali nchini humo limesema siku ya Alhamis zaidi ya
watu 5,000 wameuwawa tangu duru ya kwanza ya mazungumzo kuanza Januari
22.Kiasi ya watu 47 wameuwawa siku ya Ijumaa katika shambulio la bomu
lililotegwa katika gari mbele ya msikiti kusini mwa kijiji
kinachodhibitiwa na waasi cha Yaduda, wakati kundi linalopambana kwa
nadharia ya jihad la ISIL limewauwa watu 27 wakati waasi hasimu
wakiwafukuza kutoka katika vijiji katika jimbo la kaskazini la Aleppo.
Na Umoja wa Mataifa umeonya siku ya Ijumaa kuwa zaidi ya wakimbizi 2,700
walimiminika katika mpaka na Lebanon wakati shambulizi la majeshi ya
serikali ya syria katika milima ya Qalemun likiendelea , na kusababisha
hali ya tahadhari hususan kwa upande wa mji unaoshikiliwa na upinzani wa
Yabrud , ukitarajia kushambuliwa na jeshi la aridhini la Syria.
Vifo zaidi
Maelfu ya watu tayari wameukimbia mji huo , lakini zaidi ya watu 50,000
wanaaminika kuwa bado wako katika mji huo. Marekani imeeleza
kukasirishwa kwake kutokana na shambulio la anga na kuzingirwa kwa mji
huo.
"Tunatoa wito tena kwa jumuiya ya kimataifa , ikiwa ni pamoja na
washirika wa Assad, kuueleza utawala huo kwamba ni lazima usitishe
mashambulizi haya yasiyo lazima ambayo yanavuruga hatua za mazungumzo ya
Geneva na matumaini ya amani nchini Syria," msemaji wa wizara ya mambo
ya kigeni ya Marekani Edgar Casquez amesema.
Mjini Geneva kulikuwa hakuna ishara ya hatua za maendeleo kuelekea
kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka mitatu
sasa na kuuwa zaidi ya watu 136,000 na kuwalazimisha mamilioni wengine
kukimbia nchi hiyo na wengine kukimbia makaazi yao.
Haifahamiki iwapo Brahimi ataweza kuzishawishi pande zinazohusika kurejea tena kwa ajili ya duru nyingine ya mazungumzo.Marekani , ambayo inaunga mkono upinzani na ambayo imeshawishi kuitishwa
kile kinachofahamika kama Geneva II pamoja na Urusi ambayo ni mshirika
wa utawala wa Syria , imeeleza fadhaa yake kutokana na kukwama kwa
mazungumzo hayo.
"Mazungumzo kwa ajili ya kujionesha tu hayana maana," Amesema afisa mwandamizi wa Marekani siku ya Ijumaa.Katika juhudi za kuweka uhai katika mazungumzo hayo, Marekani na Urusi
zimetuma wajumbe wa ngazi ya juu katika mazungumzo hayo ya Geneva wiki
hii kukutana na Brahimi pamoja na pande hizo mbili.
Lakini baada ya kukutana na wanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Marekani
na Urusi siku ya Alhamis, mpatanishi huyo amekiri kuwa " hali ya
kushindwa bado inatukodolea macho".
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :