LEMA AMJIBU RAIS KIKWETE , AMTAKA OCD ARUSHA AACHIE NGAZI
Posted in
Siasa
No comments
Friday, April 25, 2014
By
danielmjema.blogspot.com
Lema alimtaka OCD huyo kujitoa kwenye uongozi wa Jeshi la Polisi na
kwenda kufanya kazi ya uenezi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Lema alisema
Aprili 22 mwaka huu aliandika barua ya kuomba ulinzi kwenye mikutano
yake.
OCD huyo alifuta mikutano ya shughuli za mbunge huyo aliyoiruhusu kwa
kigezo kuwa alipokea maombi mengine ya CCM kufanya mkutano eneo
alilotaka kufanya mkutano.
Lema alisema Aprili 23 alipokea barua ya OCD ikimzuia kufanya mkutano
kwa hoja kwamba kuna tishio la usalama jijini Arusha kutokana na
mlipuko wa bomu uliotokea kwenye baa ya Arusha Night Park, hivyo
hawaruhusu mikusanyiko.
“Mimi ni mwakilishi wa wananchi wa Arusha, watu wangu wamepigwa
mabomu, nataka nizungumze nao niwatie moyo nazuiwa… wiki ijayo naenda
kwenye kikao cha Bunge la Bajeti, nataka niwasikilize wananituma
nikawasemee nini sipewi ruhusa, nataka nisikilize kero za wapiga kura
wangu OCD ananizuia.
“Hivi tukimaliza hapa kama madereva wanaogopa kuendesha gari
kutangaza mkutano, kazi hiyo nitaifanya mwenyewe, huu ni uhuni kwa
sababu kuna mikutano ya injili inaendelea, ibada zinafanywa makanisani
na misikitini, masoko ambayo ndiyo yenye mikusanyiko mikubwa inaendelea.
“Kumbi za starehe tena za usiku zinafanya kazi kama kawaida, hata
hapo palipopigwa bomu watu wanakusanyika, kwanini mkusanyiko wa mbunge
na wananchi wake ndiyo unaonekana kuhatarisha usalama?” alihoji Lema.
Alisema sheria ya kinga, haki na madaraka ya Bunge inamruhusu
kuzungumza na wananchi wake kwa uhuru, na yeyote atakayejaribu kumzuia
atatenda kosa na anapaswa kushitakiwa.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Leberatus Sabas, alipotakiwa kutolea
ufafanuzi suala hilo, alijibu kwa mkato: “Tayari tumeshalimaliza suala
hilo, tumeruhusu mikutano yake.”
Awali Aprili 17, mwaka huu, Lema alimwandikia barua OCD akiomba
kufanya mikutano ya wananchi kwa nafasi yake kama mbunge kwenye kata za
Levelosi, Terrat, Daraja Mbili na Moshono kwa tarehe tofauti.
Lema alisema kuwa siku hiyohiyo alipokea barua toka kwa OCD
akimruhusu kuendelea na mikutano yake, lakini katika hali isiyo ya
kawaida, Aprili 20, akapokea barua nyingine kutoka kwa kiongozi huyo wa
polisi akizuia mikutano hiyo kwa maelezo kuwa Aprili 19, mwaka huu CCM
nao wamepeleka barua wakiomba kufanya mikutano maeneo hayo jambo
wanaloona linaweza kusababisha uvunjivu wa amani.
Lema amjibu JK
Katika hatua nyingine, Lema amemtaka Rais Jakaya Kikwete aelewe kuwa
maandamano ya Jiji la Arusha husababishwa na watendaji wa serikali yake
kupindisha sheria na kuminya haki za umma, hivyo huwalazimu kuandamana
ili kuzidai.
Alisema kuwa hategemei kusifiwa na kiongozi huyo wa nchi katika
harakati zake za kupigania haki ya wananchi wake na siku ikitokea
anamsifu, itabidi ajitathmini ni wapi amekosea.
Lema alisema jambo la kusikitisha ni kuwa wale wanaohusika na
uvunjivu huo wa sheria na haki za binadamu ni kutoka ndani ya Jeshi la
Polisi, na wote wamepandishwa vyeo.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :