CHUMBA CHA UPASUAJI HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA KILIMANJARO (MAWENZI) KUKAMILIKA MWISHONI MWA MWEZI HUU.

Posted in
No comments
Sunday, July 6, 2014 By danielmjema.blogspot.com


Mwandishi wetu, Kilimanjaro
KITENDAWILI cha lini chumba cha upasuaji katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kilimanjaro (Mawenzi), itakamilika ujenzi wake na huduma za upasuaji kurejea kama kawaida katika Hospitali hiyo kuteguliwa mwishoni mwa mwizi huu, imeelezwa

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi (CCM) mkoani hapo, Iddi Juma katika kikao chake na waandishi wa Habari, kilichofanyika juzi, Ofisini kwake.

Ujenzi wa Chumba hicho kilichoanza mwishoni mwa mwaka 2004, kuchelewa kwa kukamilika kwake kumesababisha adha kubwa kwa wagonjwa kutoka ndani na nje ya mkoa huo, hususani Mama mjamzito na mtoto ambapo mara nyingi wagonjwa wanaohitaji  kufanyiwa upasuaji wamekuwa wakipelekwa katika Hosptili ya St. Joseph na Hospitali ya rufaa ya KCMC.

Katika kutegua kitendawili hicho Iddi Juma pamoja na baadhi ya viongozi wakuu wa CCM mkoani hapo walilazimika kufanya ziara Hospitalini hapo ikiwa ni baada ya wandhishi wa habri kuhoji ahadi yake aliyoitoa mwaka jana kuwa ujenzi wa chumb ahicho kingekamilika mwishoni mwa mwezi julai mwaka 2013.

Katika taarifa yake, Juma alisema baada ya kuonana na timu ya wataalamu kutoka katika Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa huo, Mganga mkuu wa mkoa pamoja na wataalamu waliopewa kandarasi ya kujenga Chumba hicho, wamemuahakikishia kuwa pamoja na changamoto zilizopo chumba hicho kitamalizika mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu.

Mwenyekiti huyo alisema aliamua kutembelea jengo hilo na kuona utekelezaji wake baada ya kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, kuhusiana na jengo hilo la upasuaji ambalo limechukua muda
mrefu kujengwa.

“Nimekutana na viongozi wa mkoa kwa maana ya RAS, mganga mkuu na mtaalamu anayejenga jingo hilo, sasa nitamka wazi kuwa tatizo hilo litamalizika mara baada ya kukamilika kwa jengo la upasuaji mwishoni mwa mwezi julai mwaka huu, kila kitu kinakwenda sawa, nimefika pale na nimeridhika,” alisema Juma.

Juma alisema kwa mujibu wa ripoti ya mkandarasi aliyepewa kazi ya ujenzi wa Chumba hicho ambacho kimejengwa katika awamu tatu, kwa gharama ya shilingi bilioni 1, 290, 416, 425, ukamilishwaji wake umechelewa kutokana na mabadiliko ya ghafla ya sera ambapo mwaka jana Hospitali hiyo ilipanda cheo na kuwa ya Rufaa hivyo ujenzi wa Chumba ukalazimika kuwa cha hadhi ya Hospitali ya Rufaa.

Taarifa hiyo ilisema sambamba na mabadiliko hayo, jengo hilo ambalo awali lilitolewa taarifa kwamba lingekamilika mapema mwezi julai mwaka jana, lilishindikana kukamilika kutokana na uagizwaji wa baadhi ya vifaa kutoka nje ya nchi ikiwemo taa na gesi kwa ajili ya upasuaji.

Changamoto nyingine iliyopelekea kutokamilika kwa jengo hilo ambalo awamu ya tatu ya ujenzi wake ilianza January 16, mwaka 2013, ilikuwa ni tatizo la upatikanaji wa wakandarasi wadogo.

Aidha alisema kuwa, kumekuwa na ongezeko la gharama za ujenzi ikiwa ni hatua ya kutaka jengo hilo liendane na hadhi ya Hospitali ya Rufaa kama ilivyoanishwa katika sera ya serikali ambapo awali bajeti ya jingo hilo pamoja na vifaa vyake ilikuwa ni shilingi bilioni 1,068, 255,941.

“Jengo la upasuaji sasa inatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa na kuanza huduma mwishoni mwa mwezi julai mwaka huu,ujenzi huu ulichelewa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuchelewa kwa vifaa vilivyokuwa vinaagizwa kutoka nje ya nchi, lakini kwa sasa tunawakikishia mwishoni mwa mwezi julay jengo lile litakabidhiwa na kuanza huduma” alisema Juma.

Hospitali hiyo ya mkoa  iliyopo mjini Moshi, haina huduma ya upasuaji kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, hali ambayo imetokana na wizara ya afya na ustawi wa jamii, kukifunga chumba cha upasuaji hospitalini hapo kwa kile kilichoelezwa kuwa  hakikidhi vigezo vya upasuaji vilivyowekwa na wizara ya Afya na ustawi wa Jamii.

Toka kufungwa kwa chumba hicho cha upasuaji, idadi kubwa ya wagonjwa waliohitaji huduma hiyo wamekuwa wakilazimika kutibiwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC na Hospitali ya St. Joseph za mjini Moshi, ambako ni gharama kubwa na wagonjwa wengi hususani wa kipato cha chini hushindwa kuzimudu.

Kukamilika kwa jengo la upasuaji kutakua mkombozi mkubwa kwa wananchi hususani wakina mama wajawazito, ambao sera ya afya inaelekeza watibiwe bure, lakini wamekuwa wakijikuta wakiingia gharama kubwa za upasuaji katika hospitali binafsi kutokana na kukosekana kwa huduma hiyo katika hospitali ya mkoa.
Mwisho.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .