Waraghabishi wakoleza kasi ya mabadiliko wilayani Kishapu
Posted in
Habari na Jicho Pevu la Kijiwe
No comments
Saturday, December 26, 2015
By
danielmjema.blogspot.com
Na Krantz Mwantepele ,Kishapu
Mabadiliko
katika jamii yoyote kwa kiasi kikubwa huchangiwa na ongezeo la mahitaji ya
binadamu katika mambo mbalimbali. Kwamba, kadri dunia inavyopitia mabadiliko,
kadiri ile ile changamoto, mahitaji na huduma katika jamii husika huongezeka.
Ili
kufikia malengo yanayotokana na misukumo na mageuzi yasiyokwepeka, binadamu
amelazimika kubuni mikakati mbalimbali ya maendeleo. Si hivyo tu, mabadiliko
haya yamemfungulia binadamu fursa ya uthubutu wa kujaribu mambo mbalimbali,
siyo tu kwa faida yake, bali jamii nzima inayomzunguka.
"Sikutegemea
kama siku moja katika maisha yangu nitapata wazo ambalo lingebadili na kushawishi
watu kuchukua hatua kwa mustakabali wa jamii.”
Hiyo
ni kauli ya mraghbishi Revocatus Richard ambaye pia, kitaaluma ni mwalimu katika
shule ya msingi Uchunga. Richard alitoa kauli hiyo baada ya kupitia mafunzo ya uraghbishi
na mwalimu mwenzake, Restusta Katobesi, ambao
baadaye kwa pamoja, walianzisha Kituo cha KIMAJU
(Kituo cha Maendeleo cha Jamii ya Uchunga) kwa kushirikiana na uongozi wa
kijiji na wananchi. Na hilo ndiyo lilifanya achaguliwe kuwa Mkurugenzi wa kituo
hicho.
Walimu
hao walikuwa miongoni mwa waraghbishi 30 walioshiriki mafunzo ya uraghbishi yaliyotolewa
mwezi Machi, mwaka 2012 wilayani Kishapu katika mkoa wa Shinyanga. Kutokana na
faida na maarifa waliyoyapata kwenye mafunzo hayo, walimu hao waliamua kuunda
umoja uliokuwa chachu ya kuanzishwa kituo hicho cha maendeleo.
Mwanazuoni
Sarah Earl, aliwahi kusema: "Maendeleo
ni watu na mazingira yao. Kwamba, kusingekuwa na maana iwapo barabara,
hospitali, shule na miradi mingine ya
maendeleo inayojengwa kwa ajili ya watu isingetumika."
Kwa mantiki
hiyo, miradi yote ya maendeleo, ikiwamo Chukua Hatua ni kwa ajili ya ustawi wa
maisha ya watu. Kwa kuwa kiini cha maendeleo ni watu. Shabaha kubwa ya mradi huu
wa Chukua Hatua ni kuhakikisha wananchi
(waraghbishi) wanajielewa na kujitambua katika
kutimiza majukumu yao na kupata haki zao zikiwamo huduma bora za kijamii
na kuhakikisha wananufaika na rasilimali
zao. Pia unawasaidia kuwawajibisha viongozi wao ili watimize majukumu yao ya kuhamasisha
maendeleo na kutatua shida za wananchi.
Mraghbishi
ni mwananchi anayeleta uhai mpya ndani ya jamii kwa kutambua matatizo na
kupendekeza njia sahihi za kuyatatua.Katika
kipindi cha miaka mitano ya mradi, zaidi ya waraghbishi 380 wameleta uhai
katika jamii zao, hususani kwenye vijiji vya mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Geita
na Arusha hasa katika wilaya ya Ngorongoro.
Tafsiri
ya uhai huu ni pamoja na kuwachukulia hatua viongozi wabadhirifu, watendaji
wabovu, kuandaa midahalo, kudai huduma bora za kijamii, kuibua na kufuatilia matatizo
mbalimbali katika vijiji vyao kama ambavyo waraghbishaji Richard na Katobesi
wamefanya.
Uraghbishi
Kijiji cha Uchunga
Baada ya
kupatiwa mafunzo ya uraghbishi, walimu hawa walirudi kijijini kwao wakiwa na
jukumu moja la kutambua changamoto zinazoikabili jamii yao na kupendekeza nini
kifanyike wakitumia nafasi na uwezo walio nao.
Kikubwa
walichoangalia ni mustakabali wa mtoto wa Kijiji cha Uchunga, kwa maana ya nafasi
ya mtoto, ikiwamo ya kufahamu huduma anazopata.Katika
kufikiria sehemu ya kuanzia na ili kumpa mtoto wa kike nafasi katika jamii,
hasa ya kuongoza, walianza na wanafunzi wa shule wanayofundisha, Uchunga.
“Nimepata
bahati ya kuwa mwalimu mkuu msaidizi mara kadhaa na nimetumia fursa hiyo kuleta
mabadiliko, nikianzia kubadilisha utaratibu wa kuchagua viongozi wa wanafunzi
katika shule yetu," alisema Richard na kuongeza:
"Kwanza
tulibadilisha wazo la Kaka Mkuu na badala yake tukasema tutakuwa na Kiranja
Mkuu, ili kutoa fursa kwa wanafunzi wa kike kushika nafasi za uongozi wa
wanafunzi."
Hadi
sasa chaguzi mbili za kidemokrasia za kuchagua viongozi wa wanafunzi
zimefanyika shuleni Uchunga Julai 2012 na Mei 2013.
Katika
kuhakikisha wanaendeleza mawazo hayo, waraghbishi hao walikuja na wazo la
kujenga kituo cha kujisomea. Walianza kuwatembelea wanafunzi wa Shule ya
Sekondari ya Kata ya Uchunga wanaoishi katika kijijini hapo.
Baadhi ya
wananchi na wajumbe wa Kituo cha Maendeleo cha Uchunga wakiwa mbele ya kituo
kabla hakijaezekwa na mabati.
Ili
kufikia malengo yao, waliomba ushirikiano, siyo tu kwa walengwa ambao ni
wanafunzi, bali kutoka kada zingine ndani ya jamii.
Akielezea
jinsi walivyoanza, mraghbishi Katobesi alisema:
“Tulikutana
na wanafunzi na kuunda umoja wa kikundi wa Wanafunzi wa Sekondari Uchunga
(UWASU). Kikundi hiki kiliamsha hamasa
kwa wanafunzi waliokukubali kujitolea kufanya kazi.”
Na
baadhi ya wanafunzi hao wametembelea shule nyingine na kuhamasisha wenzao kujitolea
kusaidia kazi mbalimbali kama kuchota maji na kuokota mawe kwa ajili ya ujenzi
wa jengo la kituo hicho cha kujisomea.
Ndani
ya jamii yoyote kuna mamlaka, hivyo ili malengo yao yatimie kuliwalazimu waraghbishaji
hao kupata ruhusa kutoka kwa walimu na aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji wakati
huo, Mahona Punguja.
“Baada
ya kutoka kwenye mafunzo yao, walikuja kuzungumza na mimi kuhusiana na mambo
waliyojifunza na jinsi watakavyoleta mabadiliko. Nilikubaliana nao na kuweka utaratibu
wa kuwashirikisha wazazi kama wadau muhimu na makundi mengine maalumu,” alisema
Punguja.
Makundi
maalumu ni pamoja na watumishi wa uma, kwa maana ya walimu na mtendaji wa kijiji
na kata, wazee maarufu, viongozi wa dini, vijana na wajumbe wa halmashauri ya
serikali ya kijiji. Waraghbishi hawa kwa ushirikiano na uliokuwa uongozi wa
serikali ya kijiji waliweza kukutana na makundi hayo ili kuwaelimisha kuhusu
wazo la kituo cha kujisomea. Baada ya kila kundi kukutana na waraghbishi,
uliitishwa mkutano wa pamoja wa kujadili jambo hilo na kamati ikaundwa ya kusimamia mchakato mzima. Kamati
hii ilichaguliwa kwa kila kundi kuwa na mwakilishi wake.
“Njia
ya kwanza ilikuwa ni kukusanya fedha, kisha kuwaomba wananchi kuchangia nguvu zao.
Kila mmoja kwa nafasi yake alijitolea. Wengine tulisomba mawe na kuchimba
msingi. Wanawake walileta vyakula kwa
ajili ya mafundi ambao nao walijitolea pia utaalamu wao bure”, anaelezea
Michael Butu, Mwenyekiti wa Kituo cha KIMAJU.
Wanajamii
waliohamasika waliombwa kuchangia kila mmoja Shilingi 10,000 za Kitanzania,
ingawa baadhi walitoa nusu ya mchango huo. Kila kitongoji kiliombwa kuchangia Shilingi
60,000. Michango hii ilikusanywa baada ya kuundwa kwa nguvu ya pamoja na
wenyeviti wa vitongoji. Kati ya vitongoji vitatu, viwili vilikamilisha ahadi
zao.
Harakati
hizi ziliwezesha wanajamii kujenga kituo hadi ngazi ya linta, kabla ya mlezi wa
kituo hicho, Charles Dida kutoa shilingi
355,000 kama mkopo kwa ajili ya kununua
mabati na mbao.
“Nilipoona
jengo letu linasuasua, niliamua kujitolea kufanikisha ujenzi. Niliamua
kumshirikisha mke wangu, ambaye aliunga mkono uamuzi wangu kwa kujua mafanikio
yatakayopatikana ni ya jamii nzima,” alisema Charles Dida.
Katika
hili tumejifunza mahusiano yaliyopo baina ya baba na mama katika kufanya
maamuzi ya pamoja. Ni tofauti na mfumo dume uliozoeleka katika jamiii ya
kisukuma. Na mpaka sasa kituo kimeweza kulipa kiasi cha Shilingi 110,000 na
hivyo bado kinadaiwa Shilingi 245,000.
Ili
kuhakikisha kituo kinaendelea kutoa huduma kwa watoto wa Uchunga wajumbe wa
kamati tendaji wanafanyakazi kwa kujitolea kwa kuwa wao kuwa sehemu ya jamii ya
wananchi wa kijiji cha Uchunga.
“Nilihamasika
baada ya kupendezwa na wazo la kuanzishwa kwa kituo hiki. Na siku nilipoombwa
kuwa sehemu ya kuleta mafanikio, nilikubali mara moja na kushiriki mikutano na
ratiba nyingine,” alifafanua katibu wa vijana, Bahati Juma.
Moja
ya majukumu aliyokabidhiwa ni huhakikisha kituo kinafunguliwa saa mbili asubuhi
na kufungwa saa 10 jioni. Kwa wastani, kituo kinahudumia wanafunzi 20 kwa siku.
Mbali
na katibu huyo, watendaji wengine ni pamoja na mkurugenzi, katibu, mhasibu, na
kamati tendaji chini ya mwenyekiti na mlezi wa Kituo. Nafasi hizi zote zina
wasaidizi isipokuwa ya mkurugenzi na mlezi.
Uongozi
huu ulipatikana kidemokrasia kwa kuchaguliwa kwenye mkutano mkuu wa kijiji.
Baada ya kupata uongozi walitengeneza katiba na kukisajili kituo chao. Kwa
mujibu wa katiba ya kituo hicho, uongozi unachaguliwa kila baada ya miaka
mitatu.
“Waasisi
wa kituo ndio waliopendekeza mfumo wa uongozi na baada ya hapo wakauwakilisha
kwenye mkutano mkuu wa kijiji. Kwa hiyo walioweza walishiriki. Na kila mtu
aliyeona anafaa kuwa sehemu ya uongozi wa kituo hicho alipendekeza jina lake
ama la mwenzake. Baada ya majina hayo kupatikana ndipo yalipigiwa kura na
kupata viongozi,” anafafanua mwenyekiti wa kituo, Michael Butu.
Tukiachilia
suala la uongozi, kuna utaratibu maalumu wa kuendesha kituo hicho. Kuna vijana
wanaohusika na kuhakikissha ofisi inafunguliwa ili kutoa huduma za kujisoma
bure, ikiwa ni mkakati wa kuhamasisha watu na kukifahamu kituo.
Huduma
za KIMAJU
Taasisi
hii ya kijamii kwa kiasi kikubwa imelenga kwenye uzalishaji maarifa kwa kutoa
huduma ya maktaba, ambayo wanafunzi wanaoishi kijiji cha Uchunga hutumia kusoma
na kufanya kazi za nyumbani baada ya masomo shuleni.
Katika
ziara za ufuatiliaji na uwezeshaji, wafanyakazi wa shirika mtendaji la TAMASHA
katika mradi huo wa Chukua Hatua, walishauri kituo kupanua wigo wa huduma zake,
kama anavyoelezea Afisa Mradi Winston Churchill.
“Tuliwashauri
kuwalenga pia vijana walio nje ya shule ili kuwawezesha vijana wote kutumia
kituo hicho vizuri kijijini hapo.”
Watu
wazima pia wanatumia kituo hicho kujisomea magazeti, ambayo huwa ni ya siku
nyingi na hii ndio sababu ya umuhimu wa kutafuta redio ili watu wasikilize
taarifa za habari.
Hali
hii imehamasisha wanafunzi wa shule za sekondari na msingi kuja kujisomea, kama
anavyoelezea mwanafunzi wa darasa la saba Leticia Isaka kutoka Shule ya Msingi Uchunga,
“Kituo
kinanisaidia kutambua mambo mbalimbali, kwa mfano kupitia mafunzo ya hapa,
napata malezi bora ya kuniandaa niwe mwalimu au daktari. Lakini si hivyo tu, wakati
wa mapumziko ya saa sita huwa tunakuja kujisomea hapa baada ya kupatiwa mazoezi
na walimu shuleni,”
Pamoja
na sababu nyingine, uwepo wa kituo hiki umechangia kuongezeka kwa kiwango cha
ufaulu katika shule ya sekondari ya kata ya Uchunga, ambapo mwaka 2013 jumla ya
wanafunzi .... tu ndio waliofaulu katika ngazi
ya ... , wakati mwaka uliofuata waliongezeka na kufikia kiasi cha ...
"Mbali
na mafanikio haya, kituo kina changamoto kadhaa ikiwamo ukosefu wa meza, viti
na makabati ya kuhifadhia vitabu," anasema mkurugenzi wa kituo, Richard na
kuongeza:
“Haya
mabenchi na meza tumeazima kanisani na tukimaliza tunarudisha sehemu husika.
Hatuna vitabu vya mitaala kwa ajili ya wanafunzi wetu, ingawa eneo la kujisomea
lipo vizuri, nishati ya umeme nayo ni shida.”
Kimsingi,
wanajamii wa Uchunga kwa kushirikiana na waraghbishi na uongozi kwa kijiji
wamefanikiwa kufikia malengo.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :