YALIYOJIRI: TRUMP AMSHUKIA PAPA FRANCIS
Posted in
Jukwaa la Habari
No comments
Monday, February 22, 2016
By
danielmjema.blogspot.com
BILIONEA anayewania kuteuliwa na Chama cha Republican kuwania urais nchini Marekani, Donald Trump, amemkosoa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis na kusema ni aibu kwa kiongozi huyo wa dini kuhoji imani yake.
Kauli ya Trump imekuja siku chache baada ya Papa kukosoa kauli yake ya kwamba atajenga ukuta kutenganisha Marekani na Mexico na kusema kuwa “mtu anayeweza kujenga ukuta kutenganisha watu badala ya kujenga daraja si Mkristo.”
Papa alitoa kauli hiyo wakati akimalizia ziara yake nchini Mexico ambako alisema kauli yake hailengi kuwashawishi watu wasimpigie au kumpigia kura mgombea huyo ambaye amekuwa na kauli zinazozua gumzo mara kwa mara.
Trump alimjibu Papa na kudai kuwa; “Kiongozi hususani wa dini ni aibu kuhoji imani ya mtu,” alisema na kuongeza kuwa pamoja na kauli hiyo yeye hajali na kwamba haikuwa ya Papa binafsi bali ilichagizwa na Serikali ya Mexico.
Pia watu kadhaa wakiwemo mahasimu wa kisiasa wa Trump wameonyesha kupinga kauli ya Papa huku wengine wakiwa hawaamini kama Papa anaweza kutoa kauli hiyo.
Mpinzani wake katika kinyang’anyiro cha awali Seneta Marco Rubio, alisema hataki kuzungumzia suala hilo hadi atakaposoma maoni yote ya Papa.
Hata hivyo, aliongeza kuwa Marekani ina haki na wajibu wa kutekeleza sheria zake za uhamiaji.
“Hili ni taifa huru na tuna haki ya kudhibiti anayekuja, muda anaokuja na namna anavyokuja,” The Guardian ilimnukuu Rubio akiwa South Carolina.
“Mji wa Vatican unadhibiti wanaoingia, muda wanaoingia na namna wanavyoingia na kwa hivyo Marekani nayo ina haki ya kufanya hivyo.”
Hata hivyo, Rubio ambaye ni Mkatoliki alisema anaamini na kumheshimu Papa kama mrithi wa Mtume Petro.
Mpinzani mwingine wa Trump ambaye alibadili dhehebu na kuwa Mkatoliki na aliyekuwa Gavana wa Florida, Jeb Bush, alimwambia mwandishi wa Guardian kuwa: “Ukristo ni kati yake na muumba wake.”
Akizungumzia kauli ya Papa alisema haelewi inamaanisha nini lakini yeye binafsi anaunga mkono suala la kujenga ukuta na fensi pale panapohitajika.
“Nafikiri ni sahihi nikiwa kama Mkatoliki nipewe maelekezo ya Ukatoliki kutoka kwa Papa, lakini si kwenye mambo ya uchumi au mazingira,” alisema Bush.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :