ZANZIBAR: KUELEKEA UCHAGUZI WA JUMAPILI, WANAHABARI WATIWA KASHIKASHI
HALI ya kisiasa visiwani Zanzibar imezidi kuwa tete baada ya vyama
viwili vyenye wanachama na wafuasi wengi kutangaza kutovumiliana. Vyama hivyo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF)
kwa nyakati tofauti wiki hii vimetangaza kujibu mapigo katika matukio ya
aina yoyote yenye mwelekeo wa kusababisha vurugu dhidi ya wanachama au
wafuasi wao ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara kipindi hiki cha
kuelekea uchaguzi mkuu wa marudio.
Kwa mujibu wa Taarifa iliyochapishwa leo na Gazeti la MTANZANIA, sambamba na hali tete kati ya vyama hivyo, vyombo vya ulinzi na usalama visiwani Zanzibar jana
vilimkamata mpiga picha wa Gazeti hili, Silivan Kiwale, wakati
akitekeleza majukumu yake ya kikazi na kumwamuru kufuta picha zote
alizokuwa amepiga katika eneo la bandari ya Zanzibar.
Kiwale alitiwa nguvuni wakati akipiga picha katika eneo la bandari ya
Zanzibar na kuamuriwa na wana usalama hao kufuta picha zote alizokuwa
amepiga katika eneo hilo kisha akapewa tahadhari ya kuwa makini na
nyendo zake wakati wote atakaokuwa visiwani humo.
Baada ya kufuta picha hizo na kuachiwa, Kiwale alijikuta akikamatwa
kwa mara ya pili wakati akifuatilia kitambulisho maalumu cha kazi
kinachotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ambapo baada ya
kuhojiwa aliachiwa.
Katika tukio jingine mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji la
Ujerumani na Mwakilishi wa Gazeti la Mwananchi visiwani Zanzibar, Salma
Said, jana alikamatwa na maofisa usalama akiwa katika uwanja wa ndege wa
Zanzibar.
Salma alikamatwa saa 08:05 mchana muda mfupi kabla ya kuanza safari ya kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu. Akizungumzia tukio hilo, mume wa mwandishi huyo aliyejitambulisha kwa
jina la Ali, alisema wakati ndege ndogo aliyokuwa akitarajiwa kusafiri
nayo Salma aina ya Auric ikijiandaa kuruka, abiria walitangaziwa kwamba
ndege hiyo itasubiri kwa muda kabla ya maofisa usalama kuingia na
kumkamata.
“Ndege imecheleweshwa karibu nusu saa, abiria wakaelezwa ndege
inasubiri kwanza na ndipo walipokuja polisi na kumchukua,” alisema Ali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis, alipoulizwa
kuhusu kukamatwa kwa mwandishi huyo alisema hana taarifa hizo. Salma amekamatwa ikiwa ni siku chache tu baada ya Mkurugenzi wa
Makosa ya Jinai Zanzibar, Salum Msangi, kutoa kauli kwamba polisi ina
orodha ya watu 31 wakiwamo waandishi wa habari ambao itawaita kwa
kuwahoji kuhusiana na matukio mbalimbali yanayoendelea visiwani Zanzibar
yakiwamo ya ulipuaji wa mabomu katika sehemu mbalimbali za Unguja na
Pemba.
Tayari polisi wamekwishawahoji Mkuu wa Mikakati wa CUF, Eddy Riyami
na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho kwa upande wa Zanzibar, Nassor
Mazrui, huku wakiendelea kumshikilia Kaimu Mkurugenzi wa Habari,
Mawasiliano ya Umma wa CUF, Hamad Masoud.
TAMKO LA UMOJA WA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA JUU YA KUTEKWA KWA MWANDISHI WA HABARI WA SAUTI YA UJERUMANI ( DW ) SALMA SAID.
Salma Said mwandishi wa DW Zanzibar ametoweka baada ya kutekwa na watu ambao hawajafahamika jijini Dar es salaam, hali ambayo imeleta fadhaa na mshtuko kwa waandishi, jamii na familia yake hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa marejeo Zanzibar.
Ifahamike kuwa Kazi ya mwandishi wa habari ni kutoa habari juu ya kila kinachoendelea katika jamii , hivyo kama kuna dosari , dosari hiyo ni ya jamii na sio ya anayeieleza dosari .
UTPC inalaani na kupinga utekaji uliofanywa ambao sababu zake bado hazijulikani, hivyo tunaitaka serikali kuhakikisha Salma Said anatafutwa, kupatikana na anaachiwa huru mara moja kwa kuwa Serikali ndio yenye jukumu la kulinda raia wake.
Kama utekwaji wa Salma umefanywa kutokana na kazi yake ya uandishi habari tunalaani vikali hatua hiyo, vitendo hivi havipaswi kuendelea katika nchi inayoheshimu misingi haki na Demokrasia, Vitendo vya namna hii vinadumaza na kufifisha uhuru wa habari .
Tunapinga kwa nguvu zetu zote waandishi wa habari kukamatwa na vyombo vya dola au makundi ya kihalifu kwa visingizio ama vya uchochezi au maslahi ya taifa. Waandishi tutaendelea kufanya kazi zetu bila kujali vitisho vya aina yoyote ile kutoka kwa mtu yoyote au Serikali.
Imetolewa na
DEOGRATIUS NSOKOLO
RAIS WA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA -UTPC.
March 19, 2016.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :