Ujerumani yamtafuta mshukiwa raia wa Tunisia

Posted in
No comments
Thursday, December 22, 2016 By danielmjema.blogspot.com

Rais wa Ujerumani, Joachim Gauck
Polisi wanamtafuta raia wa Tunisia anayeshukiwa kuhusika katika shambulizi kwenye soko la Krismasi mjini Berlin. Mshukiwa huyo anafahamika kwa vyombo vya usalama kama gaidi ambaye ombi lake la uhamiaji lilicheleweshwa.

Shirika la habari la Ujerumani, dpa, limemtaja mshukiwa huyo kuwa ni Anis A, likizinukuu duru za usalama. Mshukiwa huyo anachukuliwa na idara ya ujasusi ya Ujerumani kama mtu hatari ambaye yuko tayari kufanya vitendo vya kigaidi wakati wowote.
Gazeti la Allgemeine Zeitung limeripoti kuwa hati za uhamiaji za raia huyo wa Tunisia mwenye umri wa miaka 21 zilipatikana ndani ya lori lililotumika kufanyia shambulizi hilo na anafahamika na maafisa wa usalama kwa kuhusika katika makosa mengine matatu.
Duru nyingine ya usalama imeliambia shirika la dpa kwamba polisi wameanza operesheni inayohusiana na shambulizi hilo katika jimbo la North Rhine Westphalia, magharibi ya Ujerumani. Gazeti la Ujerumani, Bild, limeripoti kwamba mtu huyo amesajiliwa katika mji wa Cleves, mji mdogo katika jimbo hilo katika mpaka na Uholanzi. Waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la North Rhine Westphalia amesema mshukiwa aliishi Berlin kuanzia Februari mwaka huu.
Serikali yathibitisha
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere, alithibitisha kuwepo kwa mshukiwa mpya. "Kuna mshukiwa mpya na anatafutwa. Ningependa kusema, kama wengine wote walivyosema: Huyu ni mshukiwa tu na sio lazima awe muhusika aliyefanya shambulizi. Uchunguzi ungali unaendelea katika kila upande. Kila kitu kinachunguzwa na mshukiwa huyu amekuwa katika orodha ya watu wanaotafutwa tangu usiku wa kuamkia leo."
Hata hivyo waziri de Maiziere amekataa kuthibitisha mara moja taarifa kadhaa za vyombo vya habari kwamba mshukiwa huyo ni mhamiaji kutoka Tunisia mwenye mafungamano na makundi yenye misimamo mikali ya kidini.  De Maiziere na mkuu wa idara ya ujasusi Hans-Georg Maassen wamefanya mazungumzo kuhusu hatua za kiusalama kufuatia shambulizi hilo katika kikao cha dharura cha kamati ya bunge inayoshughulikia masuala ya ndani.
Wakati haya yakiarifiwa, rais wa Ujerumani Joachim Gauck aliwatembelea baadhi ya wahanga wa shambulizi la Jumatatu katika hospitali ya Charite mjini Berlin. Gauck alisema amefaulu kukutana na mwanamume aliyeangukiwa na mlingoti alipokuwa akimsaidia mtu mwingine aliyejeruhiwa.
Rais Gauck alisema, "Ziara yangu ni ishara kwamba mamilioni ya watu nchini kote wanafuatilia kujua hatma ya wahanga na wale walio katika hali mahututi, pamoja na wale wenye nafasi nzuri ya kupona kabisa. Wasihisi wako peke yao na kwamba mbali na madaktari hapa, watu kote Ujerumani wana matumaini na wanawasubiri wapone."
Soko la Krismasi lililoshambuliwa linatarajiwa kufunguliwa LEO Alhamisi.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .