NIMEIKUTA KWENYE WALL YA MNYIKA NIMEIPENDA NA MARAFIKI ZANGU MSOME
Posted in
No comments
Saturday, June 30, 2012
By
danielmjema.blogspot.com
INAKUHUSU SANA UWE KWENYE NDOA AU LA, SOMA
Inahuzunisha lakini kuna fundisho kuu kwetu sote.
“Nilipofika nyumbani usiku ule, mke wangu aliponitayarishia chakula,
nilimshika mkono na kumwambia, Kuna kitu nataka nikwambie. Mke wangu
alikaa chini na kula chakula kimya akiwa tayari kunisikiliza. Tena
nikagundua macho yake yalionyesha anaumizwa. Nilishindwa hata namna ya
kuanza kufumbua kinywa changu. Lakini ilibidi nimwambie ili ajue
nilikuwa nikifikiri nini juu yake.
Nataka kukupa talaka.
Nilianza kusema kwa utulivu. Alionekana kutokereka na maneno yangu
badala yake aliniuliza kwa sauti ya upole ‘kwa nini?’ Sikumjibu swali
lake. Kutojibu kulimfanya akasirike. Akatupa kijiko na akanikaripia,
‘wewe si mwanamume!’ Usiku ule, hakukuwa na maongezi kati yetu. Alikuwa
akilia kwa kwikwi. Nilifahamu kwamba alitaka kujua ni nini kimetokea
kwenye ndoa yetu. Lakini kwa hakika nisingeweza kumpa jibu wala sababu
ya kuridhisha; alionekana si mali kitu kwangu penzi langu lilihamia kwa
Jane. Sikumpenda tena mke wangu mawazo yote yalikuwa kwa Jane. Kwa kweli
nilimdharau mke wangu!
Huku moyo wangu ukijua wazi kwamba
nafanya kosa, niliandika talaka ambayo ilionyesha kwamba yeye (mke
wangu) angepata nyumba yetu, gari na atakuwa na hisa 30% ya kampuni
yetu. Aliangalia talaka ile na kuichana vipande vipande.
Mke
ambaye tumeishi nami kwa miaka 10 alionekana mgeni machoni mwangu.
Nilimuonea huruma kwa muda, rasilimali na nguvu alizopoteza lakini
sikuweza kurudi nyuma kwa sababu Jane aliuteka moyo wangu kisawasawa.
Hatimaye mke wangu alilia kwa sauti mbele yangu, jambo ambalo kwa hakika
nilitarajia. Kwangu mimi kilio chake kilinipa nafuu.
Wazo la kuachana na mke wangu limenisumbua kwa majuma kadhaa na sasa limeendelea kuimarika na kuwa jambo la hakika zaidi.
Siku iliyofuata nilikuja nyumbani kwa kuchelewa sana nikakuta mke wangu
akiandika jambo mezani. Sikutamani hata kula chakula alichonipikia
nilikwenda moja kwa moja chumbani na usingizi ulinichukua mara moja kwa
sababu nilikuwa nimechoka baada ya kula raha za kufa mtu na Jane.
Usiku nilishtuka usingizini mke wangu alikuwa bado akiandika. Sikujali
kabisa nikajifunika vyema shuka na kulala tena. Asubuhi yake
alinikabidhi masharti ya talaka yake: hakutaka kitu chochote kutoka
kwangu lakini alihitaji apate angalau mwezi mmoja wa kujiandaa kabla
hajaachika. Akaomba kwamba katika kipindi hicho cha mwezi mmoja sote
mimi na yeye tujitahidi kuishi maisha ya upendo au kawaida kwa kadiri
itakavyowezekana. Sababu yake ilikuwa ndogo lakini muhimu: mwanetu wa
kiume alikuwa akikaribia kufanya mtihani katika mwezi uliofuata kwa hiyo
hakupenda mtoto aathirike kisaikolojia kwa sababu ya kuachana kwetu.
Hili halikuwa tatizo kwangu, nilikubali mpango wake. Lakini alikuwa na
sharti la ziada, aliniomba nikumbuke jinsi nilivyombeba siku za fungate
yetu hasa siku ya harusi yetu. Akaniomba na kunisihi kwamba katika
kipindi hicho cha mwezi mmoja niwe nambeba kutoka kitandani kwetu mpaka
mlango wa kutokea kila asubuhi. Nilidhani anakaribia kuwa kichaa. Ili
kufanya siku zetu za mwisho zisiwe na migogoro nilikubaliana na masharti
yake ya ajabu.
Nilimsimulia Jane kuhusu masharti ya kuachana
na mke wangu. Jane alicheka sana, aliona ni ujinga. ‘Hata akitumia
ujanja wa namna gani talaka ni lazima’, alisema Jane tena kwa dharau.
Mimi na mke wangu hatukuwahi kugusana tangu nilipomweleza dhamira ya
kumtaliki. Kwa hiyo nilipombeba kwa mara ya kwanza sote tulinuniana.
Mwanetu alifurahi sana na kupiga makofi nyuma yetu, ‘aah baba kambeba
mama mikononi mwake’. Maneno yake yalinichoma moyoni moja kwa moja.
Kutoka chumbani kwetu hadi sebuleni, halafu tena mpaka mlangoni, ni
zaidi ya mita kumi nimembeba mke wangu. Alifumba macho na kusema kwa
sauti laini na ya upole; usimwambie mwanetu juu ya talaka. Nilikubali
kwa kichwa, ingawa nilijisikia vibaya. Nilimuweka chini nje ya nyumba.
Alienda kituoni kusubiri basi la kazini kwake nami nikaendesha gari
kwenda ofisini kwangu. Siku ya pili, zoezi lilikuwa rahisi kwetu sote.
Aliegemea kifuani pangu. Nilisikia harufu nzuri ya uturi aliofukiza
kwenye blauzi yake. Nikagundua kwamba sijamuangalia kwa makini mke wangu
kwa kipindi kirefu sana. Nikagundua hakuwa binti tena. Kulikuwa na
mikunjo usoni na nywele zake zilianza kuwa nyeupe! Ndoa yetu imekula
urembo wake. Kwa dakika moja nikafikiri kwa nini namfanyia hivi.
Siku ya nne nilipombeba hisia za mapenzi kati yetu zilirejea. Huyu ni
mwanamke aliyejitoa kuishi nami na tumeishi kwa miaka kumi sasa. Siku ya
tano na ya sita ilikuwa wazi kwamba mapenzi yetu yalikuwa yakimea upya.
Sikumwambia Jane kuhusu jambo hili. Kadiri mwezi ulivyokaribia kwisha
niliona raha kumbeba mke wangu na zoezi likawa rahisi zaidi. Pengine
kufanya kazi hii kila siku kuliniimarisha zaidi.
Alikuwa
akichagua nini cha kuvaa asubuhi. Alichagua mavazi kadhaa hakupata
linalomfaa. Kisha akaguna, ‘nguo zangu zote zimekuwa kubwa’. Nikagundua
kwamba mke wangu amepungua sana, nadhani ndiyo maana niliweza kumbeba
kirahisi. Ghafla jambo likanichoma... mke wangu ana uchungu na maumivu
makuu moyoni mwake. Bila kujitambua nikamgusa kichwa chake. Mara mtoto
wetu akatokeza na kusema ‘baba ni wakati wa kumbeba mama muende kazini’.
Kwake kumuona baba akimbeba mama likawa ni jambo la furaha sana. Mke
wangu alimuonyesha ishara mwanetu asogee karibu na akamkumbatia kwa
upendo mkuu. Niligeuza uso wangu nisije nikabadili mawazo katika dakika
ya mwisho. Kisha nikambeba mikononi mwangu kutoka chumbani, sebuleni
halafu mpaka mlangoni. Mkono wake laini ulikuwa umeizunguka shingo yangu
kwa upendo. Nilimkumbatia mwili wake; ilikuwa ni mithili ya siku ya
ndoa yetu. Lakini wepesi wake ulinitia mashaka.
Siku ya mwisho
nilipombeba nilipata shida hata kupiga hatua moja. Mtoto wetu
alishakwenda shuleni. Nilimshika kwa karibu na kumwambia sikubaini
kwamba maisha yetu yalikosa upendo. Nikaenda zangu ofisini…. Nikashuka
garini hata bila kufunga mlango. Maana nilihisi nikichelewa tu ninaweza
kubadili nilichoamua.... nikapand ngazi. Jane alifungua mlango
nikamwambia, ‘Samahani, Jane, sihitaji tena kumtaliki mke wangu’.
Akaniangalia kwa kustaajabu, halafu akagusa kichwa changu. Akaniuliza
‘Unaumwa?’ Nikaondoa mkono wake kichwani kwangu. ‘Samahani, Jane,
nimesema sitaki kumtaliki mke wangu. Nadhani ndoa yangu haikuwa na
furaha kwa sababu sikuthamini undani wa maisha yetu, mimi na mke wangu,
si kwamba hatupendani. Nimetambua hilo tangu nilipombeba siku ya ndoa
yetu nilitakiwa kumbeba siku zote za maisha yetu, nampenda mke wangu
sitamuacha mpaka kifo kitakapotutenganisha.’
Ikawa kama Jane
alizinduka usingizini. Akanizaba kibao cha nguvu, akajiegemeza mlangoni
na kuanza kulia. Nikashuka ngazi na kuondoka zangu. Nikaingia kwenye
duka la maua nikaagiza maua mengi mazuri kwa ajili ya mke wangu. Muuzaji
akaniuliza aandike nini kwenye kadi. Nikatabasamu na kuandika
“Nitakubeba kila asubuhi mke wangu mpaka kifo kitakapotutenganisha”.
Jioni ile nilifika nyumbani na maua mikononi mwangu, tabasamu kubwa
usoni nikakimbia mpaka chumbani, nikapokelewa na maiti ya mke wangu
kitandani.
Kumbe mke wangu alikuwa akisumbuliwa na saratani kwa
miezi kadhaa nami nilishindwa kubaini kwa sababu nilihamishia akili
yangu kwa Jane. Alijua kwamba angekufa karibuni na alitaka asiniingize
katika chuki na mwanetu kama ningelazimisha talaka mapema.
Angalau machoni mwa mwanangu naonekana ni mume mwema….
Jamani vitu vidogo vidogo vizuri ni vya msingi sana katika mahusiano
yetu... Siyo majumba au magari au fedha zilizoko kwenye benki. Hivi
vitakupa tu mazingira ya kufurahi lakini vyenyewe siyo furaha. Kwa hiyo
jitahidi kuwa na muda mzuri na mazingira rafiki ya kuwa na mwenzi wako,
kuwa rafiki wa mwenzi wako. Fanya vitu mlivyofanya wakati wa uchumba na
wa ndoa yenue ambavyo vitawaweka karibu siku zote. Muwe na ndoa yenye
furaha. Mara nyingi watu hushindwa katika ndoa kwa kutotambua ni kwa
kiasi gani walikuwa karibu wakati wa kujenga uhusiano wao
Mungu awabariki nyote mliosoma na kujifunza hapa.
salome kitomari via facebook.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :