AKIBOA WASITISHA MGOMO MOSHI NA ARUSHA

Posted in
No comments
Tuesday, July 10, 2012 By danielmjema.blogspot.com


MGOMO wa  magari ya abiria uliotikisa miji ya Moshi na Arusha  kwa takribani siku nne mfululizo  umepata kufumbuzi kutoka kwa chama  cha  usafirishaji kanda ya kasikazini (AKIBOA) walipotangaza rasmi  mgomo umesitishwa.
 
Tamko la kusitishwa kwa mgomo huo lilitolewa kwa madereva wote wa mjini moshi na mwenyekiti wa chama cha usafiri wa kanda, (AKIBOA) Hussein Mrindoko likiwataka kurudisha magari yao kituoni hapo na kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

Akizungumza kijiweblog  kwa njia ya simu, Mrindoko alisema wamefikia hatua hiyo mara baada ya kufanya kikao na kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro na kukubaliana kusitisha mgomo na kuongeza kuwa ushuru utakaotumika  kwa sasa ni ule wa zamani.

 Akithibitisha kupokea taarifa za kusitishwa kwa mgomo zikimtaka kuingiza magari kituoni, mwenyekiti wa madereva wa Moshi na Arusha, Damian Barongo, alisema kuwa alipigiwa simu na mwenyekiti wa AKIBOA, Husseini Mrindoko ikimtaka kutoa taarifa kwa madereva kwamba mgomo umesitishwa.

“Nimepigiwa simu na msimazi wa kituo kunijulisha kwamba magari yameeingia kituoni na nilipomtafuta Bw. Mrindoko ambaye ndiyo mwenyekiti wa AKIBOA alilithibitisha na kunitaka kutoa tangazo kwa madereva wote kwamba ushuru ni ule wa zamani,” alisema Barongo.

Wakati hayo yakiendelea kijiweblog kilikuta magari yakiruhusiwa  kupita bila ya kutozwa ushuru wowote na lilipotaka kupata maelezo kutoka kwa wakala wa ushuru katika kituo cha mabasi Moshi, mmoja wa wawakilishi wa wakala huyo, Pinacle prod. Ltd, Emmanuel kinga alisema wao kama wakala wanasubiri kupata maelekezo kutoka kwa mwajiri wao ambaye ni Manispaa.

Kwa upande wao Kaimu mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Ibrahim Msengi na kaimu mkurugenzi wa manispaa ya moshi walipoulizwa kuhusu makubaliano ya kutumika kwa ushuru wa zamani walisema hawana taarifa yoyote kuhusu mabadiliko hayo.

Msengi alisema,  serikali bado inaendelea kusisitiza kwamba ushuru unaotambulika ni ule uliotangazwa kutumika kuanzia tarehe 01 julai mwaka huu na kuongeza kuwa sheria hiyo haijabatilishwa ila mazungumzo bado yanaendelea kupata mwafaka.

Nao baadhi ya abira waliokutwa kituoni hapo walionesha kufurahishwa na kuushukuru uongozi wa AKIBOA, kwa kitendo cha kusitisha mgomo huo na kushauri kuwa kama kuna madai yoyote ambayo hayajafikiwa basi yafanywe kwa njia ya majadiliano na sio migomo.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .