Dk. Migiro: Nina siri nzito kugombea urais 2015!

Posted in
No comments
Tuesday, July 10, 2012 By danielmjema.blogspot.com

ALIYEKUWA Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Dk. Asha Rose Migiro, amesema suala la yeye kugombea urais mwaka 2015 ni siri yake moyoni.
Dk. Migiro, alitoa kauli hiyo kwa mara ya kwanza jana, baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, mjini Dar es Salaam, akitokea nchini Marekani.

Itakumbukwa kipindi kirefu Dk. Migiro, amekuwa mmoja wa watu mashuhuri ambao wanahusishwa na mbio za urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), mwaka 2015.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Dk. Migiro alisema suala hilo litabaki kuwa siri yake moyoni, kwa kuwa hivi sasa Rais Jakaya Kikwete bado yupo madarakani.

“Hivi sasa tunajua Tanzania, inaongozwa na Rais Kikwete… hakuna tena mtu mwingine, hivyo si vizuri kusema ninahitaji kugombea nafasi hiyo wakati muda bado, tuwe na subira.

“Mimi leo (jana) nimerejea nchini, nafurahi nimefika salama na kupokelewa na Watanzania wenzangu, ikumbukwe wakati napata nafasi hii, nilikuwa mfanyakazi serikalini na tena nilikuwa likizo ya bila malipo.

“Kesho (leo) asubuhi na mapema breki yangu ya kwanza ni kwenda kuripoti kazini kwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ili kunipangia ratiba ya kazi, baada ya hapo ndipo nitajua cha kufanya tena.

“Kutokana na kuthamini mchango wangu, bado nimeteuliwa na Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki Moon, mjumbe wa masuala ya Ukimwi,” alisema Dk. Asha.

Kuhusu kugombea nafasi yoyote ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alikataa na kusema taratibu za UN zinambana mno kutokana na kutoruhusu kugombea nafasi ya kisiasa.

Akizungumzia suala la Katiba mpya, alimpongeza Rais Kikwete kuruhusu mchakato wa kupata Katiba, jambo ambalo limeijengea sifa kubwa Tanzania.

Kuhusu maendeleo, alisema mbali ya nchi mbalimbali kupiga hatua, lakini bado nchi za Afrika, ikiwamo Tanzania zinakabiliwa na changamoto nyingi za kupambana na umasikini kwa wananchi wake.

Akizungumzia juu ya usalama wa nchi, alisema katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, tathimini inaonyesha dunia ilipata amani kubwa, husasan nchi za Afrika.

Alisema Tanzania, imefanikiwa kupiga hatua mbalimbali za kimaendeleo katika nyanja za afya, kisiasa, utawala bora, elimu, masuala ya kijinsia katika uongozi.

Alisema ameamua kurudi nchini, kwa furaha kwa sababu ilikuwa ni siku yake ya kuzaliwa ambapo aliwataka Watanzania kujumuika pamoja kusherehekea.

Dk. Migiro aliwasili nchini na kupokelewa na umati mkubwa, wakiwemo akina mama, viongozi wa Serikali na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa (UN), walioko hapa nchini.

Mapokezi hayo, yaliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, huku kukiwa na askari wengi ambao walikuwa na kazi moja ya kuhakikisha usalama unakuwapo kwa viongozi hao.

Habari Zingine

0 MAOINI :

Fadhili Athumani



EastAfrica Swahili Blogger, Journalist at Mwanaspoti Kenya, Nairobi Kenya, Call: +254705246475, whatsapp:+255654724337, Email: fadhiliathumani85@gmail.com

Proudly Powered by EAMG .