GAMA AWAONDOA HOFU WANANCHI KUHUSU USALAMA WA SIRI ZAO KATIKA SENSA
Posted in
No comments
Sunday, July 29, 2012
By
danielmjema.blogspot.com
Leonidas Gama-mkuu wa mkoa wa kilimanjaro |
MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama amevitaka vyombo
vya Dola kuhakikisha vinaongeza usalama katika kipindi hiki cha sensa kama njia
ya kuondoa wasiwasi uliotanda miongoni mwa wananchi kuhusu usalama wa zoezi
hilo.
Gama Alitoa kauli hiyo katika kikao cha dharura na Waandishi
wa Habari kilichofanyika Ofisini mwake jana kwa lengo la kujadili na kuangazia
mambo mbalimbali ikiwemo zoezi la kuhesabu watu na makazi ambayo imepangwa
kufanyika usiku wa kuamkia Agosti 26.
Alisema ipo haja ya Kamati ya Ulinzi na Usalama katika kila
Wilaya ikishirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha swala la Ulinzi na Usalama
wa Raia unapewa kipao mbele, hasa katika kipindi hiki cha Sensa,
kutokana na kuwepo kwa hofu ya shughuli hiyo kutoa Mwanya kwa wahalifu kuhatarisha
usalama wa Raia.
“Natoa agizo kwa kamati ya Ulinzi na Usalama katika kila
Wilaya kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha kwamba Usalama wa Raia
katika kipindi hiki cha Sensa kinapewa kipaumbele na umuhimu mkubwa kuliko
vipindi vingine vyote,kuna watu wanataka kutumia zoezi hili kutekeleza uhalifu
wao,hilo hatutaliruhusu hata kidogo ” alisema Gama.
Aidha Gama aliwataka wakuu wote wa kila kaya kutunza kumbukumbu
muhimu kama vile Umri, Jina, Jinsia, Kiwango cha Elimu, Uraia, Shughuli za
kiuchumi, mahali anapoishi na kushinda, kama ameolewa au ameowa na watoto, za
watu walioamkia katika kaya yake kutokana na vitu hivyo kuwa mahitaji muhimu katika
kutathmini Maendeleo ya sehemu husika.
Alisema kuwa taarifa zitakazokusanywa kutoka kwa Wananchi zitatunzwa
kwa matumizi yakitakwimu tu kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Namba 1 ya mwaka
2002, hazitatolewa kwa Mtu yeyote Yule na kusisitiza kwamba , Usiri wa Taarifa
hizo utazingatiwa na hivyo kuwaondoa hofu wananchi kuhusu uwezekano wa siri zao
muhimu kuvujishwa kwa matumizi yasiokusudiwa.
“Nawakikishia Wananchi kuwa, Taarifa watakazo toa zitatunzwa
kwa siri na zitatumika kwa Shughuli za
kitakwimu tu, hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu, namba 1 ya mwaka 2002,”alisema
Gama.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, aliwataka Wananchi kuendelea
na Shughuli zao za Kiuchumi kama kawaida wakati wote wa zoezi la kuhesabu Watu
na Makazi kutokana na zoezi hilo kutoathiri shughuli za kiuchumi za Mkoa huku akikemea
vikali Tabia ya Watu kubweteka kwani ili Juhudi za kunyanyua uchumi wa Nchi
zifanikiwe, inabidi watu kujituma kwa Nguvu zote na kwa nyakati zote.
Kwa upande wake, Mratibu wa Sensa Mkoa wa Kilimanjaro, Alex
Luwavi, alibainisha kwamba swala la Usalama wa Wananchi umezingatiwa kwa
kuhakikisha kwamba Makarani wote watapewa Vitambulisho na Sare maalumu zitakazo
watambulisha kama njia ya kuziba mianya inayoweza kutumiwa na Watu wasio waaminifu
na kusabibabisha madhara kwa Jamii.
Pia aliwataka Wawezeshaji wapatao 186, waliomaliza mafunzo yaliochukua
takribani wiki mbili na kufungwa mwishoni mwa wiki hii, kutoa mafunzo kwa Makarani
wote watakaochaguliwa na kuwasisitiza, kufanya kazi kwa uadilifu na kwa Bidii
kutokana na umuhimu na ugumu wa kazi hiyo ili kuwezesha zoezi hili kufanikiwa kwa
asilimia kubwa.
Habari Zingine
Mjulishe Mwenzako
0 MAOINI :